Sunday, 11 September 2016

WAISLAM ZAIDI YA MILIONI MOJA NA NUSU WAANZA IBADA YA HIJJA HUKO SAUDI ARABIA

Ibada ya Hijja ya kila mwaka inayotekelezwa na Waislamu imeanza Jumamosi (10.09.2016) nchini Saudi Arabia huku hatua kali za kiusalama zikiwa zimeimarishwa kwa takriban mahujaji milioni 1.5 wanaoshiriki hija hiyo.
Baada ya kufanyika kwa taratibu za awali za ibada hiyo katika Msikiti Mkuu katika mji wa Mecca eneo takatifu kabisa kwa Waislamu duniani mahujaji hao Jumamosi wameanza kuelekea eneo la tambarare la Mina lilioko kama kilomita tano mashariki ya Meccca kwa kutumia vyombo mbali mbali vya usafiri na hata kwa miguu chini ya hali ya joto inayopindukia nyuzi joto 40.

Mahujaji hao watakuwa wanafuata nyayo za Mtume Muhammad (SAW) aliyefanya utaratibu huo huo wa ibada miaka 1,400 iliopita.Mamia kwa maelfu ya mahujaji wakiwa katika mavazi yao meupe yasiokuwa na mishono walianza kuondoka mji mtakatifu wa Mecca Jumamosi alfajiri kwa safari yao hiyo ya Mina ambapo watalala huko na watakamilisha hijja kwa kwenda kusimama kwenye mlima Arafat hapo Jumapili.
Tarehe 24 Septemba mwaka jana Mina palikuwa ndio mahala kulikotokea maafa mabaya kabisa katika historia ya hija kutokana na mkanyagano wakati mahujaji walipokuwa wakielekea kwenye Daraja la Jabarat kwa ajili ya kumpiga mawe shetani. Mwaka huu kumpiga mawe shetani kutaanza Jumatatu.

No comments:

Post a Comment

Maoni yako