Saturday 2 January 2016

MAJANGILI WA WANYAMA PORI KUKIONA CHA MOTO

Mmoja wa Majenerali wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania walioteuliwa kushika nyadhifa nyeti serikalini,Meja Jenerali Gaudence Milanzi,ameanza kazi kwa kutoa tahadhari kwa majangili akisema atatumia mbinu za medani kuwakabili na kuwatokomeza kabisa.

Akizungumza Muda mfupi baada ya kuapishwa mbele ya Rais John Magufuli kuwa Katibu Mkuu Wizara Ya Mali Asili na Utalii,Meja Jenerali Milanzi alisema ni aibu Tanzania kuendelea kupoteza wanyama pori bila hatua stahiki kuchukuliwa.

"Siwezi kuvumilia kuona serikali ikishindwa kusimamia rasilimali za nchi ambazo ndizo zinaoongeza idadi ya watalii nchini na pato la taifa.Majangili wanaongozwa na uchu na uchoyo kwa watanzania wengine.

"Maliasili zilizopo ni kwa ajili ya kuwanufaisha watanzania wote na kuliletea sifa taifa letu.Ni aibu kuonyesha dalili za kushindwa katika mapambano dhidi ya ujangili.Maliasili na utalii ndio kitovu cha mapato ya taifa, kwani wanyama hasa wale adimu ndio huvutia watalii.

"Nitatumia mbinu na uwezo wangu wa kijeshi kukabiliana na hilo,kwa sasa ni mapema kusema lolote.Kuna mambo mengi ninatakiwa nijifunze kwanza,lakini tutaangazia matatizo yote yanayoikabili wizara hii nyeti.

"Kuna masuala ya vitalu vya uwindaji,kuna tatizo la wananchi kuwepo ndani ya hifadhi za taifa;yote tutayaangazia pamoja na kuangalia namna ya kutoa elimu kwa wananchi juu ya uhifadhi na ujangili." Alisema Meja Jenerali Milanzi.
Mhe.Meja Milanzi siku akila kiapo

No comments:

Post a Comment

Maoni yako