Saturday 7 March 2015

DAKTARI FEKI, ASKARI FEKI, SASA "PADRE FEKI"

Jeshi la Polisi mkoani Morogoro, linamshikilia mkazi wa Manispaa hiyo, Josephat Asenga (47), mwenye taaluma ya uhasibu, kwa tuhuma za kujifanya Padri.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Leonard Paulo, alisema kuwa, Asenga alikamatwa juzi saa 10:30 jioni, katika maeneo ya Modeco, Kata ya Mazimbu katika Kanisa Katoliki Parokia ya Mtakatifu Maria.

Kwa mujibu wa Kamanda Paulo, mtuhumiwa huyo alifika parokiani hapo Juni mwaka jana akiwa amevaa mavazi ya Padri na kujitambulisha kwa Paroko wa parokia hiyo, Malt Dyfrig Joseph, kuwa yeye ni Padri anaishi Jimbo la New York Marekani.
Kwa mujibu wa kamanda huyo, baada ya kujitambulisha kwa Paroko huyo na kuonesha kitambulisho chake, alimuomba Paroko huyo kumpangia zamu ya kuendesha Misa ya Jumapili iliyofuata na kukubaliwa na Paroko huyo bila kukagua vizuri kitambulisho chake.

Alisema mara baada ya misa hiyo, Paroko alipata taarifa kutoka kwa msamaria mmoja wa Kituo cha Amani cha Chamwino mjini hapa, kuwa Padri huyo feki anaishi na mwanamke katika maeneo ya Ujenzi kinyume na taratibu za upadri.
Baada ya kupata taarifa hizo, inadaiwa Paroko huyo aliwaomba waumini wamshawishi Padri huyo feki, afike parokiani hapo na baada ya kufika, alihojiwa na Paroko huyo na kudai kuwa alipata upadrisho katika Jimbo Kuu Katoliki Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa kamanda huyo, baada ya Paroko huyo kupata maelezo hayo alifanya mawasiliano na Katibu wa Jimbo hilo la Dar es Salaam na kujibiwa kuwa hakuna jina la Padri huyo.
Juzi Alhamisi majira ya saa 10:30, Padri huyo feki alimpigia simu Paroko huyo na kumuomba ampange kuendesha Misa Takatifu ya Jumapili parokiani hapo, na kukubaliwa na paroko huyo na kumtaka afike kanisani.
Kwa mujibu wa Kamanda huyo, baada ya kufanya mahojiano na mtuhumiwa, alikiri kuwa yeye sio Padri na walipokwenda nyumbani kwake kwa ajili ya kufanya upekuzi, walimkuta akiwa na majoho saba ya upadri.
Mtuhumiwa huyo ameendelea kushikiliwa Polisi na atafikishwa mahakamani mara baada ya upelelezi kukamilika

1 comment:

  1. Habari imekosa picha ya huyo pandri,huenda ameliza wengi akitumia majina tofauti

    ReplyDelete

Maoni yako