Wednesday 31 August 2016

MHE RAIS MAGUFULI ATEUA KATIBU MKUU MPYA WIZARA YA FEDHA NA MIPANGO

CHADEMA WASITISHA MAANDAMANO YA UKUTA

Mwenyekiti wa chama cha Demokrasia na Maendeleo,Freeman Mbowe ametangaza kusitishwa kwa maandamano ya Oparesheni UKUTA yaliyokuwa yamepangwa kufanyika kesho nchi nzima hadi tarehe moja Octoba.

Akizungumza na wanahabari leo, makao makuu ya chama hicho, Mtaa wa Ufipa, Kinondoni jijini Dar es Salaam, Mbowe amesema, Chadema inalazimika kuahirisha maandamano na mikutano ya kesho kutokana na kuheshimu wito wa viongozi wa dini zote waliowaomba.

“Viongozi wa dini zote hapa nchini kuanzia, Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri (KKKT), Mkuu wa Kanisa la Kianglikana Tanzania, Rais wa Baraza la Maaskofu (TEC), Katibu Mkuu wa Baraza la Kikristo Tanzania (CCT), Mkuu wa Kanisa la African Inland Church Tanzania (AICT), Katibu Mkuu wa Baraza la Makanisa ya Kipentekoste (CPCT), Mufti Mkuu wa Baraza Kuu la Waislamu (BAKWATA) na Mufti Mkuu wa Zanzibar, wametusihi tuahirishe ili wao wazungumze na Rais John Magufuli kutafutia suluhu suala hili,” amesema Mbowe.

Mbowe amezitaja taasisi na watu wengine wenye heshima kubwa ndani na nje ya nchi waliokiomba chama hicho kuahirisha maandamano na mikutano hiyo kuwa ni Mzee Joseph Butiku ambaye ni Mwenyekiti wa Tasisi ya Mwalimu Nyerere, Jukwaa la Katiba Tanzania (JUKATA), Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) pamoja na mjane wa Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere Mama Maria Nyerere ambaye alizungumza na Edward Lowassa kwa niaba ya chama hicho.

“Kwa heshima ya viongozi wetu wa dini na taasisi hizi, tunawatangazia wanachama wetu kote nchini kuwa tunaahirisha maandamano hayo kwa muda wa mwezi mmoja ili kuwapa nafasi viongozi hawa waonane na Rais Magufuli na kama asipowaelewa hata hao, sisi tusilaumiwe,” amesisitiza Mbowe

Bw.GERSON MSIGWA ATHIBITISHWA NA RAIS MAGUFULI KUWA MKURUGENZI WA MAWASILIANO IKULU

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli, amemthibitisha Bw. Gerson Partinus Msigwa kuwa Mkurugenzi wa Kitengo cha Mawasiliano ya Rais, (Director of Presidential Communication - DPC).

Taarifa iliyotolewa leo Jumatano Agosti 31,2016 na Katibu Mkuu Ikulu Bw. Peter Ilomo imeeleza kuwa Bw. Gerson Partinus Msigwa amethibitishwa kuanzia leo tarehe 31 Agosti, 2016 kushika wadhifa huo.

Kabla ya uthibitisho huo, Bw. Gerson Partinus Msigwa alikuwa Kaimu Mkurugenzi wa Kitengo cha Mawasiliano ya Rais, katika Ofisi ya Rais Ikulu kuanzia tarehe 17 Novemba, 2015.

