Sunday 21 August 2016

CHADEMA: OPERESHENI UKUTA IPO PALE PALE SEPTEMBA MOSI

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimeendelea kushikilia msimamo wa kuendeleza operesheni UKUTA Septemba mosi mwaka huu.

Mbunge wa Kawe, Halima Mdee, alisema kwenye Baraza la Mashauriano la Kanda ya Pwani, lililofanyika jana Dar es Salaam kuwa wataitaarifu Polisi kuhusu maandamano yao watakayoyafanya bila kubeba silaha ili wapewe ulinzi.

Kwa mujibu wa Mdee ambaye ni Mwenyekiti wa Baraza hilo kwa Kanda ya Pwani, hawategemei kufanya fujo katika maandamano hayo, bali watatekeleza wajibu wao wa kudai demokrasia ambayo ni haki yao ya kikatiba, huku wakiwa wamejifunga vitambaa vyeupe mkononi na fulana nyeusi.

“Atakayefanya fujo katika maandamano hayo hayo Polisi watakuwa na haki ya kumkamata, vinginevyo tutadai haki yetu ya kidemokrasia ya kufanya mikutano na shughuli za kisiasa kwa njia ya amani”, Mdee alisema.

Wapinzani wamedhamilia kufanya maandamano hayo, licha ya Rais Magufuli kupiga marufuku maandamano na mikutano ya kisiasa isiyo na lengo jema ikiwemo ya viongozi kutoka kwenye maeneo yao kwenda kufanya mikutano kwenye maeneo mengine, jambo linalopingwa na Chadema kwa maelezo kuwa ni ukiukaji wa demokrasia.

No comments:

Post a Comment

Maoni yako