Wednesday 4 May 2016

MWANAFUNZI GENTRUDE CLEMENT KUSOMESHWA NA TAASISI KIDATO CHA TANO NA SITA

Kwa kutambua umuhimu wa elimu kwa kizazi cha miaka ijayo, Taasisi ya Misaada ya Kijamii ya Hamisi Kigwangalla iliyoanzishwa na Naibu Waziri wa Afya, Ustawi wa Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dkt. Hamisi Kigwangalla imejitolea kumlipia ada Getrude Clement kwa masomo yake ya kidato cha tano na sita.

Uamuzi huo wa kumsomesha Getrude umekuja baada ya jana kukaribishwa kuongea kwenye kikao cha wabunge watetezi wa haki za watoto ambapo Getrude alipata nafasi ya kutoa historia yake ambayo iliwatoa baadhi ya wabunge machozi.

Getrude aliwaeleza wabunge historia yake na hali yake ya kimaisha na kusema kuwa baba yake ni kinyozi na mama yake anafanya biashara ndogo ndogo za nyanya na vitunguu lakini bado amekuwa akijtuma katika masomo yake ambapo kwa sasa yupo kidato cha tatu katika shule ya Sekondari Mnarani, Mwanza.

Baada ya kusema hivyo, ndipo Dkt. Kigwangalla aliamua kujitolea kumsaidia mtoto huyo ili aweze kujiendeleza zaidi kielimu na kufikia malengo yake na zaidi akiahidi kumsomesha katika shule za kisasa ili apate elimu bora zaidi.

“Kwa kuthamini kipaji chake na mchango wake na kutambua nafasi yangu kama Naibu Waziri kwenye Wizara inayosimamia mambo ya Watoto na kama mbunge na mzazi wa mabinti, lakini zaidi kama mtu kutoka kwenye background ya maisha ya chini na ninayethamini mchango wa elimu kwenye maisha yangu, nimeamua kujitolea kumsomesha kidato cha tano na cha sita kwenye shule za kisasa,

“Taasisi yangu ya misaada ya kijamii ya Hamisi Kigwangalla Development Foundation itamlipia ada za masomo yake ya high school,” alisema Dkt. Kigwangalla.

Getrude Clement ambaye ana miaka 16 amepata nafasi hiyo ya kipekee baada ya kupata nafasi ya kutoa hotuba kwa niaba ya watoto na vijana wengine duniani katika mkutano wa Umoja wa Mataifa ambapo alikaribishwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki Moon na kusifiwa na watu mbalimbali duniani kutokana na hotuba yake nzuri.

No comments:

Post a Comment

Maoni yako