Sunday 13 September 2015

DKT MAGUFULI AWA CHANGAMOTO MIKOA 11 ALOPIGA KAMPENI KUTOKANA NA YAFUATAYO

KAMPENI za mgombea urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk John Magufuli, zimemalizika katika mikoa 11 jana, kwa kumalizia katika Mkoa wa Simiyu, huku ajenda kadhaa na ubora wake wa kutawala jukwaa, vikimng’arisha mgombea huyo na kumfanya kuwa kivutio cha wananchi.

Mpaka sasa Dk Magufuli ameshafanya kampeni katika mikoa ya Katavi, Rukwa, Songwe, Mbeya, Njombe, Ruvuma, Mtwara, Morogoro, Tanga, Mara na jana alifikisha mkoa wa 11 Simiyu.

Kabla ya kufika Mara na Simiyu, takwimu za CCM zilizotolewa na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi, Abdalah Bulembo, zimeonesha katika mikoa hiyo mingine tisa, Dk Magufuli alikuwa ameshasafiri kwa barabara katika wilaya 42 na kufanya mikutano 48 iliyo katika ratiba na mikutano mingine 260 isiyo rasmi.

Moja ya ajenda kubwa iliyombeba Dk Magufuli katika mikutano hiyo mpaka Simiyu, ilikuwa uadilifu katika utendaji wake wa kazi katika wizara mbalimbali alizofanya kazi katika miaka 20 ya utendaji wake, ikiwemo katika Wizara ya Ujenzi, ambako ametumikia kwa miaka 15.

Uadilifu
Katika mikoa mingi alikopita, uadilifu wake umezungumzwa kwa namna tatu tofauti, ikiwemo mwenendo alioonesha katika nafasi yake ya Waziri katika Wizara ya Ujenzi, iliyokuwa ya kipaumbele kibajeti.

Kwa mfano katika Bajeti ya Serikali kwa mwaka huu wa fedha 2015/2016, Wizara ya Ujenzi imekabidhiwa Sh trilioni 1.2 za wizara, huku Mfuko wa Barabara ulio chini ya wizara hiyo, ukikabidhiwa zaidi ya Sh bilioni 866 na hivyo kwa ujumla kukabidhiwa Sh trilioni mbili, ambazo amepaswa kuzisimamia.

Kwa mujibu wa Dk Magufuli mwenyewe, akipiga hesabu ya fedha za umma alizosimamia kwa ajili ya miradi ya ujenzi wa barabara katika miaka kumi ya uongozi wake, ni zaidi ya Sh trilioni 9.5, lakini hakula hata senti tano, badala yake akajenga mtandao mrefu wa barabara za lami nchi nzima.

Namna ya pili ya kuzungumzia uadilifu wake ni ushirikiano wake na watendaji na wadau wa sekta ya ujenzi, ambao amekuwa akiwapa kazi za mabilioni ya shilingi, katika kuwatumikia Watanzania.

Namna ya tatu iliyotumika kuelezea uadilifu wa Dk Magufuli, imeelezwa na Jaji Joseph Warioba mkoani Mara, ambapo alisema mwaka 1996, aliteuliwa na Rais Benjamini Mkapa, kuongoza Tume ya Kero za Rushwa.

Katika uchunguzi wao, Jaji Warioba alisema walibaini rushwa kubwa na nyingi zilikuwa katika sekta ya ujenzi wa barabara, lakini akafafanua baada ya Dk Magufuli kuanza kufanya kazi katika sekta hiyo, kelele ya rushwa katika sekta hiyo imetoweka.

Uchapakazi
Mbali na uadilifu, ajenda nyingine iliyombeba Dk Magufuli na kusababisha awe kivutio kikubwa kwa maelfu kwa maelfu ya wananchi waliojitokeza katika mikutano yake, ni sifa ya uchapakazi wake ambayo imeendana na matokeo yanayoonekana ya kazi hiyo.

Mbali na watumishi, ukali wake pia umejidhihirisha mara kwa mara alipozungumzia Baraza la Mawaziri atakalounda na hasa Waziri wa Ujenzi, akisema huyo waziri atakayemteua, kama hawezi kazi aseme mwenyewe kabla ya kutimuliwa, kauli ambayo pia imepokewa kwa shangwe na wananchi.

Ubora jukwaani
Dk Magufuli pia katika mikoa hiyo 11, ameonesha umahiri mkubwa wa kutawala majukwaa kwa mbinu mbalimbali, ikiwemo uwezo wa kutoa salamu na vionjo vya makabila zaidi ya kumi jambo lililokuwa likiwavutia wananchi wengi katika mikutano ambayo imekuwa ikifikia mpaka 15 kwa siku.

Akifafanua sababu ya kutumia lugha za makabila mbalimbali, Dk Magufuli amekuwa akisema mwitikio wa salamu hizo, umekuwa ukionesha namna jamii ya Tanzania ilivyo na umoja kwa makabila mbalimbali kukutana katika mikutano yake na kufurahia pamoja.

Mara kadhaa baada ya kutoa salamu hizo, alikuwa akimalizia kwa kusema hiyo ndio Tanzania yenye kila mchanganyiko wa kabila, lakini wanaishi kwa umoja na amani bila aina yoyote ya ubaguzi.

Baada ya kutoa salamu hizo, Dk Magufuli pia amekuwa akiomba kura kutoka kwa vyama vyote, kuanzia CCM, Chadema, CUF, NCCR-Mageuzi, ACT na kwa watu wasio na vyama, huku akiwaambia kuwa kazi yake itakuwa kuwaletea maendeleo na kwa kuwa maendeleo hayabagui, ndio maana anaomba kura za vyama vyote.

Ahadi zake
Dk Magufuli katika mikutano hiyo, amekuwa akiahidi kushusha bei ya vifaa vya ujenzi hasa saruji, mabati na misumari, ili wananchi wanaofanya kazi wajenge nyumba bora.

Katika kuongeza idadi ya Watanzania wanaofanya kazi ili kufikia lengo hilo, Dk Magufuli alisema katika kila mtaa na kijiji, Serikali yake itatoa Sh milioni 50 kwa ajili ya kuanzisha na kukuza biashara ndogo za wanawake na vijana.

Alisema atataka kila anayefanya kazi apate kipato kizuri kitakachomsaidia kukabiliana na mahitaji ya maisha yake, ikiwemo kujenga nyumba bora kutokana na kushushwa kwa bei za bidhaa za ujenzi.

No comments:

Post a Comment

Maoni yako