Thursday 18 June 2009
TUJIKUMBUSHE HAYA......
NGUZO TANO ZA UJAMAA - KWA MUJIBU WA JULIUS K. NYERERE, SABA SABA 1970
1. 'WATU WOTE NI SAWA'"...
Kama hukubali hilo, yaani kama unadhani watu wengine ni miungu wengine, malaika, wengine nusu-nyani, basi hukubali ujamaa. Ujamaa kwako hauna maana, kwa sababu ujamaa unahusu usawa wa watu: hapo ndipo unapoanza...Sisemi usawa wa urefu wala ufupi; kwa urefu namzidi Kawawa, sana tena. Sisemi maguvu, hata; nasema utu, watu, na ubinadamu wao. Kuna binadamu zaidi ya mwenziwe? Kama huliamini hilo, utakuwa mjamaa? Hilo la kwanza... mkaliulize-ulize, mlielewe maana yake. Na mtu anayepinga ujamaa naye ajiulize kama anapinga hilo nalo. Mtu mpingaji ujamaa aseme, 'Hilo nalo, usawa wa watu, napinga; kwamba binadamu wote hivi si sawa'" - Mwalimu Julius K. Nyerere
2. 'LAZIMA MTU AFANYE KAZI'
"...Binadamu hao unaotuona hapa, na hao waliosambaa dunia nzima wanaishi kwa kazi. Hawana namna nyingine ya kuishi. Wakiacha kufanya kazi watakufa; hawana namna nyingine; kuishi kwao, na kuendelea kuishi, lazima wafanye kazi...Lakini binadamu haishi kama farasi. Binadamu haridhiki kuishi kama farasi au punda; binadamu ana kitu anakiita maendeleo; lazima aendelee...Wakati mwingine ili kusudi maendeleo haya yaje wana shughuli za kupigana misasa akili, wanapanuana mawazo tu, nayo ni kazi...nendeni mkaulizane...kama kazi si kitu cha lazima, kama binadamu anaweza kujikalia tu hafanyi kazi, akaishi, na maendeleo yakaja bila kazi. Na huyo anayepinga ujamaa naye ajiulize kama hilo analipinga? Na hilo la kufanya kazi analipinga au kuna jingine analopinga?" - Julius K. Nyerere
3. 'HAKUNA MTU KUMNYONYA MTU'"...
Kama binadamu ni sawa, tunalikubali hilo...Pili tunasema kitu kazi ni jambo la lazima kwa kila mtu, hakuna aliyesamehewa kazi. Basi siwezi kukufanyia kazi. Kukufanyia kazi maana yake ni kwamba wewe unasamehewa kazi! Siwezi kukufanyia kazi. Wewe utafanya kazi, na mimi nitafanya. Sio mimi nifanye, wewe hufanyi; lazima ufanye kazi. Kwa hiyo wewe utafanya kazi, na mimi nitafanya kazi; kila mtu atafanya kazi. Yaani namna ya kulitamka hilo ni kwamba kunyonyana hakuna. Hakuna mtu kumnyonya mtu; sasa tena msingi wa kumnyonya unatoka wapi? Tumesema watu sawa; na mtu ili aishi hana budi afanye kazi, na kazi ndio msingi wa maendeleo. Sasa mwanachama... ajiulize kama anaweza kuwa mjamaa na huku ananyonya! Unamnyonya mkeo; mkeo anakwenda kufanya kazi wewe unakwenda kupiga chibuku; hivi kweli mjamaa wewe? Tunasema kazi jambo la lazima, lakini wewe hufanyi kazi, unamnyonya mkeo. Wewe mjamaa? Nasema na hilo mjiulize...Unaweza kuwa mjamaa na huku unanyonya? Na anayepinga ujamaa ajiulize hilo nalo analipinga, kwamba yeye anaona kunyonya ni sawa tu! Sawa yeye kunyonya mwingine au wengine kumnyonya yeye, huyu anayesema kunyonya ni sawa. Kama kunyonya ni sawa baba, sasa tuanze kunyonya, au mkuki kwa nguruwe?" - Julius K. Nyerere
4. 'VYOMBO MUHIMU VIMILIKIWE PAMOJA'