Jaffar Haniu
Kaimu Mwandishi wa Habari wa Rais Msaidizi.
Dar es Salaam
31 Agosti, 2016

Tuesday 30 August 2016

NDEGE ZILIZONUNULIWA NA TANZANIA HUKO CANADA KUWASILI NCHINI MUDA WOWOTE SEPTEMBA

Hii ndio moja ya ndege mpya ya Air Tanzania iliyo tayari kwa kila kitu.Hapa ipo kwenye Hangar(eneo la matengenezo ya ndege) nchini Canada tayari kwa kuanza safari ya kuja Tanzania.Wakati wowote na siku itakayotajwa ya mwanzoni mwa mwezi September ndege hizi mbili zitatuwa katika uwanja wa Kimataifa wa Julius Nyerere Dsm.
Hakika ndege hizi ni rafiki kwa mazingira ya viwanja vya Tanzania na usafiri wa ndani.Itasaidia kutua hata katika viwanja "korofi" kama Mtwara,Kigoma,Tabora,Iringa,Songea,Dodoma(japo nasikia inafanyiwa ukarabati) na viwanja vingine kama Arusha,Mwanza,Znz,Tanga na Mbeya.
WELCOME TO THE MARKET ATCL.....THE WINGS OF THE KILIMANJARO

MHE AUGUSTINE MREMA AWAOMBEA KAZI MATEJA

Mwenyekiti wa Bodi ya Taifa ya Palore nchini, Dkt. Augustino Lyatonga Mrema, amemwomba Rais Dkt. John Pombe Magufuli kuongeza maeneo ya kutoa tiba ya kuachana na matumizi ya dawa za kulevya.

Sambamba hilo, Mrema amemuomba Rais kuwasaidia wahanga wa dawa za kulevya waliopatiwa tiba kurejea katika shuguli za kuzalisha uchumi.

Akiongea na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam kuhusiana na changamoto wanazokutana nazo wahanga wa dawa za kulevya nchini, Dkt. Mrema amelitaka jeshi la polisi kuacha mara moja kuwanyanyasa waathirika wa madawa hayo huku akimtaka Rais Dkt. John Pombe Magufuli kuwapatia ajira pindi wanapoacha kutumia madawa hayo.

Naye Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Akili kutoka Hosptali ya Taifa Muhimbili Kitengo cha Madawa ya Kulevya Dkt. Cassian Nyandindi amesema ni vyema serikali ikajenga maeneo mengine nchini ya kutoa huduma ya matibabu kwani maeneo matano pekee yaliyopo nchini hayatoshi kuweza kuwahudumia waathirika hao ambao wanaongezeka kila siku.

EATV ilifanya mahojiano na baadhi ya waathirika wa dawa za kulevya ambao wamelilalamikia jeshi la polisi kuchukua fedha zao huku kila mara wakiwahusisha na kuuza dawa za kulevya ambazo tayari wameacha kutumia.

Monday 29 August 2016

VIONGOZI WA CHADEMA WASHINDWA KUFANYA KIKAO CHAO LEO

Viongozi wa Chadema wamekamatwa na polisi na kupelekwa Kituo Kikuu cha Polisi Dar es Salaam kwa ajili ya mahojiano.

Akizungumzia kukamatwa kwa viongozi hao Mwanasheria Mkuu wa Chadema, Tundu Lissu alisema; “Tulikuwa kwenye kikao cha Kamati Kuu kilichojumuisha wajumbe na wabunge kwa ajili ya kujadili masuala mbalimbali ya chama. Jumla ya wajumbe walikuwa 170. Tukiwa kwenye kikao walikuja watu wanasema tunatakiwa polisi kwa sababu tumekiuka agizo lililokataza mikutano.”

Waliotakiwa kufika makao makuu ya polisi, ni pamoja na mwenyekiti wa chama hicho taifa, Freeman Mbowe; mjumbe wa Kamati Kuu na waziri mkuu mstaafu, Edward Lowassa; Katibu Mkuu, Vicenti Mashinji na naibu katibu mkuu (Bara), John Mnyika.

Mkutano wa kamati kuu ya Chadema, umeitishwa ili kujadili ufanikishaji wa maandamano ya oparesheni UKUTA.

