Monday 18 July 2016

JE WAJUA HISTORIA YA KIJIJI CHA GEZAULOLE ("KIJIJI CHA WAZURURAJI")

Picha na maelezo kwa hisani ya Majjid Mjengwa
Ndugu zangu,
Nakumbuka utotoni katika jiji la Dar es Salaam, nilishuhudia kwa macho yangu msako wa wazururaji. Ni katikati ya miaka ya 70.
Niliona jinsi mgambo wa jiji walivyokuwa wakiwadhalilisha vijana na watu wazima kwa kuwakamata, kuwafunga mashati na kuwapandisha kwenye malori tayari kwa safari za kwenda Gezaulole. Kosa lao? Walikuwa wakizurura mijini bila kazi. Hivi, anayetafuta kazi atabaki nyumbani kuisubiri, si ni lazima apige mguu kuitafuta? Nakumbuka kama mtoto nilijisikia vibaya sana kuona udhalilishaji ule uliofanywa kwa watu wazima.
Na sijui leo ukifanyika msako wa wazururaji Dar yatahitajika malori mangapi?
Na miaka ile ya sabini tulipokuwa watoto tulisikia hata nyimbo za redioni kuhimiza ‘ wazururaji’ waende kwenye vijiji vipya vilivyoandaliwa na Serikali kama makazi ya ‘ Wazururaji’. Watoto wa enzi hizo huenda tunakumbuka wimbo huu;
“ Gezaulole baba, Gezaulole mama ee,Twendeni Kibugumo na Mwanadilato kwenye makao mapya,
Gezaulole baba, Geza ulole mama eee!”
Na Kigamboni ya enzi hizo ilikuwa shamba kweli. Wengi wa waliofikishwa huko Gezaulole na vijiji vingine kule Kigamboni wakayaanza maisha mapya ya vijijini.
Kuna waliokimbia Gezaulole wakarudi tena mjini au kwenye vijiji vyao vya asili. Kuna waliobaki huko Gezaulole, wakafyeka mapori yao. Wakaanza kilimo. Wakaizoea hali mpya. Wakajenga familia zao huko.
Ajabu, leo wenye fedha ndio wanaokwenda kuyanunua kwa bei ya hadaa, maeneo ya watoto na wajukuu wa ‘ wazururaji’ wa enzi za Mwalimu. Kuna watoto na wajukuu wa ‘wazururaji’ waliobaki na vieneo vidogo. Miongoni mwao ndio hao wanaofanya shughuli za kusukuma mikokoteni na kuendesha maguta.
Ni Neno La Leo.
Maggid,
Iringa

1 comment:

Maoni yako