Sunday 7 June 2009

ST. AUGUSTINE UNIVERSITY DAR

Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo akiotesha mti kuzindua Chuo cha Mt. Augustino Tawi la Dar katika eneo la Msimbazi Centre jana. Chuo hiki kina makao yake kule Jiji la Mwanza.


Polycarp Kardinali Pengo


Habari Zaidi:


FEBRUARI 21 mwaka huu wakati nanunua kitabu chenye sehemu ya historia ya maisha ya Askofu Mkuu Mwandamizi wa Jimbo Kuu Katoliki, Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo, nilipata wazo la kuandika makala lakini sikulizingatia pengine kwa sababu si kawaida na sijawahi kusoma maandiko kwenye jarida au gazeti kuhusu maisha ya kiongozi yoyote mkuu wa dini nchini. Baada ya kukisoma kitabu hicho chenye kurasa 24 wazo la kuandika makala kuhusu maisha yake lilinijia tena ila niliona ni jambo gumu hivyo ilibidi nitafute namna ama ya kuiandika isitafsiriwe tofauti au nisubiri kuwe na mazingira fulani yatakayotoa fursa ya kuchapishwa kwa makala haya.

Nilinunua kitabu hicho katika Viwanja vya Kanisa Kuu la Mtakatifu Joseph, Dar es Salaam ili nimfahamu kiongozi huyu wa kanisa linalowahudumia mamilioni ya Watanzania kiroho na kimwili, Kardinali wa pili Tanzania anayeongoza parokia 57 za Dar es Salaam.
Si hivyo tu nilipenda kumfahamu raia huyo wa Vatican, aliyepata daraja la Upadre Juni 20 mwaka 1971 katika Parokia ya Mwazye, Jimbo la Sumbawanga mkoani Rukwa. Sina hakika kama wazazi wake, Joseph na Rozalia walitarajia kwamba mmoja wa watoto wao tisa angekuwa katika daraja alipo Kardinali Pengo leo.

“Ni kweli mimi nina uraia wa Vatican. Kiserikali Vatican ni dola huru kama dola nyingine yoyote duniani, ndiyo maana ina mabalozi wake, na yenyewe inapokea mabalozi toka nchi nyingine. Hivyo kama ni sarafu Vatican ina sura mbili, ni makao makuu ya kiroho ya Wakatoliki, lakini pia ni nchi huru yenye uhusiano wa kibalozi na nchi nyingine,” anasema Kardinali Pengo alipofanya mahojiano na Padre Stefano Kaombwe na Paschal Maziku.

“Mimi ni Mtanzania kwa kuzaliwa na Mvatican kutokana na imani yangu, na kwa kuwa hali hizi mbili hazipingani, siwezi kusema kilicho cha kipaumbele ni kipi. Lakini imani ya kidini wakati wote inashika nafasi ya kwanza. Kama ni kuchagua kati ya Vatican na Tanzania, Mungu anatangulia mbele kati ya yote.

Hata maisha yangu yenyewe, ni heri kufa kuliko kuikana imani yangu,” anasema na kubainisha kwamba amejitoa maisha yake kumtii Papa kwa kuwa anaifikisha sauti ya Mungu kwake. Anasema ingawa anafahamu kwamba Baba Mtakatifu hawezi kumweleza akafanye kazi Vatican, endapo ataambiwa hivyo, hatofurahi ila atatii na anamwomba Mungu asiambiwe akafanye kazi huko kwa kuwa itamuumiza. Anasema haoni ugumu kwa Watanzania kuwa na uraia wa nchi mbili kama wananchi wengi watakubali na kwamba Bunge lijadili kwa kina suala hilo.

“Tunaweza kuwa na mashaka juu ya uzalendo wa mtu mwenye uraia wa nchi mbili, ila hata hivi leo tunapokuwa na uraia wa nchi moja bado kuna Watanzania wenzetu ambao uzalendo wao ni wa mashaka,” anasema mwanachama huyo wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania lenye miaka 50. Askofu Mkuu Pengo ana msimamo katika kile anachokiamini na amekuwa wazi kueleza hisia zake hasa kukemea maovu katika jamii yakiwamo matukio mabaya ya ufisadi, ulafi, ulevi wa madaraka, ubinafsi, ukatili, na uchoyo.

“Hali ya sasa ambayo imeanza kutawaliwa na ufisadi ni mbaya na watu hawatavumilia. Tusipoweza kurekebisha hali ya uchumi kuhodhiwa na walafi wachache leo, hakika kesho itakuwa hali mbaya sana, tumwombe Mungu atusalimishe,” anasema. Anasita kusema Tanzania ni kisiwa cha amani kwa maelezo kwamba, kuna maovu mengi katika jamii yakiwamo mauaji ya albino na ameonya kwamba kama hali itaendelea hivi siku zijazo mwenye nguvu ndiye atakayeishi.