Sunday 28 August 2016

KUTOKA MAGAZETINI

JUBILEI YA NDOA YA MHE MZEE MKAPA YAWAKUTANISHA MHE RAIS MAGUFULI NA MHE LOWASSA

Rais Magufuli amesema anashukuru hafla ya Jubilei ya Miaka 50 ya ndoa ya Rais mstaafu Benjamin Mkapa kuleta muujiza wa kukutana na kupeana mkono na Waziri Mkuu wa zamani, Mhe Edward Lowassa

Friday 26 August 2016

HONGERA DIAMOND KWA KUITANGAZA TANZANIA

Endelea kuwaambia popote uendapo "Wanakaribishwa Tanzania"
Diamond Platnumz alipowasili nchini Kenya jana

Thursday 25 August 2016

VIDEO: WASANII WAUNGANA KUPINGA "UKUTA"

CHEKA NA WAGENI

Wageni wa siku hizi wazuri, sio wasumbufu kama wa zamani. Wakifika kwako hawaulizi chai ya rangi, juice wala soda, bali utasikia, "UNA CHARGER YA PIN NDOGO?"

Wednesday 24 August 2016

WAPI TUNAELEKEA?: ASKARI POLISI WAUAWA NA MAJAMBAZI WAKIWA KATIKA LINDO CRDB BANK MBAGALA

Jeshi la Polisi limethibitisha kuwa jumla ya askari wake wanne wameuawa usiku wa kuamkia leo baada ya majambazi kuvamia tawi la benki ya CRDB lililopo Mbande, wilayani Temeke, Dar es Salaam.

Akizungumza moja kwa moja kupitia kituo cha Redio One Stereo leo asubuhi, Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Simon Sirro, amesema watu kadhaa wamekamatawa na msako unaendelea ili kuwapata waliotekeleza unyama huo. Sirro amesema taarifa kutoka eneo la tukio zinaonesha kuwa majambazi hao walikuwa 14 na baada ya kufanya mauaji hao, walivamia kituo cha polisi cha Mbande kisha wakavunja stoo na kuchukua sare ya askari na silaha.

Akielezea namna tukio hilo lilivyotokea, Kamanda Sirro amesema wahalifu hao walitumia mwanya wakati askari wakibadilishana lindo katika taasisi hiyo ya fedha na kuibuka ghafla na kuanza kurusha risasi. Kwa mujibu wa Sirro, gari la polisi limechakazwa kwa risasi na askari mmoja aliyekuwa lindo alifanikiwa kukimbia na ndiye aliyeweza kutoa taarifa na maelezo ya namna tukio lilivyofanyika.

“Watu kadhaa wamekamatwa na tunaendelea na msako. Tunawataka wakiwa hai au wafu,” amesema Kamanda Sirro huku akiwataka watu kujihadhari na yeyote anayejitambulisha kwao kuwa ni askari bila kuonesha kitambulisho.

Ameendelea kusema kuwa baada ya operesheni ya kukomesha mtandao wa wahalifu kama hao na wengine kukimbilia nchi jirani, masalia wameanza kujikusanya na kutekeleza matukio ya mauaji huku askari wakiwa ndio walengwa.
Aidha CP Mssanzya aliwataja askari waliouawa katika tukio hilo wakati wakibadilishana lindo kuwa ni E.5761 CPL Yahya, F.4660 CPL Hatibu, G 9524 PC Tito na G 9996 PC Gastoni na raia wawili waliojeruhiwa aliowataja kuwa Ali Chiponda na Azizi Yahya wote wakiwa wakazi wa Mbande.

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mhe.Mwigulu Nchemba alifika katika eneo lilikofanyika tukio hilo na kumjulia hali Raia aliyejeruhiwa

Tuesday 23 August 2016

MHE LOWASSA ASHINDWA KUFANYA KIKAO HUKO MBEYA

Aliyekuwa Waziri Mkuu wa Tanzania na Mjumbe wa Kamati Kuu ya CHADEMA, Edward Lowassa leo amezuiwa na Polisi kufanya kikao cha ndani na wanachama cha chama hicho Mbarali mkoani Mbeya.
Aliyekuwa Waziri Mkuu wa Tanzania na Mjumbe wa Kamati Kuu ya CHADEMA, Edward Lowassa leo amezuiwa na Polisi kufanya kikao cha ndani na wanachama cha chama hicho Mbarali mkoani Mbeya.

