Thursday, 3 December 2015

MHE. RAIS MAGUFULI AONGEA NA VIONGOZI WA SEKTA BINAFSI NCHINI

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akiongea na wadau wa Sekta Binafsi na kuwaahidi kuwapa ushirikiano mkubwa kwani anatambua mchango wao katika ukuaji wa uchumi na kuwasihi kuwa wazalendo katika suala la utoaji kodi ili kulipeleka taifa katika nchi yenye uchumi wa Kati Ikulu leo Jijini Dar es Salaam.
Rais wa Jamhuri ya Muungano Tanzania Dkt.John Pombe Magufuli amewapa siku saba kuanzia tarehe 03/12/2015 wafanyabiashara wote ambao waliingiza mizigo yao bila kulipa kodi wakalipe kwani baada ya hapo watachukuliwa hatua kali za kisheria.

Hayo yamesemwa leo Ikulu jijini Dar es Salaam na Mheshimiwa Rais katika mkutano wake na wadau wa sekta binafsi alipoamua kufanya mazungumzo nao pamoja na kuwasikiliza maoni yao ikiwa ni sehemu ya ahadi zake katika kipindi cha kampeni za kuomba kura za kiti cha Urais,lengo likiwa ni kukuza uchumi wa nchi kupitia sekta binafsi.

Mheshimiwa Rais aliendelea kusema kuwa katika kipindi hichi cha miaka mitano amedhamiria kuijenga nchi na watu wasimuelewe vibaya kwa maamuzi anayofanya kwani ni kwania njema ya kuleta maendeleo na siyo ujeuri.

“Tutaangalia namna ya kupunguza utitiri wa ushuru katika bidhaa mbalimbali,mfano katika kipindi cha kampeni niligundua katika Mkoa wa Kagera na Kilimanjaro wanakolima zao la Kahawa,wamekuwa wakitozwa tozo 26 kwa zao hilo na hiyo imechangia kusababisha wafanyabiashara wa zao hilo kufanya biashara haramu ya kupeleka zao hilo kwa magendo kuuza katika nchi jirani”,alisema Mheshiwa Rais Dkt. Magufuli.

Pamoja na hayo Mheshimiwa Dkt.Magufuli amewaahidi wadau wasekta binafsi ushirikiano mkubwa kwani anatambua mchango wao katika kukuza uchumi na pia amewataka wadau hao kuwa wazalendo na kuliacha kukwepa kulipa kodi ili tuweze kujenga taifa lenye maendeleo makubwa ya kiuchumi.

Mheshimiwa Rais Dkt.Magufuli ameendelea kusema kuwa kama kutakuwa na mfayabiashara yeyote atakayetaka kuwekeza na akakwamishwa na mtu aliyechini ya uteuzi wake basi mtu huyo ataondoka kwani sasa ni wakati wa wadau wa sekta binafsi kuanza kuanzisha viwanda mbalimbali vitakavyo toa ajira.

Pamoja na hayo Mheshimiwa Rais Dkt. Magufuli amewapa mawazo ya kibiashara wadau wa sekta binafsi kuanzisha kampuni ya kutenganisha udongo unaotoka kwenye machimbo ya madini,kuanzisha viwanda vya samaki pembezoni mwa bahari pamoja na kutengeneza samani zitokanazo na mazao ya misitu.

Kwa upande wa Mwenyekiti wa Taasisi ya Sekta Binafsi (TPSF) Bw.Regnald Mengi amesema kuwa wako tayari kumpa ushirikiano mkubwa Mheshimiwa Rais katika kuhakikisha uchumi watanzania unakuwa kwa haraka na pia amemuomba mheshimiwa rais kuendelea kukemea masuala ya rushwa pamoja kusaidia kupunguza utitiri wa kodi.

No comments:

Post a Comment

Maoni yako