Tuesday 2 September 2014

MHE. AGUSTINEMREMA(MB) amshitaki MHE.MBATIA KWA RAIS



MBUNGE wa Vunjo, Augustine Mrema (TLP), amemwomba Rais Jakaya Kikwete amnyang’anye ubunge Mbunge wa Kuteuliwa, James Mbatia.
 
Mrema alitoa ombi hilo juzi mjini Dodoma, alipokuwa akizungumza katika kikao kilichowakutanisha wanachama wa Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD) na Rais Kikwete kwa ajili ya kutafuta mwafaka wa Bunge Maalumu la Katiba.
 
Chanzo chetu cha habari kilichokuwa katika kikao hicho kilichofanyika Ikulu ndogo eneo la Kilimani, kilisema Mrema alisema kuwa Mbatia ni mtu hatari kisiasa na anatakiwa kuchukuliwa hatua na Rais Kikwete kwa kuwa ameanza kampeni kabla ya wakati.
 
“Mrema jana (juzi) alikuwa mbogo kwa sababu alipopewa nafasi ya kuzungumza, alimwambia Rais Kikwete amfukuze Mbatia katika ubunge kwa sababu anafanya kampeni katika jimbo lake la Vunjo.
 
“Mrema alisema Mbatia ni hatari sana, akasema pamoja na kwamba anafanya kampeni kabla ya wakati, anayemlaumu zaidi ni Rais Kikwete kwa sababu ndiye amempa jeuri baada ya kumteua.
 
“Alipokuwa akisema hayo, Rais alicheka hadi akanyanyua miguu juu, yaani ilikuwa ni burudani kwa sababu alikuwa akizungumza kwa msisitizo akionyesha kukerwa na Mbatia,” kilisema chanzo chetu.
 
Kwa mujibu wa chanzo hicho, Rais Kikwete alipokuwa akijibu malalamiko hayo, alimtaka Mrema asiwe na wasiwasi kwa sababu wananchi wa Vunjo wanamjua mbunge wao ni nani kati yake na Mbatia.
 
Alipozungumza na MTANZANIA kwa simu jana, Mbatia alikiri Mrema kumshutumu mbele ya rais na kusema kuwa hiyo ni mara ya pili kufanya hivyo hadharani.
 
“Ni kweli alilalamika kwa rais na hii ni mara ya pili, kwani mara ya kwanza alilalamika Agosti 2, mwaka huu katika kikao cha TCD.
 
“Mrema namheshimu sana, namwomba aendelee kuwatumikia wananchi wa Vunjo, ila kwa kuwa anazidi kunifuatafuata, Septemba 6, mwaka huu nitahutubia mkutano wa hadhara huko Vunjo kueleza msimamo wangu,” alisema Mbatia.
 
Naye Mrema akizungumza na MTANZANIA kwa simu, alisema alilazimika kumfikishia kilio chake Rais Kikwete kwa sababu ndiye alimteua Mbatia.
 
“Mbatia ni mtu hatari sana, yaani anakwenda jimboni na kuwaambia wananchi mimi ni mzee, na kibaya zaidi anasema tumekubaliana nimwachie jimbo.
 
“Kwahiyo, ni kweli nilimsema kwa Rais kwa sababu ananifanyia rafu kule jimboni, yaani huyo jamaa ni hatari sana,” alisema Mrema.

Habari hii nikwamujibu wa: Mtanzania

No comments:

Post a Comment

Maoni yako