UDAKU WA LEO

"Aliyekutoa mwiba wa makalio mthamini, ndiye anakupa jeuri ya kukaa kitako ukautoa mwiba wa mguuni". - Bi Hindu

Monday 22 August 2016

VIDEO: MBUNGE WA ARUSHA MHE GODBLESS LEMA(CHADEMA) ASEMA HAYA KUELEKEA "UKUTA"

MHE.LOWASSA ASISITIZA "UKUTA"

Leo nimezunguka katika majimbo ya Mbeya Vijijini ,Vwawa na Tunduma nikiwaeleza kuhusu Operation UKUTA,

UKUTA si fujo , UKUTA si machafuko na hatuna haja ya kufanya fujo , tunapiga kelele dhidi ya uvunjwaji wa haki ya kidemokrasia na katiba ya nchi unaofanywa na utawala huu wa awamu ya tano .

CHADEMA ni nani wakapambane na polisi ,polisi ambao ni watoto wetu ,ndugu zetu na hata wake na waume zetu ila tuwahakikishie hatutorudi nyuma pale katiba na haki ya kidemokrasia ikichezewa au kuwa chini ya mtu fulani .

Najua polisi watapiga watu ,wataumiza watu na hata kuua ila niwahakikishie wao na walio na mamlaka wataishia katika mahakama ya Kimataifa .

Siasa ni mazungumzo ,lazima tuzungumze milango yetu iko wazi kufanya mazungumzo ila kwa kuwa hawahitaji na sisi hatutorudi nyuma September Mosi ,tumejiandaa vya kutosha na sasa tuko ngazi ya kaya na wajumbe wetu wanakamilisha kazi katika kaya ili tarehe mosi sauti ya kutosha ipazwe kwa maandamano na mikutano kama tulivyokubaliana katika kata zetu na majimbo nchi nzima .

Haiwezekani hata kidogo mtu mmoja azuie kila kitu ,nchi hii ni mali yetu sote na inaongozwa na Katiba na sheria.

Kamati kuu ilipoamua katika suala la UKUTA haikukurupuka , kamati kuu yetu inaundwa na mchanganyiko wa wasomi wa kada mbalimbali ,wazee wenye busara na vijana machachari kamwe hawawezi kukukurupuka na UKUTA ni haki ya watanzania wote.

Pili naomba niwape siri ya ushindi 2020 ndugu zangu na wanachama wenzangu , tutashinda uchaguzi Mkuu 2020 kama tutafanya yafuatayo na kuyasimamia
Kwanza; Umoja ndani ya Chama na wanachama ,tuheshimiane ,tusameheane na tuimarishe chama chetu
"chama ndani ya Chama , chama nje ya chama na chama ndani ya Umma "- LOWASSA

TSHIRTS ZA KUHAMASISHA "UKUTA" ZAKAMATWA JIJINI DAR

Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam limesema limejiandaa kudhibiti maandamano ya Umoja wa Kupambana na Udikteta Tanzania (Ukuta) yaliyoandaliwa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) yanayotarajiwa kufanyika Septemba Mosi mwaka huu.

Wakati akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam, Kamanda wa Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam Simon Sirro amewatoa hofu wakazi wa mkoa huo kuwa hakuna mtu na au kikundi chochote cha watu kitakachofanya maandamano siku hiyo.

“Habari ya Ukuta haipo,umeshabomoka na kama haujabomoka utabomoka, wakazi wa Dar es Salaam msiwe na hofu, fanyeni kazi na hata siku hiyo hakuna mtu atakayejitokeza barabarani kuandamana,” amesema.

