Thursday 28 April 2016

WABUNGE WASIOCHANGIA BUNGENI KUBANWA

Kiti cha Spika wa Bunge kimesema ipo haja ya kufanya marekebisho ya Sheria pamoja na Kanuni ili kila mbunge apate posho kulingana na kazi aliyofanya bungeni, badala ya utaratibu wa sasa wa kuangalia mahudhurio pekee.

Aidha, kimewataka wabunge kubadilika na kuacha tabia ya kuchukua posho za vikao vya Bunge bila kuzitolea jasho.

Kauli hiyo imekuja kutokana na Mwongozo ulioombwa Aprili 25, mwaka huu na Mbunge wa Nzega Mjini, Hussein Bashe (CCM) ambaye alikitaka kiti cha Spika kutoa Mwongozo kuhusu usahihi wa wabunge wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kulipwa posho na mishahara wakati hawashiriki na kutimiza wajibu wao wa kuchangia kwenye mjadala wa Bunge la Bajeti linaloendelea katika Mkutano wa Tatu wa Bunge la 11.

Bashe alisema mbunge huyo alitumia Kanuni ya 68(7) ya Kanuni za Kudumu za Bunge akiomba Mwongozo wa Spika kutokana na Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, kuamua kutoshiriki mjadala unaoendelea bungeni, lakini wabunge hao wanasaini na kulipwa mishahara na posho.

Hivyo akaomba Mwongozo endapo ni haki kwa wabunge hao kupokea posho wakati hawashiriki wala kutimiza wajibu wao wa kisheria.

Katika kujenga hoja hiyo, Bashe alitumia Ibara ya 63(3) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania isemayo, “Kwa madhumuni ya utekelezaji wa madaraka yake Bunge laweza kujadili utekelezaji wa kila Wizara wakati wa Mkutano wa Bunge wa kila mwaka wa bajeti.”

Aidha, Bashe alitumia Ibara ya 73 ya Katiba ya Tanzania kufafanua kuhusu malipo ya mshahara, posho na malipo mengine kwa wabunge.

Akitoa Mwongozo wa Spika, Naibu Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson alisema kwa mujibu wa Katiba ya Tanzania, Ibara ya 73 imeainisha masharti ya kazi ya wabunge.

Alisema mbunge anastahili kulipwa mshahara kwa kila mwezi, na kufafanua kuwa mbunge anapohudhuria vikao bungeni na kamati atalipwa posho ya vikao kwa kiwango kitakachowekwa na Serikali na Kanuni za Bunge.

Alisema malipo ya mshahara ni suala la Kikatiba na Sheria hulipwa kwa mbunge kutokana na kazi yake ya ubunge.

Hivyo malipo ya posho kwa wabunge yanatokana na mahudhurio yao bungeni na siyo kwa kuchangia kama ambavyo wengi wao wanapenda iwe hivyo.

“Kimsingi kuhudhuria bungeni pekee siyo njia inayopendeza kwa kuwa mbunge anapofika bungeni anatarajiwa atekeleze majukumu yake yalivyoainishwa katika Ibara ya 63.

“…Tabia hii ya kutochangia mijadala na kuzunguka zunguka bungeni haikubaliki na haitakiwi kuendelea, kila mbunge atekeleze wajibu wake na sio anahudhuria ili alipwe posho,” alisema Dk Ackson.

No comments:

Post a Comment

Maoni yako