Tuesday 7 July 2009

CHUO KIKUU KINGINE KIPYA KUJENGWA DAR

Na Moshi Lusonzo

umla ya shilingi bilioni 50 zinatarajiwa kutumika kwa ajili ya ujenzi wa Chuo Kikuu kipya Jijini Dar es Salaam ambapo ujenzi wake umeshaanza rasmi.
Chuo kikuu hicho kitakachoitwa United African, kinajengwa katika eneo la Vijibweni, Kigamboni Jijini, kwa msaada wa watu wa Korea ya Kusini, Marekani na Tanzania.

Akizungumza hivi karibuni, Msimamizi Mkuu wa ujenzi wa Chuo hicho, Mchungaji Joshua Lee, amesema chuo hicho kitakuwa na vitivo mbalimbali vya elimu pamoja na viwanda vitakavyotumika kujifunzia kivitendo.

Akasema, majengo ya chuo hicho yatajengwa ndani ya eneo la ekari 300, ikiwa ni pamoja na majengo mbalimbali ya huduma za kijamii.

Mchungaji Lee akasema kwa kuanzia, tayari miradi miwili ya jengo la ufundi stadi na ofisi mbalimbali imekamilika.

"Ujenzi utafanyika kwa awamu, hivi sasa tumeanza awamu ya kwanza kwa kujenga majengo mawili yatakayotumika kwa mafunzo ya ufundi stadi, awamu ya pili itakuwa hospitali na baadhi ya madarasa ya wanafunzi," akasema.

Akaongeza kuwa chuo hicho kitakuwa cha pekee katika ukanda wa Afrika na kwamba wanafunzi watajifunza kinadharia na vitendo chuoni hapo, pasi na matatizo.

"Tunajua wapo Watanzania wenye upeo mkubwa sana. Lakini wameshindwa kuonyesha vipaji vyao kutokana na kukosa nyenzo... tutawapa fursa ili wawe na uwezo zaidi pindi watakapomaliza kwenye chuo hiki," akaongeza.

1 comment:

Maoni yako