Sunday 22 May 2016

SURA NNE ZA MHE.RAIS MAGUFULI

JAMII ya Watanzania imetakiwa kujifunza sura za Rais John Magufuli, kutokana na hatua yake ya kutengua uteuzi wa aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Charles Kitwanga.

Akizungumza na gazeti hili jana kuhusu hatua hiyo ya Rais Magufuli, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Tanzania, Johnson Minja, alisema Rais ametuma salamu kwa sura nne kupitia utenguzi huo.

Sura ya kwanza kwa mujibu wa Minja, alisema Rais amewakumbusha watumishi wote wa umma kwamba uadilifu ni jambo muhimu mahali pa kazi, na wanapaswa kuheshimu na kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia muda na sio kutumia muda huo vibaya.

Pili, Minja alisema Rais ametuma salamu kwa walio karibu yake, kwamba uswahiba wao hauhusiani na kazi ya nchi, hivyo suala la kufahamiana si kigezo cha kiongozi avunjaye maadili kuachwa, bali wanapaswa kutambua nchi inaongozwa kwa Sheria na Katiba.

Akizungumzia sura ya tatu ya uamuzi huo, Minja alisema Rais amewakumbusha Watanzania kuwa haangalii muda gani amemteua kiongozi au muda gani ametumikia nafasi aliyopewa, bali kinachoangaliwa ni utendaji kazi wake kwa Taifa.

Aidha sura ya nne, imeelezwa kwamba Rais ameonesha kuwa haendeshwi kwa siasa za vyama kwa kuangalia wanasiasa watasema nini, hasa wakati huu wa uwepo wa Sakata la Kampuni ya Lugumi, na kusema alichoangalia ni kosa limetendeka muda gani.

“Kwa kweli Rais kaonesha ukomavu wake, ameonesha ni Rais mwenye msimamo, bila kusita amefanya uamuzi sahihi, hakuangalia vyama vya siasa vinasema nini, bali aliangalia maadili ya utumishi wa umma yanasema nini na kuchukua hatua,” alisema Minja.

No comments:

Post a Comment

Maoni yako