Kamanda Sirro amedai kuwa siasa zinatakiwa kufanywa kwa amani na utulivu na kwamba wanasiasa wanaoitumia siasa kufanya vurugu hawatafanikiwa.

“Mimi niwahakikishie kwamba tunajiandaa kwelikweli kuhakikisha watu wanafuata sheria , anayetaka kuvunja sheria kwa kufanya maandamano aanze yeye ili nasi tuanze naye,” amesema.

Ameongeza kuwa ” Suala la utii wa sheria ni la msingi,kama kuna watu au kikundi cha watu kinataka kuitumia siasa kufanya uvunjifu wa amani wajue kwamba nafasi hiyo kwa Dar es Salaam haipo.”

Aidha,Kamanda Sirro amesema August 20 2016 Jeshi la Polisi lilipata taarifa toka kwa raia wema kuwa maeneo ya Kinondoni kuna duka linauza flana zenye maneno ya uchochezi yaliyoandikwa ‘’TUJIPANGE TUKATAE UDIKITETA UCHWARA’’ , ‘UKUTA’ ‘

Amesema Polisi baada ya kupata taarifa hizo walifika eneo la tukio na kumkamata mtuhumiwa aitwaye YORAM SETHY MBYELLAH miaka 42, mfanyabiashara na mkazi wa Mburahati akiwa anauza fulana hizo dukani kwake.

KICHEKO CHA LEO: INAYOSTAHILI KUITWA "BREAKFAST"

MASHINDANO YA OLIMPIKI RIO 2016 YAMALIZIKA HUKO BRAZIL

Rio imemaliza michuano ya Olimpiki kwa shamrashamra za aina yake, licha ya mvua kuwanyeshea maelfu wanamichezo pamoja na watazamaji waliofika kushuhudia michezo hiyo kutoka maeneo mbalimbali duniani.
Mwenge wa Olimpiki umezimwa katika uwanja wa Maracana nchini Brazil, na kuashiria michuano ya Olimpiki Rio imemalizika rasmi:
Mashindano ya Olimpiki yanayofuata yatafanyika huko nchini Japan.

Sunday 21 August 2016

CHADEMA: OPERESHENI UKUTA IPO PALE PALE SEPTEMBA MOSI

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimeendelea kushikilia msimamo wa kuendeleza operesheni UKUTA Septemba mosi mwaka huu.

Mbunge wa Kawe, Halima Mdee, alisema kwenye Baraza la Mashauriano la Kanda ya Pwani, lililofanyika jana Dar es Salaam kuwa wataitaarifu Polisi kuhusu maandamano yao watakayoyafanya bila kubeba silaha ili wapewe ulinzi.

Kwa mujibu wa Mdee ambaye ni Mwenyekiti wa Baraza hilo kwa Kanda ya Pwani, hawategemei kufanya fujo katika maandamano hayo, bali watatekeleza wajibu wao wa kudai demokrasia ambayo ni haki yao ya kikatiba, huku wakiwa wamejifunga vitambaa vyeupe mkononi na fulana nyeusi.

“Atakayefanya fujo katika maandamano hayo hayo Polisi watakuwa na haki ya kumkamata, vinginevyo tutadai haki yetu ya kidemokrasia ya kufanya mikutano na shughuli za kisiasa kwa njia ya amani”, Mdee alisema.

Wapinzani wamedhamilia kufanya maandamano hayo, licha ya Rais Magufuli kupiga marufuku maandamano na mikutano ya kisiasa isiyo na lengo jema ikiwemo ya viongozi kutoka kwenye maeneo yao kwenda kufanya mikutano kwenye maeneo mengine, jambo linalopingwa na Chadema kwa maelezo kuwa ni ukiukaji wa demokrasia.