Amekanusha madai kuwa amepunguza ‘moto’ wa kukemea maovu hasa masuala ya kitaifa na amedai kuwa kuna mengi ameyazungumza lakini hayajaandikwa kwa kuwa vyombo vya habari vinaandika habari wanazozipenda waandishi wa habari na wamiliki. “Cha kushangaza zaidi ni kuwa, vyombo vya watu binafsi ndivyo vina kelele zaidi ya vile vya serikali na kwa kweli ndivyo vinavyotawala nchini,” anasema. Ni mtoto wa sita kuzaliwa katika familia yao, aliianza safari yake ya maisha Agosti 5, 1944 katika Kijiji cha Mwazye akiwa ni mtoto wa tatu wa kiume, ndugu zake wengine ni Kordula, Vincent, Elfrazia, Selvasia, Modesti, Gaspar, Helena na Chrisant.

Historia ya maisha yake inaonyesha kwamba alikuwa na hamu ya kumtumikia Mungu tangu akiwa mdogo ndiyo maana baada ya kuhitimu elimu ya msingi mwaka 1956 katika Shule ya Mwazye, mwaka uliofuatia alijiunga na Seminari ndogo ya Karema na mwaka 1959 akajiunga na Seminari nyingine ndogo ya Kaengesa na kuhitimu kidato cha nne 1964. Hakuishia hapo, 1965 alijiunga na Seminari Kuu Kipalapala, Tabora na kusoma falsafa na Taaluma ya Mungu, akahitimu mwaka 1971 na ukawa mwanzo wa kuanza rasmi safari ya kuhubiri neno la Mungu na kuongoza waumini katika vigango, parokia, majimbo ya Nachingwea na Tunduru Masasi na sasa Jimbo Kuu la Dar es Salaam.

Anaongoza jimbo lenye uhaba wa wachungaji hivyo ana mkakati wa kuwalea na kuwaimarisha waseminari na hata kama mapadre wa jimbo watakuwa wengi ataomba wamisionari wengi wafanye kazi katika jimbo hilo lenye waumini zaidi ya milioni moja. Anasema jimbo hilo lina parokia 57, lakini kwa uwiano wa idadi ya watu linahitaji parokia 500, na anaamini kwamba, kabla hajaaga dunia ndoto yake ya kuwa na parokia 100 jimboni humo itatimia. “Changamoto ni kuwa tutakapofika parokia mia moja tutakuwa tunadaiwa elfu moja.

Tungefikia makubaliano na Papa kuligawa jimbo ingekuwa ni utatuzi mkubwa wa shida hii,” anasema na kubainisha kwamba anasali ili Jimbo Kuu la Dar es Salaam ligawanywe ikiwezekana yawe majimbo matatu kwenye eneo la sasa. Wengi wanamfahamu Pengo kwa kazi zake za kichungaji lakini wapo wanaomfahamu kwa uwezo wake wa kufundisha. Alikuwa mwalimu kwa miezi tisa katika Seminari Kuu ya Kipalapala mwaka 1977 hadi 1978 na alifundisha Seminari ya Segerea hadi alipoteuliwa kuwa Askofu.

Licha ya madaraka katika Jimbo Kuu Dar es Salaam ana majukumu katika Kanisa Katoliki Afrika, yeye ni Rais wa Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika na Madagascar. Karama alizonazo katika uongozi zimemwezesha mtumishi huyo wa Mungu, kwa nyakati tofauti kujiwekea historia katika maisha yake ikiwa ni pamoja na kuteuliwa kuwa Gombera (Mkuu wa Seminari) wa kwanza wa Seminari Kuu ya Segerea kuanzia mwaka 1978, akaifanya kazi hiyo hadi Novemba 1983.

Si hivyo tu, Pengo ni Askofu wa kwanza Jimbo la Tunduru Masasi, Oktoba 17, 1986 aliteuliwa kuwa askofu huko, Februari 12 akasimikwa kuanza kazi katika eneo ambalo kwa asili lilikuwa la Waislamu. “Wazee wa Tunduru hawakunipinga, japo wachache walio tofauti hawakosekani. Kwa ujumla wazee wa mji huo walinipokea, hata nilipoanza kujenga nyumba ya Askofu, wafanyakazi wengi walikuwa ni Waislamu,” anasema na kubainisha kwamba wakati anakwenda kuanza kuongoza Jimbo Kuu la Dar es Salaam hakuwa na uhakika kama wangempokea.

Novemba 1983 kama Baba Mtakatifu Yohane Paulo wa II asingemteua kuwa Askofu wa Jimbo la Nachingwea angeweza kuendelea na madaraka yake katika Seminari ya Segerea, Dar es Salaam. Alianza rasmi madaraka ya Uaskofu Januari 6, 1984 kwa kuwekwa wakfu mjini Roma, Italia. Hakutarajia kama kuna siku angekuwa Askofu ndiyo maana alipoteuliwa kushika madaraka hayo ilikuwa ni siku ngumu kwake na hakupata usingizi, wakati anateuliwa alikuwa pia mwalimu na mhazini katika Seminari ya Segerea.

