Monday 26 September 2016

TAMKO LA MHE:RAIS MAGUFULI BAADA YA KUTEMBELEA BANDARI YA DAR

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe 26 Septemba, 2016 ametembelea Bandari ya Dar es Salaam na kuzungumza na wafanyakazi wa bandari hiyo ambapo pamoja na mambo mengine ametoa miezi miwili kwa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) kununua mashine nne za kukagulia mizigo bandarini (Scanning Mashine).

Rais Magufuli ametoa agizo hilo baada ya kubaini kuwa kati ya mashine nne za ukaguzi wa mizigo zilizopo, ni mashine mbili tu ndizo zinafanya kazi na hazina uwezo wa kukagua mizigo yote inayotoka na kuingia nchini kupitia bandari hiyo hali inayosababisha kutokuwepo kwa udhibiti wa uhakika wa udanganyifu.

“Kwa hiyo nawaagiza TPA, na Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi Prof. Mbarawa na Mamlaka ya Mapato mpo hapa hakikiseni mnanunua mashine za kukagulia mizigo nne ndani ya miezi miwili, na ikifika miezi mitano muwe mmenunua mashine sita, ni lazima mizigo yote ikaguliwe kwa mashine” Amesema Rais Magufuli

Dkt. Magufuli ameiagiza (TPA) kwa kushirikiana na Wizara husika kuanza mazungumzo na kampuni ya kimataifa ya kuhudumia shehena ya makasha bandarini (TICTS) ambayo inapakia na kupakua mizigo katika gati namba nane hadi kumi na moja ili kurekebisha mkataba ambao Kampuni hiyo imeingia na Serikali kwa lengo la kuhakikisha nchi inapata manufaa yanayostahili.

Rais Magufuli aliyetembelea eneo la mita za kupimia mafuta yanayopakuliwa melini (Flow Meters) na kubaini kuwa mita hizo hazifanyi kazi, ameiagiza TPA kuharakisha mchakato wa kununua mita mpya na kuzifunga katika eneo hilo ili kudhibiti ukusanyaji wa mapato ya kodi ya mafuta.

Aidha, Dkt. Magufuli ameitaka TPA kujipanga kujenga bandari kavu (ICD) katika eneo la Ruvu Mkoani Pwani ili kuachana na bandari kavu zilizoanzishwa na watu binafsi hapa Jijini Dar es Salaam na ambazo zimekuwa zikitumika kukwepa kodi.

Akizungumza na Wafanyakazi mara baada ya kumaliza kutembelea bandari, Rais Magufuli amewatoa shaka wafanyakazi hao na wafanyakazi wengine Serikalini, kuwa zoezi la kuhakiki vyeti linaloendelea nchi nzima halina lengo la kuwafukuza kazi wafanyakazi bali linafanywa kwa lengo la kukabiliana na tatizo kubwa la wafanyakazi hewa ambao wamefikia 17,500 na pia kuondoa tatizo la wafanyakazi wanaotumia vyeti vya kufoji.

Katika ziara hiyo Rais Magufuli ameongozana na Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi Prof. Makame Mbarawa Mnyaa.

Katika hatua nyingine, Rais Dkt. John Pombe Magufuli amemuapisha Dkt. Zainab Abdi Seraphin Chaula kuwa Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI).

Dkt. Zainab Abdi Seraphin Chaula amejaza nafasi iliyoachwa wazi na Dkt. Deodatus Mtesiwa ambaye amestaafu.

Kabla ya kuteuliwa katika nafasi hiyo Dkt. Zainab Abdi Seraphin Chaula alikuwa Mganga Mfawidhi katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma.

Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam

26 Septemba, 2016

No comments:

Post a Comment

Maoni yako