BRAZIL YAITOA UJERUMANI KWA PENATI KATIKA FAINALI ZA OLYMPICS HUKO RIO

Timu ya Taifa ya Soka Olympics 2016 ya Brazili imeshinda Medali za Dhahabu baada ya kuitoa Ujerumani kwa Penati. Timu hizo ambazo zilimaliza muda wa kawaida kwa droo ya 1 - 1 iliongezewa dakika 30 na ikabaki 1-1 ndipo zikapiga penati na Brazil ikapata 5 Ujerumani 4. Penati ya ushindi ilifungwa na mchezaji machachari Neymar.

Saturday 20 August 2016

SIMBA SPORTS CLUB WAZINDUA UJENZI WA UWANJA WA KLABU YAO HUKO BUNJU B DAR ES SALAAM

Aliyekuwa mwenyekiti wa Simba, Hassan Dalali akizindua ujenzi wa Uwanja huo huko Bunju B nje kidogo ya Jiji la Dar

ANGALIA JESHI LETU LIKIJIWEKA FIT KIMAZOEZI

TIMU YA TAIFA SOKA WANAWAKE UJERUMANI YATWAA MEDALI ZA OLYMPICS HUKO BRAZIL

Timu ya soka wanawake ya Ujerumani ilitinga fainali na kucheza na Sweden hapo jana usiku saa za Afrika Mashariki katika uwanja wa Maraccana huko Rio Brazil. Timu hiyo ilishinda kwa magoli 2 kwa 1 na hiyo kutwaa medali za dhahabu katika mashindano hayo
Timu ya sweden wakati wa Upokeaji Medali za silver
Timu ya Ujerumani wakati wa upokeaji wa Medali za Dhahabu

Friday 19 August 2016

MKUU MPYA WA MKOA WA ARUSHA AAPISHWA

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akimuapisha Mrisho Gambo kuwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha Ikulu jijini Dar es Salaam.
Rais Dkt. John Pombe Magufuli akiwa katika picha na Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa pamoja na Mkuu mpya wa Mkoa wa Arusha Mrisho Gambo mara baada ya tukio la Kiapo Ikulu jijini Dar es Salaam. Wengine katika picha ni Katibu Mkuu Kiongozi Balozi John Kijazi wa kwanza (kulia) na Naibu Waziri, Ofisi ya Rais Tawala za mikoa na Serikali za Mitaa TAMISEMI Selemani Jafo wa kwanza (kushoto)

WENZANGU NA MIMI MNAKUMBUKA PIPI GOLOLI (PEREMENDE)?

Thursday 18 August 2016

JE WAJUA: WALIOWAHI KUJARIBU KUSHIKA SHARUBU ZA SIMBA ("Mwl Nyerere") NA MATOKEO YAKE

1. Idd Amini – Alipoivamia Tz. Mwalimu alitamka tutampiga nduli!. Na kweli Idd Amini alipigwa hadi akaikimbia Uganda.

2. Kolimba – Alipotamka CCM imepoteza Dira na Mwelekeo. Mwalimu alimwita Dodoma akamuuliza nani kakutuma useme hivyo?! Ndio ukawa mwisho wa Kolimba!.

3. Samweli Sitta – Alipokuwa kiongozi wa serikali ya wanafunzi UDSM aliongoza mgomo wa wanafunzi wenzake kudai siagi na maziwa!. Mwalimu aliibuka pale chuoni akamuuliza Samweli Samweli kwenu mnakunywa maziwa kweli?!. Akamwambia lala chini, akamcharaza bakora na mgomo ukaishia hapo hapo!.

4. Aboud Jumbe – Alipotaka serikali tatu! Nyerere alimuuliza moja kujumlisha moja ni ngapi?! Jumbe akajibu ni mbili!. Nyerere akamwambia kama ni mbili mbona unataka serikali tatu?!.. Huo ndio ukawa mwisho wa Abdul Jumbe kuwa Rais wa Zanzibar!

