Wednesday 11 November 2015

SERIKALI YA MAGUFULI KUPUNGUZA WIZARA, KUBANA MATUMIZI

Siku chache baada ya kufuta safari za vigogo nje ya nchi,Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dr John Magufuli anakusudia kufyeka wizara 8 miongoni mwa 28 zilizopo sasa ili kubana matumizi.

Hatua hiyo ya Dr Magufuli ni sehemu ya utekelezaji wa ahadi alizozitoa kwa wananchi wakati akijinadi kwenye kampeni zake za kuwania Urais kupitia Chama cha Mapinduzi-CCM kwamba atapunguza ukubwa wa serikali kwa kuunda baraza dogo la mawaziri.

Katika miaka 10 ya uongozi wa Rais Kikwete, kumekuwa na malalamiko ya ukubwa wa baraza la Mawaziri huku baadhi ya wizara zikiwa na mawaziri watatu.

Kwa mkakati huo,endapo Dr Magufuli ataweza kufyeka Wizara 8, maana yake atakuwa amewatupa nje ya ajira vigogo zaidi ya 20 ambao ni mawaziri na manaibu wao pamoja na makatibu wakuu na manaibu wao ambao kasma zao za mishahara ni mzigo mkubwa kwa serikali

Baraza la kwanza la Rais mstaafu Kikwete mwaka 2005 lilikuwa na Mawaziri na Manaibu wao 60, jambo ambalo lililalamikiwa na wadau wengi kwamba halina tija bali lilikuwa na lengo la kulipana fadhila

Taarifa zaidi zinasema kuwa huenda Rais Magufuli akachelewa uteuzi wa mawaziri hadi Disemba mwaka huu ili kujipa muda zaidi wa kuangalia na kufanya uchambuzi wa wizara zipi za kuzifyeka kwani baadhi hazina tija

No comments:

Post a Comment

Maoni yako