Monday 22 August 2016

TSHIRTS ZA KUHAMASISHA "UKUTA" ZAKAMATWA JIJINI DAR

Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam limesema limejiandaa kudhibiti maandamano ya Umoja wa Kupambana na Udikteta Tanzania (Ukuta) yaliyoandaliwa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) yanayotarajiwa kufanyika Septemba Mosi mwaka huu.

Wakati akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam, Kamanda wa Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam Simon Sirro amewatoa hofu wakazi wa mkoa huo kuwa hakuna mtu na au kikundi chochote cha watu kitakachofanya maandamano siku hiyo.

“Habari ya Ukuta haipo,umeshabomoka na kama haujabomoka utabomoka, wakazi wa Dar es Salaam msiwe na hofu, fanyeni kazi na hata siku hiyo hakuna mtu atakayejitokeza barabarani kuandamana,” amesema.

Kamanda Sirro amedai kuwa siasa zinatakiwa kufanywa kwa amani na utulivu na kwamba wanasiasa wanaoitumia siasa kufanya vurugu hawatafanikiwa.

“Mimi niwahakikishie kwamba tunajiandaa kwelikweli kuhakikisha watu wanafuata sheria , anayetaka kuvunja sheria kwa kufanya maandamano aanze yeye ili nasi tuanze naye,” amesema.

Ameongeza kuwa ” Suala la utii wa sheria ni la msingi,kama kuna watu au kikundi cha watu kinataka kuitumia siasa kufanya uvunjifu wa amani wajue kwamba nafasi hiyo kwa Dar es Salaam haipo.”

Aidha,Kamanda Sirro amesema August 20 2016 Jeshi la Polisi lilipata taarifa toka kwa raia wema kuwa maeneo ya Kinondoni kuna duka linauza flana zenye maneno ya uchochezi yaliyoandikwa ‘’TUJIPANGE TUKATAE UDIKITETA UCHWARA’’ , ‘UKUTA’ ‘

Amesema Polisi baada ya kupata taarifa hizo walifika eneo la tukio na kumkamata mtuhumiwa aitwaye YORAM SETHY MBYELLAH miaka 42, mfanyabiashara na mkazi wa Mburahati akiwa anauza fulana hizo dukani kwake.

No comments:

Post a Comment

Maoni yako