Wakati Balozi wa Papa alipokwenda Segerea kumfahamisha kuhusu uteuzi huo hakumkuta, Mwalimu Pengo alikuwa katika Kituo cha Maaskofu Kurasini, Dar es Salaam, alimfuata huko na kumkabidhi barua ya Baba Mtakatifu, alipoisoma akashikwa na butwaa, na alipoulizwa maswali hakujibu. “…akili yangu ilikuwa mbali mno. Balozi akaniambia anasubiri jibu kutoka kwangu ndani ya saa 24, tena liwe kimaandishi na kwa mkono wangu,” amesema Askofu Mkuu Pengo wakati alipofanya mahojiano na Padre Stephano Kaombe na Paschal Maziku.

Februari mwaka huu ameadhimisha miaka 25 ya uaskofu, amekuwa Askofu Mkuu Mwandamizi wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam tangu Baba Mtakatifu Yohane Paulo II alipomteua Machi 10 mwaka 1990, miezi sita baadaye kiongozi huyo wa Kanisa Katoliki Duniani akaja Tanzania. “Ni ukweli miaka hii ishirini na tano nikitazama nyuma imekuwa ni ya furaha. Wasiwasi ulikuwa ni jinsi gani ninapokwenda sehemu mpya nitakavyopokelewa na nitakavyokubalika.

Ndicho pia kilitokea nilipokuwa nakuja Dar es Salaam, nilijiuliza je, watanipokea? Waumini na watu waliozoea kukaa na mzee, tena Kardinali (Lauren Rugambwa), wakati mimi ni kijana Askofu Mwandamizi tu?,” anasema. “Ni vigumu kusema mafanikio au matatizo ni yapi. Jambo hili hasa linaweza kufanywa na wengine. Ila kwa upande wangu sijawahi…nimeishi na uaskofu wangu kwa miaka hii yote kwa furaha,” anasema na kueleza kwamba, inawezekana katika utekelezaji wa majukumu yake ya uaskofu kuna aliowasikitisha, na amekuwa akiomba msamaha kwa Mungu.


Nilikuwa miongoni mwa waliohudhuria ibada ya Jubilei ya Fedha (miaka 25) ya uaskofu wake, mengi yalisemwa kuhusu yeye, na yeye pia alisema mengi ila miongoni mwa ninayoyakumbuka ni mamna alivyomwagiza Rais Mstaafu wa Serikali ya Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa akahiji katika eneo alipozikwa hayati Baba wa Taifa, Julius Nyerere, ili afikishe shukurani zake kwa kujenga mazingira yaliyoliwezesha Kanisa kufanya kazi zake. Kardinali Pengo alimtuma Mkapa akamweleze Nyerere kuwa yeye anamshukuru kwa kuwa alijenga mazingira yaliyoliwezesha Kanisa lifike lilipofika. Alimtaka Mkapa afikishe shukurani hizo kwa marais waliomtangulia akiwamo Rais mstaafu wa Serikali ya Awamu ya Pili, Ali Hassan Mwinyi, na Rais wa sasa, Jakaya Kikwete.

Julai 22, 1992 alianza rasmi kuongoza Jimbo Kuu la Dar es Salaam, amefanikiwa katia mambo mengi ikiwa ni pamoja na kuongeza idadi ya mapadri, na kuboresha huduma za kijamii zikiwamo shule. Baba Mtakatifu aliyepita na wa sasa, Papa Benedict XVI walitambua uwezo wake katika kazi za kichungaji ndiyo maana ana madaraka aliyonayo, amekuwa Kardinali tangu Februari 21 mwaka 1998.

“Furaha na huzuni kwa Askofu yeyote yule vinafanana. Askofu anakuwa na furaha anapotoa daraja ya Upadre, iwe yeye mwenyewe au mwingine kwa niaba yake. Upadrisho daima umekuwa chemichem ya furaha kwangu,” anasema kiongozi huyo wa Kanisa mwenye Shahada ya Uzamivu (PHD) ya maadili aliyoipata mwaka 1977 katika Chuo cha Laterano, Rome nchini Italia.

“Padre yeyote ni mkono wa kuume wa Askofu. Jambo la huzuni ni pale unapoona padre anashindwa kutekeleza utume wake. Huwa najiuliza, je, mimi ndiye sababu ya kushindwa kwake? Padre anapopotoka husababisha maumivu makali moyoni mwangu,” anasema Mwadhama Pengo. Sehemu ya historia ya Askofu Mkuu Pengo imeandikwa katika kitabu kiitwacho Kuishi Kwangu ni Kristo.