Saturday 18 June 2016

BARUA YA WAZI KWA MHE FREEMAN MBOWE (CHADEMA/UKAWA)

Na Thadei Ole Mushi.

Kama ni mfuatiliaji wa siasa za Tanzania mbinu ya wapinzania kutoka njee ya bunge kwa sababu mbali mbali haikuanza leo. Na tangu wameaanza kuitumia mbinu hii haijawahi kuwasaidia au hata kueleweka kwa wananchi badala yake sisi wananchi ndio huwa tunapata hasara.

Kwa mara ya Kwanza wapinzani walitoka njee ya Bunge wakati raisi Kikwete alipoingia madarakani kwa mara ya pili kwa kile walichokidai kuwa ni kutomtambua. Walitoka njee wakati wa kuhutubia bunge na kulifungua bunge.

Je waliposusia bunge mwisho wa siku hawakuja kumtambua raisi Kikwete?? jibu ni NDIO wakikuja kumtambua na walivunja rekodi kupiga hodi ikulu kuomba busara za raisi kuliko vipindi vingine vyote.Tuliwashuhudia wakiburudika na juice mara nyingi tu Ikulu wakipata picha ya pamoja nk.

Mara ya pili tunawaona upinzani ukitoka njee kususia bunge la katiba. Mwisho wa siku bunge liliendelea na katiba pendekezwa ikapitishwa bila kuwa na mawazo mbadala ya wapinzani ndani ya katiba ile inayosubiria kupigiwa kura.

Mara ya tatu upinzani unatoka njee kupinga matokeo ya uraisi yaliyompa raisi Magufuli ushindi. Wanatoka siku ya raisi kulifungua bunge kama walivyotoka kipindi cha Kikwete. Raisi analifungua bunge na baada ya hapo bunge lilelile lililopewa uhalali na rais Magufuli baada ya kulifungua wapinzani wanarudi na kulitumia. Na hata sasa wapinzani wameshamtambua raisi Magufuli kuwa ni raisi halali na aliyechaguliwa kihalali.

Mara ya nne ni hili la kumkimbia Dr Tulia. Katika hali ya kawaida nilifikiri wangelifanya hivi kwa siku moja tu. Mpango wa kususia kila siku kumetuathiri sana sisi wananchi kuliko kulivyomuathiri Dr Tulia. Tena wapinzani wanatoka njee kipindi muhimu kabisa ambacho walipaswa kuombea majimbo yao miradi ya kimaendeleo toka kwenye bajeti ambayo itapitishwa muda mfupi ujao.

Upinzani umetoka kwenye mstari wa kujenga hoja hadi kususia kususia mambo ya ajabu ajabu.Nakiri kabisa kuwa kilichoijenga kambi ya upinzani nchini ni hoja zao nzito miaka ya 2005-2015.

Sote tunakumbuka jinsi upinzani ulivyopata umaarufu kwa kujenga hoja za kukataa ufisadi, kudai katiba mpya, swala la Buzwagi, na hata juzi juzi swala la ESCROW. Kafulila pamoja na kutukanwa tumbili alisisimama kidete hadi akafanikiwa kuwangoa kina Warema bungeni na wengineo. Nataka nikuonyeshe nguvu ya hoja ilivyo na mantiki kuliko hii zomea zomea na kutoka nje ya bunge.

Katika nchi zote za jumuiya ya Madola Tanzania upinzani ndio unaongoza kwa kuthaminiwa kuliko nchi zote. Thamani hii upinzani umeshindwa kuutambua na kuutumia kujijenga badala yake wamekimbia na kinachowakimbiza ni kanuni walizojiwekea wenyewe.

Ni Tanzania tu katika ukanda huu Kambi rasmi ya upinzani inatambulika bungeni, kuwa na baraza la mawaziri kivuli, na baadhi ya kamati nyeti zinazogusa maslahi ya Taifa kuwekewa kanuni lazma ziongozwe na upinzani kama PAC nk.

Hii ni fursa ambayo upinzani walipaswa kuitumia kujitangaza kuliko kuzurura njee ya viwanja vya bunge. Inauma sana kuona wanakosea na hawataki kujirekebisha.

Naamini si wabunge wote wa upinzani wanataka kutoka njee ya Bunge lah hasha. Prof Elton Mayo aliwahi kutoa nadharia ya Hawthorne Effect, nadharia ya kisaikolojia ambapo mtu hufanya jambo kwa kuwa tu kuna mtu anayemsimamia kufanya hivyo au anafanya tu kwa kuwa anajua anaonekana anachokifanya. Hivyo unafanya jambo si kwa kuwa unapenda kulifanya ila unafanya kwa kuwa kuna sababu zinakufanya ufanye.Nikiangalia huu utoto anaoufanya Mbatia pamoja na uelewa wake wote naona madhara ya mob psychology.

MBOWE nakuomba usitumie tena mbinu hii haiwajengi inawabomoa.

Ole Mushi.

MwanaCCM mwenye kujali maslah mapana ya nchi.

No comments:

Post a Comment

Maoni yako