"...Kama watu ni sawa; binadamu wote ni sawa; kazi ni jambo la lazima kabisa; kunyonya ni haramu; la nne linafuata: Vyombo vyote vya lazima, vinavyohitajika kwa maisha ya binadamu kwa kufanyia kazi lazima vimilikiwe kwa jumla. Ardhi lazima imilikiwe kwa jumla maana tusipoimiliki ardhi kwa jumla tutamwachia Rashidi Kawawa na Sheikh Karume wao wawe ndio wenye ardhi, na ardhi ni kitu cha lazima kwa maisha, hebu tuone kwanza usawa utakuwaje. Itakuwa lazima twende kwa Rashidi na kwa Karume, 'tafadhali bwana nataka ardhi'. Umekwishamwita 'Bwana' huyu; usawa umekwisha. Lakini vilevile kama Sheikh Kawawa ana ardhi, na Sheikh Karume ana ardhi, hawa hawalazimiki kufanya kazi. Kwa nini wafanye kazi? Hawawezi kufanya kazi. Tumesema kazi ni kitu cha lazima kwa kila mtu, lakini hawa hawawezi kufanya kazi, watakaa tu wanatutoza kodi kwa ardhi yao. Ndiyo wanatunyonya hivyo tena. Mimi nafanya kazi; mimi nalima. Halafu Rashidi anasema, 'Ukishalima mahindi ukapata magunia matano, moja langu'. Ndio ananyonya hivyo. Anavunja kanuni ya usawa; anavunja kanuni ya kazi; anavunja kanuni ya kutonyonya. Kwa nini? Kwa sababu tumemruhusu amiliki yeye vitu ambavyo vinastahili viwe vya wote. Mtu ambaye yeye ana ardhi; umemkabidhi viwanda, ukishakuwa umemkabidhi majambo mengine haya, umemwongezea nguvu zake, yeye utu wake umeongezeka-ongezeka na wangu mimi umeupunguza-punguza. Kwa hiyo vitu vilivyo vya lazima kwa kila mtu, kama ardhi ambayo ni ya lazima kwa kila mtu, lazima vimilikiwe na wote. Sasa...mjiulize kama unaweza kuwa mjamaa kweli huku unajidai ardhi yangu? Na wanaopinga wanatakaje? Hao wanaosema ujamaa mbaya. 'Eti vitu vyote viwe vya ujumla'; wengine waongo, 'Eti wanasema hata wakina mama wawe wa jumla'. Tunasema ardhi, hatusemi kina mama, tunasema ardhi viwanda, madini: kwa nini mtu mmoja anakwenda kuvinyakua vikawa vyake hivi!" - Julius K. Nyerere
5. 'KUUNDA NCHI BILA MATABAKA'
"..Kama tunakubali kuwa watu wote ni sawa; na watu wote ni lazima wafanye kazi, mtu asimnyonye mtu; na mali, mali kubwa, sikusema shati langu liwe la Rashidi: misingi ya uchumi kama mabasi yale yanapita iwe kwamba tunasema mabasi yetu, asiweko mheshimiwa mmoja pale anasema 'Basi langu lile!' Basi lako! Yupo dereva mle anaendesha, anasema dereva wake! 'Dereva wangu' - dereva wako, wewe unaweza kuwa na dereva? Dereva anaweza kuwa dereva wa umma, sio dereva wako. Dereva ni sawa sawa na mwalimu; mwalimu wa umma, daktari wa umma, dereva wa umma. Huyu anakuwaje 'wako'? Hata askari siku moja utasema wako. Kama tunakubali watu wote ni sawa; watu wote lazima wafanye kazi, hakuna kunyonyana; mali,vitu vyote vile vya jumla lazima viwe vya umma; maana yake ndio kusema tunataka kuunda nchi ambayo haina tabaka: hakuna mabwana na watwana." - Julius K. NyerereNUKUU ZIMETOKA KWENYE UJAMAA NI IMANI: MOYO KABLA YA SILAHA, 1973: EAPH
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment
Maoni yako