Wednesday 8 July 2015

KIKAO CHA KUMPITISHA MGOMBEA WA URAIS CCM: MKUU WA MKOA WA DODOMA ATOA MWONGOZO KWA WAGENI

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
OFISI YA WAZIRI MKUU
TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA


Mkoa wa Dodoma
Anwani ya Simu REGCOM
Simu Nambari: 2324343/2324384
E-Mail No. ras@dodoma.go.tz
Fax No. 255 026 2320046


Ofisi ya Mkuu wa Mkoa,
S.L.P. 914,
DODOMA.TAARIFA YA MKUU WA MKOA WA DODOMA MHE. CHIKU GALLAWA
KWA VYOMBO VYA HABARI

Mkoa wa Dodoma, kwa kipindi cha wiki moja kuanzia leo tarehe 7/7/2015 kutakua na mikutano mikubwa ya Chama cha Mapinduzi (CCM) ikitanguliwa na Kamati Kuu, Halmashauri Kuu na kuhitimishwa na Mkutano Mkuu, ambapo agenda kuu ni kuchagua mgombea wa kiti cha Urais atakayeiwakilisha CCM kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwezi Oktoba.

Mikutano hii yote na shughuli nyingine mbalimbali zinazoendelea hapa Mkoani Dodoma zinajumuisha idadi kubwa ya watu wakiwemo Viongozi Wakuu wa Kitaifa, Viongozi mbalimbali, Wajumbe wa Mikutano hiyo yote na wageni waalikwa mbalimbali. Vilevile wananchi wa Mikoa mingine na hata Mataifa mbalimbali yatakuwa yakifuatilia kinachoendelea hapa Mkoani Dodoma.

Natumia fursa hii, kwa niaba ya wananchi wa Mkoa wa Dodoma, kuwakaribisha wageni wote na Itifaki nzima inayokuja hapa Mkoani Dodoma Makao Makuu ya Nchi na Chama Tawala, kwa ajili ya Mikutano hiyo Mikubwa. Mkoa wa Dodoma una uzoefu wa kubeba matukio makubwa kama haya katika nchi yetu.

Mkoa wa Dodoma tumejiweka tayari kuwahudumia wageni wote kwa huduma muhimu zitakazohitajika kwa kipindi hiki, niwaombe wananchi wa Dodoma hasa wajasiriamali wa bidhaa na huduma mbalimbali kuchangamkia fursa hii kubwa iliyopo hapa Dodoma. Pia kuhakikisha usalama na ubora wa huduma.

Vilevile, kwa niaba ya Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Dodoma, natumia fursa hii kuwataka wananchi wote hapa Mkoani Dodoma na Wageni wote kudumisha hali ya Utulivu, Amani, Ulinzi na Usalama ili mikutano hii yote na shughuli mbalimbali zifanyike kama zilivyopangwa kwa mafanikio. Kila mmoja awe balozi na mlinzi wa mwenzie na Wananchi tuwe wepesi kutoa ushirikiano kwa vyombo vyetu vya ulinzi pale inapohitajika.

Napenda kuwatoa hofu na Mashaka wageni wote na wananchi kwa ujumla hapa Mkoani Dodoma kwamba, vyombo vyote vya Ulinzi na Usalama kwa kushirikiana, vimejipanga na kujiimarisha ipasavyo ili kuhakikisha kwa namna yoyote ile kunakuwepo na Utuivu, Aman, Ulinzi na Usalama.

Niwatahadharishe wale wote wanaojipanga kwa namna moja ama nyingine kushiriki vitendo vya uvunjifu wa Amani, Utulivu, Ulinzi na Usalama kwamba tutawashughulikia kwa mujibu wa sheria za nchi. Asiye mjumbe wa Mikutano na wala siyo mwalikwa ni bora wasije kabisa Dodoma.

Kwa kuwa Mikutano hii itachangia ongezeko la idadi na muingiliano wa watu hapa Mkoani Dodoma, baadhi ya Wajumbe/Wageni watakuwa na vyombo vya Moto vya usafiri, hivyo, niwaombe madereva wote kuendesha kwa ustaarabu mkubwa na kuzingatia sheria za usalama barabarani na udereva wa kujihami, ili kuepusha ajali. Askari wa Usalama barabarani wasimamie kwa makini usalama barabarani.
Ahsanteni sana kwa kunisikiliza
Chiku A. S. Gallawa
MKUU WA MKOA WA DODOMA
Julai 07, 2015

No comments:

Post a Comment

Maoni yako