Thursday 15 September 2016

WAASI WA MAI MAI WATEKA MADREVA WA MALORI WA TZ NA KENYA

Chama cha Wamiliki wa Magari ya Mizigo nchini Tanzania (TATOA) kinaripoti kwamba, waasi wa Mai Mai nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), wamewateka nyara madereva wa Tanzania na kuchoma baadhi ya magari ya mizigo. Waasi hao wanadai dola za Kimarekani elfu nne (karibu shilingi za Kitanzania milioni tisa) kwa kila dereva ama sivyo watawapiga risasi madereva wote. Pia waasi hao wametoa siku ya mwisho (deadline) ya majeshi yanayolinda amani nchini humo kuondoka.

TATOA inasema imezungumza na mmiliki wa kampuni ya Simba Logistics, Mzee Azim Dewji ambaye amethibitisha taarifa hizi na pia balozi wa Tanzania DRC pamoja na Wizara ya Mambo ya Nje tayari serikali inashughulikia suala hili. Jumla ya magariyaliyotekwa ni 12 kati ya hayo magari 8 ya Tanzania na 4 ya Kenya. Magari 4 ya Tanzania yamechomwa moto na madereva wote walichukuliwa na waasi lakini bahati nzuri madereva wawili wa Tanzania walifanikiwa kuwatoroka. Tukio hilo limetokea sehemu inaitwa Kasebebena na Matete, wastani wa kilomita 30 kutoka mji wa Namoya.

TATOA inawashauri wanachama waliopakia mzigo kuelekea huko kuwasiliana na madereva wao ili wasitishe safari, kusubiri taarifa ya hali ya usalama kutolewa.

Mai Mai Kata ni kundi la waasi nchini DRC ambalo linadai kupigania uhuru wa jimbo la Katanga, na linaongozwa na Gédéon Kyungu Mutanga, ambaye aliunda kundi hilo mara tu alipotoroka kutoka gerezani mwaka 2011.

No comments:

Post a Comment

Maoni yako