5. John Samwel Malecela – Ni baada ya taarifa kuzagaa kuwa amebadili dini na jina ili apate kuungwa mkono na nchi za kiislamu kugombea Urais mwaka 1995! Nyerere alimwambia wee John wewe umeenda Arabuni mara moja umebadilisha jina sasa unaitwa Jumanne! Ukienda mara ya pili si utabadilisha kabila?! Huo ukawa mwisho wa ndoto zake kuwa Rais wa Tanzania !

6. Edward Lowassa – Alipokodi ndege binafsi ikampeleka hadi dodoma kwenye vikao vya mchujo wa wagombea Urais kupitia CCM mwaka 1995 alimpa lift JK!.. Nyerere alimuuliza mmekuja na Ndege dodoma pesa mmetoa wapi?! Jina la Lowassa likakatwa kabla ya vikao vya mchujo! Natamani Nyerere angekuwepo sasa na mwaka 2015!

Wednesday 17 August 2016

CHEKA UNENEPE

KIONGOZI MAARUFU DUNIANI: BABA WA MFANO

Rais wa Marekani Mhe. Barack Obama alipomtembelea binti yake wa kike Sasha eneo anakofanya kazi na kuamua kumsadia kazi

Tuesday 16 August 2016

ORIGINO KOMEDI MATATANI KWA KUVAA SARE ZINAZOFANANA NA ZA POLISI HARUSI YA MASANJA

Katika siku za hivi karibuni, kumejitokeza tabia kwa baadhi ya watu wakiwemo wasanii watu wengine mmoja mmoja kutumia mavazi yanayofanana na sare za Majeshi ya Ulinzi na usalama hapa nchini likiwemo Jeshi la Polisi katika shughuli zao za kisanii au katika kazi mbalimbali, Jambo ambalo ni kinyume cha sheria, kanuni na taratibu za Nchi.

Kwa mujibu wa Sheria ya kanuni za makosa ya Jinai, sura ya 16 na marejeo yake ya mwaka 2002, kifungu cha 178 (1) na (2) kinachozungumzia makosa dhidi ya sare za majeshi ya ulinzi na usalama, kinabainisha wazi kuwa ni kosa kisheria kwa mtu yeyote ambaye siyo mtumishi wa majeshi ya ulinzi na usalama kuvaa mavazi yanayotumiwa au kushabihiana na sare za majeshi hayo bila kibali kutoka kwa Mhe.Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Kufuatia kitendo kilichofanywa na kundi la kisanii la “ Original Comedy” kuvaa mavazi yanayoshabihiana na sare za Jeshi la Polisi, Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar Es Salaam linachukua hatua za kisheria dhidi ya wasanii hao.

Aidha Jeshi la Polisi nchini, linatoa onyo kali kwa mtu ama kikundi chochote kuacha kutumia mavazi yanayofanana na sare zinazovaliwa na majeshi ya ulinzi na usalama hapa nchini na atakayebainika hatutasita kuchukua hatua kali za kisheria dhidi yake.

Jeshi la Polisi linatoa rai kwa wale wote wenye mavazi yanayoshabihiana na sare za majeshi ya ulinzi na usalama kuzisalimisha mara moja katika vituo vya Polisi vilivyokaribu nao.

Imetolewa na:
Advera John Bulimba – Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP)
Msemaji wa Jeshi la Polisi.

Makao Makuu ya Polisi.

MHE RC MAKONDA: BAKWATA KUPATA JENGO JIPYA LA MAKAO MAKUU YAO

MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda amekabidhi ramani ya jengo la Ofisi ya Makao Makuu ya Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA), ikiwa ni ahadi ya kuwajengea jengo hilo.

Akizungumza wakati akikabidhi ramani hiyo, Makonda alisema jengo hilo linatarajiwa kuwa na ghorofa tatu na litagharimu zaidi ya Sh bilioni tano.

