Sunday 17 July 2016

MHE AUGUSTINE MREMA ATEULIWA MWENYEKITI WA PAROLE

Mh Agustino Lyatonga Mrema Mwenyekiti wa Bodi ya Parole
……………………………………………………………………………………………………………..
Na; Lucas Mboje – Jeshi la Magereza,
PAROLE ni utaratibu wa kisheria unaompa fursa mfungwa aliyehukumiwa kutumikia kifungo Gerezani cha miaka minne na kuendelea kutumikia sehemu ya kifungo chake katika jamii kwa masharti maalum baada ya kukidhi vigezo vifuatavyo:-
i). Awe ametumikia theluthi (1/3) ya kifungo chake na kuonesha mwenendo wa kurekebika kurudi katika jamii kumalizia sehemu ya kifungo chake kwa masharti maalum. Masharti hayo ni kuwa chini ya uangalizi maalum kuhakikisha kuwa hatendi kosa lolote mpaka atakapomaliza kifungo chake, kuzingatia masharti ya Parole anayopewa kikamilifu pamoja na kuwa raia mwema na kuishi kwa kujipatia kipato halali katika jamii;
ii). Awe ameonesha kujutia kosa, kurekebika tabia na kuonesha mwenendo mzuri gerezani na;
iii). Mamlaka husika kujiridhisha kuwa hatahatarisha usalama wa jamii.

Parole ni moja kati ya adhabu mbadala na imeonesha mafanikio makubwa katika nchi nyingi duniani. Utaratibu huu ni wa kipekee kwa kuwa unawagusa wafungwa wa vifungo virefu ambao ndio wengi waliopo magerezani. Aidha, ni utaratibu unaoshirikisha jamii katika urekebishaji kwa kuzingatia usalama wa jamii na dhana kwamba uhalifu ni zao katika jamii.
Madhumuni ya kuanzishwa kwa utaratibu wa Parole nchini hayatofautiani na madhumuni ya kuanzishwa kwa utaratibu huu kwenye nchi nyingine Duniani zikiwepo nchi za Afrika kama vile: Afrika kusini, Zambia na Namibia. Mfumo wa Parole ulioainishwa hapa nchini unatokana na uzoefu wa Parole unaotumika nchini Canada.

No comments:

Post a Comment

Maoni yako