Saturday 13 June 2009

MISAMAHA YA KODI KWA TAASISI ZA DINI (KANISA) KUFUTWA


Askofu Msaidizi wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Methodius Kilaini, amesema kulingana na bajeti ya iliyosomwa bungeni jana, maisha bora kila Mtanzania ni ndoto.

Askofu Kilaini alisema Kanisa limesikitishwa na kusononeshwa mno na bajeti hiyo kwa vile imejaa ‘aya’ za kukatisha tamaa.

Alisema hatua ya serikali kufuta misamaha ya kodi kwa vitu vinavyoingizwa na taasisi za kidini kwa ajili ya huduma, imetangaza upya ugomvi na madehebu ya dini na jamii.

Aliongezeka kuwa haelewi sababu za serikali kupuuza kazi njema ya kutoa huduma inayofanywa na taasisi za kidini, hususan makanisa.

Askofu Kilaini alionya kwamba viongozi wa sasa wasijifanye wana busara kuliko Baba wa Taifa, hayati Mwalimu Julius Nyerere, aliyeasisi misamaha hiyo kwa sababu alijua serikali haina uwezo wa kutekeleza wajibu wake kikamilifu.

Naye Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT), Dk Leonard Mtaita, alisema hatua ya kufuta misamaha hiyo itaumiza zaidi Watanzania na kwamba, suala hilo linaweza kuwafanya maaskofu nchini ‘kuandamana’ hadi Ikulu. Dk Mtaita alisema huduma wanazotoa ni kwa ajili ya raia wote, akashangaa kuona serikali imeshindwa kuwasaidia.

“Kwa kifupi tutashindwa kuendelea kutoa huduma za afya na elimu tunazotoa, hii ni nyundo kwenye utosi wa wananchi maskini, ambao licha ya kukosa fedha, lakini hata huduma za afya zipo mbali nao,” alisema.

Askofu Mkuu wa Kanisa la Furaha Tanzania, Jones Mola, alisema amesikitishwa na kufadhaishwa na kitendo cha serikali kufuta misamaha ya kodi kwa mashirika ya dini.

Askofu Mola alisema hakuna kiongozi wa dini anayeondoka na mali, bali miradi mbalimbali inaingizwa nchini kwa lengo la kunufaisha wananchi.


MAELEZO KWA HISANI YA Simon Mhina, Restuta James (Dar) na Salome Kitomari (Moshi).

No comments:

Post a Comment

Maoni yako