“Ijumaa nitakuja hapa kwa ajili ya kuweka jiwe la msingi na niseme tu ujenzi utaanza hivi karibuni na nimeshawaambia watu wangu wahakikishe jengo hilo linajengwa kwa muda usiozidi miezi 14 tu,” alisema Makonda.

Licha ya kukabidhi ramani hiyo, Makonda pia aliwataka viongozi hao wa dini kuendelea kuhubiri amani ili taifa liendelee kuwa na amani na mshikamano. Alisema ujenzi wa jengo hilo, umekuja baada ya kuona kuwa Bakwata imekuwa na mchango mkubwa kwa taifa ikiwemo kuhubiri amani na mshikamano.

“Viongozi wa dini ni watu muhimu sana wamekuwa wakituhubiria amani na pia viongozi hao wamekuwa wakituongoza katika safari ya kutupeleka kwa mola, endeleeni kudumisha na kuihubiri amani ili taifa ili liendelee kusifika,” alisema Makonda.

Kwa upande wake, Mufti wa Tanzania, Shehe Mkuu Abubakar bin Zubeir alimshukuru Makonda kwa uamuzi alioufanya; na kusema ameonesha njia kwa wadau wengine walio na wasio waislamu kujitolea kuchangia.

“Najua jamii inaweza kushangaa kwa nini nimepokea msaada kutoka kwa mtu ambaye si Muislamu, lakini niseme tu hata Mtume alipokea misaada kutoka kwa watu kama hawa, ni rai yangu kuwaombeni na ninyi Waislamu mjitokeze kuunga mkoa juhudi hizi kwa hali na mali,” alisema.

Monday 15 August 2016

USAIN BOLT BADO ATETEA NAFASI YAKE YA UBINGWA MARATHON

Mwanariadha Usain BOLT raia wa Jamaica ameendelea kutetea nafasi yake ya mkimbiaji bora duniani kwa jana kukimbia mita 100 kwa sekunde 9.81 na kujinyakulia medali ya dhahabu ktk mashindano ya Olympics yanayoendelea huko Rio de Janeiro Brazil. Wa pili ni Justin Gatlin wa Marekani amenyakua Silver kwa kumaliza kwa sekunde 9.89 na wa tatu ni Andre de Grasse wa CANADA ametumia sekunde 9.91 na kujinyakulia medali ya Bronze

MASANJA MKANDAMIZAJI AUKACHA UKAPERA

Hapo jana Jumapili 14 Agosti,2016 Mchekeshaji maarufu na Mchungaji Msaidizi Emanuel Mgaya au maarufu kwa jina la Masanja Mkandamizaji alifunga ndoa na mpenzi wake. Tunawaombea wote maisha mema ya Ndoa

Sunday 14 August 2016

TANZIA: RAIS WA ZAMANI WA ZANZIBAR ABOUD JUMBE MWINYI AFARIKI DUNIA

ALIYEKUWA rais wa pili wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kati ya tarehe 7 Aprili 1972 hadi 30 Januari 1984, Aboud Jumbe Mwinyi amefariki dunia mchana wa leo nyumbani kwake Kigamboni, jijini Dar es Saalam baada ya kuugua kwa muda mrefu.

Kifo cha mwanasiasa huyo mkongwe kimethibitishwa na mmoja wa wanafamilia ya marehemu.

Marehemu Jumbe atakumbukwa kwa mchango wake mkubwa wa kuiongoza serikali ya mapinduzi ya Zanzibar akichukua nafasi ya aliyekuwa rais wa nchi hiyo marehemu Abeid Aman Karume aliyefariki mwaka 1972.

Enzi za uhai wake akiwa rais wa serikali ya mapinduzi Zanzibar alishirikiana na rais wa wakati huo wa Tanzania na mwenyekiti wa chama cha TANU marehemu Julius Nyerere kuanzisha Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa kuvunja vyama vya TANU na ASP na kuunda chama kimoja cha CCM.

Nae Mhe Rais Magufuli amemlilia Mzee Jumbe kwa waraka huu;