Monday 6 July 2009

KUSAJILI SIMU TANZANIA


Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imesema mmiliki wa simu ya mkononi ambaye hatasajili simu yake ndani ya miezi sita kuanzia TAREHE 1 Julai, namba yake itafungwa. TCRA kuanzia tarehe hiyo imeanza kusajili wamiliki wote wa simu za mikononi nchini na wataruhusiwa kuwa na laini za simu nyingi kwa kadri wanavyotaka, ila zote itabidi zisajiliwe kwa kampuni za mitandao husika, lengo likiwa ni kudhibiti wizi na matumizi mabaya ya simu hizo.

Mkurugenzi Mkuu wa TCRA, Profesa John Nkoma, aliwaambia wahariri wa habari jana Dar es Salaam kwamba mtu ye yote mwenye simu ambaye hadi Desemba 31 mwaka huu, laini yake ya simu haitakuwa imesajiliwa, itakoma matumizi yake.

Alisema wameamua kutoa miezi sita ya kufanya usajili huo ili kuondoa usumbufu wa watu kukimbizana na muda wa usajili na kuwapo kwa misururu mirefu, hivyo wanaamini kipindi hicho kitatosha kukamilisha kazi hiyo ambayo inaaminika itadhibiti matumizi mabaya ya simu na wizi.

“Kila Mtanzania itabidi ajiorodheshe na wageni pia wataandikishwa wanapoingia nchini kama watakuwa wanataka kutumia simu hapa. Tunafanya hivi ili kumlinda mtumiaji, lakini pia huduma mbalimbali zimekuwa na usajili kama vile za maji, umeme, magari, pikipiki na kadhalika. Hili la usajili kwa kweli haliwezi kuepukika,” alisema Profesa Nkoma na kuongeza:

“Hiki si kitu kigeni, hata wale ambao wanatumia Post-pay (malipo baada ya huduma), wanatumia utaratibu huu, kwa maana wanajiandikisha. Hivyo si huduma ngeni, hata katika kutuma fedha kuna kujiandikisha, kwa hiyo kila mmoja itabidi ajiandikishe.”

Mkurugenzi Mkuu huyo wa TCRA alisema kazi ya usajili itafanywa na kampuni hizo za mitandao ya simu za mkononi na si mamlaka yake, na mtu atakayekwenda kusajiliwa, atahitajika kuwa na kitambulisho kimojawapo kati ya vitambulisho 10 vilivyowekwa.

Alivitaja vitambulisho hivyo ambavyo kimojawapo kinaweza kutumika kutambulisha mmiliki wa simu wakati wa usajili kuwa ni cha mpiga kura; pasipoti; cha mfuko wa pensheni; cha Saccos; leseni ya udereva; cha benki; cha ajira na barua ya mwajiri na kitambulisho cha chuo cha elimu ya juu.

Vingine ni kitambulisho cha uanachama kwenye klabu na barua ya serikali za mitaa ikiwa na picha, saini na mhuri. Profesa Nkoma alisema hivi sasa Tanzania ina watumiaji wa simu za mkononi milioni 14, kutoka watu 300,000 waliokuwapo mwaka 2000, idadi inayoonesha kuongezeka kwa watumiaji pamoja na kuboreshwa kwa huduma za simu za mkononi kutokana na ushindani nchini.

Alisema taarifa zitakazotolewa kwa kampuni za simu na wamiliki wa simu hizo za mikononi, zitabaki kuwa siri kwa kampuni husika, kwani kwa mujibu wa sheria, zinawajibika kutunza siri hizo. Aidha, alisema suala la kuuza laini za simu holela litakwisha kwa sababu kampuni za mitandao ya simu zitakuwa na namba maalumu za wauzaji wa simu hizo, hivyo itadhibiti uuzaji holela.

Kwa muda mrefu, kimekuwapo kilio cha kutaka serikali idhibiti matumizi ya simu za mkononi kwa sababu ya baadhi ya watu kuzitumia vibaya kwa kutuma ujumbe mfupi wa maneno kwa watu au kuwapigia simu za vitisho na kisha namba hizo kutokuwa hewani kwa muda mrefu

No comments:

Post a Comment

Maoni yako