MAMLAKA ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), imetangaza kupanda kwa bei ya mafuta kuanzia leo kutokana na mabadiliko ya bei katika Soko la Dunia.
Bei hizo za jumla na rejareja kwa mafuta ya aina zote ya petroli, dizeli na taa zimepanda, ikilinganishwa na bei zilizotolewa mwezi uliopita.
Mkurugenzi Mkuu wa Ewura, Felix Ngamlagosi alisema bei za reja reja, zimeongezeka kwa Sh 17 kwa lita moja ya petroli sawa na asilimia 0.88, dizeli Sh 90 kwa lita sawa na asilimia 5.24 na mafuta ya taa Sh 72 kwa lita, sawa na asilimia 4.28 ikilinganishwa na toleo la mwezi uliopita.
Kwa upande wa bei za jumla, Mkurugenzi Mkuu huyo alisema pia zimeongezeka kwa petroli, dizeli na mafuta ya taa, ambapo bei mpya za jumla zitakuwa Sh 16.56 kwa lita moja ya petroli sawa na asilimia 0.93, dizeli Sh 90.20 kwa lita sawa na asilimia 5.59 na mafuta ya taa Sh 72.29 kwa lita sawa na asilimia 4.58 .
Ngamlagosi alisema kuongezeka kwa bei hizo katika soko la ndani, kwa kiasi kikubwa kumetokana na kuongezeka kwa bei katika Soko la Dunia, na gharama za usafirishaji wa bidhaa hiyo kuja nchini.
Pamoja na mabadiliko hayo yanayoihusu nchi nzima, alisema bei hizo mpya, hazitauhusu mkoa wa Tanga ambapo vituo vya mafuta mkoani humo vimeagizwa kutopandisha bei mwezi huu.
Alisema hatua hiyo inatokana na mkoa huo, kutokupokea mafuta mapya mwezi Julai, na kufanya bei za Agosti kuendelea kutumika kama ilivyokuwa kwa mwezi Julai.
“Mamlaka (Ewura) inapenda kuukumbusha umma kwamba bei kikomo za mafuta kwa eneo husika, zinapatikana vilevile kupitia simu za mkononi kwa kupiga namba *152*00# na kisha kufuata maelekezo, ambapo huduma hii ni bure na inapatikana kupitia mitandao yote ya simu za mkono nchini,” alisema
Wednesday, 3 August 2016
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment
Maoni yako