Tuesday 27 December 2016

UJENZI WA JULIUS NYERERE I AIRPORT WAFIKIA ASILIMIA 65

Tume ya mipango imefanya ziara katika mradi wa ujenzi wa jengo la III la abiria katika uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere (Terminal III) jijini Dar es Salaam kwa lengo la kukagua maendeleo ya mradi huo na kuelezwa kuwa ujenzi umefikia asilimia 65.

Akitoa maelezo mbele ya timu ya wataalamu kutoka Tume ya Mipango, Meneja wa Mradi huo Mhandisi Mwanaidi Mkwizu alieleza kuwa ujenzi huo unaotekelezwa na Mkandarasi wa kampuni ya BAM kutoka Uholanzi ulioanza Juni 2013 na unatarajiwa kukamilika ifikapo mwezi Desemba Mwaka 2017.
Akielezea miundombinu ya uwanja huo, Mhandisi Mkwizu alisema kuwa uwanja huo wa kisasa una barabara ya kuruka ndege (runway) yenye urefu wa kilometa 3 na upana wa mita 60 ambapo upana unaohitajika kwa matumizi ya ndege ni mita 45.
Aliongeza kuwa mradi huo pia umeangalia changamoto ya kukatika umeme mara kwa mara na kuamua kutafua vyanzo mbalimbali ili kuondokana na utegemezi wa chanzo kimoja ambacho kinaweza kukwamisha shughuli katika uwanja huo pale inapotokea hitilafu.

Alieleza kuwa kutakuwa na njia mbili tofauti za kuleta umeme kutoka TANESCO ambapo njia moja ni kwa ajili ya dharura na pia endapo kutakuwa na tatizo la kukatika umeme kupitia njia za TANESCO, umeme utapatikana kutoka chanzo mbadala cha dharura kwa kutumia jenerata nne kubwa za kisasa za dizeli zilizopo eneo la mradi ambazo zinatosha kukidhi mahitaji ya eneo hilo.
Alisisitiza kuwa tayari wamefanya mazungumzo na TANESCO na kukubaliana kuwa njia hizo za umeme ni kwa ajili ya uwanja huo pekee na hakuna wateja wengine watakaounganishiwa katika njia hizo.
Mhandisi mkwizu alimalizia kwa kusema kuwa yeye pamoja na timu yake ya wataalamu wanaendelea kufanya usimamizi wa karibu ili kuhakikisha kuwa utekelezaji wa mradi huo unaenda sambamba na malengo yaliyopangwa.
Wataalamu wa ukaguzi wa miradi kutoka Tume ya Mipango walipata fursa ya kutembelea maeneo mbalimbali ya ujenzi wa mradi huo na kuonesha kuridhishwa na kasi yautekelezaji huku wakimshauri menejea wa mradi huo kuendelea na ufanisi wake katika kusimamia kazi hiyo ili kuhakikisha malengo ya mradi huo yanafikiwa.

No comments:

Post a Comment

Maoni yako