Tuesday 16 August 2016

MHE RC MAKONDA: BAKWATA KUPATA JENGO JIPYA LA MAKAO MAKUU YAO

MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda amekabidhi ramani ya jengo la Ofisi ya Makao Makuu ya Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA), ikiwa ni ahadi ya kuwajengea jengo hilo.

Akizungumza wakati akikabidhi ramani hiyo, Makonda alisema jengo hilo linatarajiwa kuwa na ghorofa tatu na litagharimu zaidi ya Sh bilioni tano.

“Ijumaa nitakuja hapa kwa ajili ya kuweka jiwe la msingi na niseme tu ujenzi utaanza hivi karibuni na nimeshawaambia watu wangu wahakikishe jengo hilo linajengwa kwa muda usiozidi miezi 14 tu,” alisema Makonda.

Licha ya kukabidhi ramani hiyo, Makonda pia aliwataka viongozi hao wa dini kuendelea kuhubiri amani ili taifa liendelee kuwa na amani na mshikamano. Alisema ujenzi wa jengo hilo, umekuja baada ya kuona kuwa Bakwata imekuwa na mchango mkubwa kwa taifa ikiwemo kuhubiri amani na mshikamano.

“Viongozi wa dini ni watu muhimu sana wamekuwa wakituhubiria amani na pia viongozi hao wamekuwa wakituongoza katika safari ya kutupeleka kwa mola, endeleeni kudumisha na kuihubiri amani ili taifa ili liendelee kusifika,” alisema Makonda.

Kwa upande wake, Mufti wa Tanzania, Shehe Mkuu Abubakar bin Zubeir alimshukuru Makonda kwa uamuzi alioufanya; na kusema ameonesha njia kwa wadau wengine walio na wasio waislamu kujitolea kuchangia.

“Najua jamii inaweza kushangaa kwa nini nimepokea msaada kutoka kwa mtu ambaye si Muislamu, lakini niseme tu hata Mtume alipokea misaada kutoka kwa watu kama hawa, ni rai yangu kuwaombeni na ninyi Waislamu mjitokeze kuunga mkoa juhudi hizi kwa hali na mali,” alisema.

No comments:

Post a Comment

Maoni yako