Thursday 21 January 2016

ZIARA RASMI YA KWANZA YA KIKAZI MIKOANI YA MHE.RAIS MAGUFULI

Rais John Magufuli anatarajiwa kuwasili mkoani hapa leo kwa ziara ya kikazi ya siku mbili. Hii ni ziara yake ya kwanza tangu alipoapishwa kushika wadhifa huo Oktoba 25, mwaka jana.

Maandalizi ya kumpokea Rais yalikuwa yamepamba moto jana ikiwa ni pamoja na kupanua barabara inayoingia na kutoka makazi ya Rais jijini hapa.
Katika Ikulu ndogo ya jijini Arusha jana jioni, wafanyakazi walionekana wakiweka mazingira sawa ya kumpokea Rais ambaye atawasili mchana kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (Kia)
Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Felix Ntibenda aliwataka wananchi kujitokeza kwa wingi kumlaki kiongozi huyo.

“Tuonyeshe moyo wa upendo na ukarimu kwani mkoa huu una heshima ya kuwapokea viongozi wa kitaifa na kimataifa na ulinzi umeimarishwa kuhakikisha muda wote kunakuwa salama,” alisema Ntibenda.

Mkuu wa Wilaya ya Arusha Mjini, Fadhili Nkurlu alikagua barabara inayoelekea Ikulu ndogo huku askari polisi wakiwa doria katika barabara zinazoingia na kutoka eneo hilo.
Katika ziara hiyo, Rais Magufuli ambaye pia Amiri Jeshi Mkuu, atatembelea Chuo cha Jeshi cha TMA, Monduli ambako keshokutwa, atawatunuku kamisheni ya uofisa, maofisa wateule wa jeshi.
Iwapo Rais Magufuli atafikia Ikulu ndogo ambayo makazi ya kiongozi wa nchi anapokuwa kwenye ziara mikoani, atakuwa anatendea kazi kauli zake wakati wa kampeni za kupunguza matumizi yasiyo ya lazima.

No comments:

Post a Comment

Maoni yako