Tuesday 28 June 2016

JELA MIAKA 30: KUMPA MIMBA,KUOA AU KUOLEWA NA MWANAFUNZI

BUNGE limepitisha kwa kauli moja Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali Namba 2 ya mwaka 2016 ambayo pamoja na mambo mengine, imeongeza adhabu kwa watu wanaowapa mimba au kuoa ama kuolewa na mwanafunzi, sasa watafungwa jela miaka 30.

Sheria hiyo ilipitishwa jana bungeni mjini Dodoma baada ya Muswada kuwasilishwa Juni 24, mwaka huu na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) ambao baadhi ya wabunge walipata fursa ya kuuchangia.

Muswada huo ulilenga kufanya marekebisho katika sheria 21 kwa lengo la kuondoa mapungufu yaliyobainika wakati wa utekelezaji wa sheria hizo na umepitishwa kuwa sheria.

Sheria zilizopendekezwa kurekebishwa na sheria hiyo ni pamoja na ya Kudhibiti Utakatishaji wa Fedha Haramu; Kudhibiti Usafirishaji Haramu wa Binadamu; Kanuni za Madai; Usajili wa Makandarasi; Elimu; Ajira na Mahusiano Kazini na Sheria ya Taasisi za Kazi.

Muswada huo uliowasilishwa bungeni na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, George Masaju unatamka adhabu ya kifungo cha miaka 30 jela katika marekebisho ya Sheria ya Elimu kwa watakaompa mimba, kumuoa au kuolewa mwanafunzi.

Awali adhabu iliyotamkwa katika sheria hiyo ya elimu ni mshitakiwa akibainika kuwa na kosa kutozwa faini ya Sh 500,000 na iwapo ni kosa la pili anatozwa faini ya Sh 500,000 au kifungo kisichozidi miaka mitatu.

Akiizungumzia sheria hiyo inayosubiriwa kusainiwa na Rais John Magufuli, Masaju alisema inawalinda watoto wote chini ya miaka 18 walioko na wasio shuleni na kuwa kosa hilo likifanywa na mtoto atahukumiwa kwa mujibu wa sheria ya mtoto.

Kifungu cha 60 A (i) kimeeleza kuwa itakuwa kinyume cha sheria katika mazingira yoyote yale kwa mtu yeyote kumuoa au kuolewa na mwanafunzi wa shule ya sekondari au ya msingi na atakayekiuka atafungwa jela miaka 30.

Katika Sheria ya Taasisi za Kazi inataka mwajiri anapokiuka masharti ya sheria ya kazi, ikiwa ni pamoja na kuchelewesha michango ya waajiriwa, kutoza faini na Ofisa wa Kazi ya papo kwa hapo isiyopungua Sh 100,000.

Wakichangia muswada huo, wabunge wameonesha furaha yao juu ya Sheria ya Elimu inayohusu adhabu ya miaka 30 jela. Hata hivyo, pamoja na furaha hiyo, baadhi ya wabunge wametoa angalizo la kutaka kupimwa kwanza DNA kabla ya kutoa hukumu huku wengine wakitaka kuwapo kwa nyongeza ya viboko.

No comments:

Post a Comment

Maoni yako