Wednesday 27 May 2015

KUELEKEA UCHAGUZI MKUU: MAJIMBO YA MBEYA MJINI NA VIJIJINI KUGAWANYWA

KIKAO cha Kamati ya Ushauri cha Wilaya ya Mbeya, jana kilikaa na kupitia mapendekezo ya kuyagawa majimbo mawili ya Mbeya na kuwa majimbo manne ya uchaguzi kwa mwaka 2015.

Kikao hicho kiliwahusisha madiwani, wanasiasa, kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya na vyombo vya habari.

Katika kikao hicho, wajumbe walikubaliana kuyagawa majimbo hayo ambayo ni Jimbo la Mbeya Mjini linaloongozwa na Joseph Mbilinyi (Chadema). Kwa mujibu wa mapendekezo, jimbo hilo litagawanywa na kuwa na majimbo ya Iyunga na Sisimba.

Mapendekezo hayo yanataka Jimbo la Iyunga liundwe na kata zote 21 za Tarafa ya Iyunga ambayo ina jumla ya wakazi wapatao 327,122.

Jimbo la Sisimba, litakuwa na kata 15 zilizopo Tarafa ya Sisimba yenye wakazi wanaokadiriwa kuwa 106,264.

Pamoja na idadi ya watu, vigezo vingine vilivyotumika kuyagawa majimbo hayo ni pamoja na jiografia ya tarafa hizo kwa kuwa Tarafa ya Sisimba imezungukwa na milima na mabonde.

Kwa upande wa Halmashauri ya Mbeya, mapendekezo yaliyopo ni kugawa Jimbo la Mbeya Vijijini linaloongozwa na Mchungaji Lacksoni Mwanjale (CCM).

Mapendekezo yaliyopo yanataka jimbo hilo ligawanywe ili lipatikane Jimbo la Mbeya na Jimbo la Isangati.

Jimbo la Mbeya, litaundwa na kata 11 za Tembela, Inyala, Itewe, Njombe, Maendeleo, Igoma, Ilungu, Ihango, Lwanjilo, Ulenje na Swaya zenye wakazi 107,349.

Jimbo la Isangati litakuwa na kata 15 za Masoko, Ilembo, Izyira, Iwiji, Isuto, Bonde la Songwe, Iwindi, Igale, Santiliya, Iyunga Mapinduzi, Itawa, Utengule Usongwe na Nsalala zenye wakazi 221,480.

Akizungumza baada ya kufungua kikao hicho, Mkuu wa Wilaya ya Mbeya, Nyirembe Munasa, alisema mgawanyo wa majimbo hayo umepita katika vikao mbalimbali vya kisheria.

No comments:

Post a Comment

Maoni yako