Saturday, 24 October 2015

MGOMBEA MWENYE HOFU YA MUNGU

\
HISTORIA ya maisha yake tangu alipozaliwa hadi sasa, John Pombe Magufuli ameishi katika matakwa ya dini ya Kikrosto.

Mbali na kuwa mkristo, mkatoliki, anamheshimu kila mtu. Mwenye imani kama yake, imani tofauti na hata wale wasio na dini, wote anawapa haki sawa. Amemtanguliza Mungu katika kila jambo. Safari yake ya kuomba urais, aliianza kwa kumtanguliza Mungu na kweli akajibu maombi yake. Kumbuka katika safari hiyo kulikuwa na watu 42 waliokuwa wakiwania nafasi hiyo, kila mmoja aliomba kwa imani yake lakini Mungu akamuongoza Mugufuli, akapitishwa.
Mchakato wake wa kutangaza nia ulikuwa wa kimyakimya. Hakutoa ruswa kwa mtu yeyote ili aipate nafasi hiyo japo baadhi ya wenzake walidaiwa kutoa ili waweze kupitishwa na vikao vya chama.

Tangu akiwa shule ya msingi, Magufuli aliishi maisha ya kumpendeza Mungu licha ya kukutana na changamoto mbalimbali zilizosababishwa na ukata.

Alitembea umbali wa kilometa 5 kila siku kutoka kijiji cha Rubambangwe hadi Shule ya Msingi Chato. Hakuwahi kuchelewa. Alikuwa ni mtu wa kujituma, hakupenda kukwazana na mtu. Zaidi alizingatia masomo yake ya kemia na baadaye kuwa mtaalamu aliyebobea katika masomo hayo.

Mwalimu wake, marehemu Cornely Pastory aliwahi kueleza dhahiri kwamba, Magufuli ni miongoni mwa wanafunzi wake waliokuwa wapole, wanyenyekevu ambao hawakuwa na historia mbaya shuleni. Aliiishi kwa matakwa ya Mungu.

Historia yake kimaisha imeendelea kuwa hivyo. Hakuwa mtu wa kujikweza hata alipokuwa waziri. Mke wake aliendelea kuwa mwalimu wa shule msingi. Watoto wake amewalea katika maadili ya dini, amekuwa mzalendo na ndiyo maana hakuna mwanaye hata mmoja aliyekwenda kusoma nje ya nchi kuanzia hatua ya awali hadi chuo kikuu.

Huyo ndiye Magufuli ambaye kwa macho ya kawaida kabisa unaona anatosha kuwa rais. Mahali popote amekuwa akimtanguliza Muingu katika majukumu yake. Baada ya Mungu, anatekeleza sheria ili asimuonee mtu.

Amekuwa akisimamia sheria katika barabara. Tumeshuhudia akivunja nyumba ambazo zimeifuata barabara bila kujali ni ya nani. Anasimamia sheria, hatishwi na tajiri. Anaangalia sheria inasema nini, kama amepindisha basi anapambana naye.

Hofu ya Mungu ndiyo inayomuongoza kusimamia sheria. Anachukia ufisadi na rushwa. Akiwa Wizara ya Ujenzi, amewatimua wafanyakazi wengi wala rushwa. Anatamani kila mmoja ale kulingana na haki yake.

Alipokuwa akihutubia kwenye Uwanja wa Jangwani jijini Dar katika uzinduzi wa kampeni zake, alianza kwa kumtanguliza Mungu mbele. Aliwashukuru Watanzania wote waliojitokeza uwanjani hapo kwa kumuamini, hakumbagua mtu kwa dini, kabila lakini zaidi aliwasalimu katika jina la Mungu.

“Ningependa kushughulika na uchumi wetu, ukue. Kila mmoja wetu awe na uchumi mzuri hususan kwa wanyonge, natamani zaidi niwasaidie hao,” alisema Magufuli kwenye mkutano huo.

Aidha, kwenye hotuba hiyo, Magufuli alitumia muda mrefu zaidi kuwazungumzia Watanzania wa hali ya chini. Hivyo ndivyo alivyokuwa akizungumza katika mikutano yake mingi. Amekuwa akisema matatizo ya Watanzania anayajua.

Aliposema anayajua alimaanisha kwani alieleza wazi kwamba ameyaishi. Amechunga ng’ombe kama wachungaji wengi wa kawaida. Hivyo atafanya kila linalowezekana kuhakikisha anamaliza tatizo la umasikini.

Akaendelea mbele zaidi kwa kuwaahidi Watanzania kwamba anatambua nchi ina watu wenye imani tofauti hivyo wote watakuwa na haki sawa, matatizo yote atayatatua pasipo kujalia itikadi za kivyama, ukabila wala udini.

Magufuli alisisitiza amani. Akazungumzia kudumisha umoja miongoni mwa Watanzania. Alipohamia mikoani, Magufuli alionekana kumtanguliza Mungu katika kila anachokifanya. Aliomba Watanzania wampe kazi ya urais ili awatumikie.

Alieleza sera zake huku akihofia kumdanganya mtu. Alikataa uongo kwani ni dhambi. Alitamka ahadi ambazo anaamini zinatekelezeka.

Kile ambacho aliona hakitekelezeki kutekeleza, alisema dhahiri huku akionesha juhudi za kupatia ufumbuzi.

“Ndugu zangu mimi nasema ukweli. Nasema ukweli kutoka moyoni, nikiahidi kitu lazima nitekeleze. Kwangu mimi ni kazi tu. Siwezi nikasema nitamaliza nyumba zote za tembe nchi nzima kwa wakati mmoja. Huo utakuwa ni uongo. Wanaosema hivyo ni waongo. Tutazipunguza kwa awamu na nina imani ipo siku zitakwisha kabisa,” alisema Magufuli katika moja ya mikutano yake ya kampeni.

Kwenye kipindi cha kampeni, wagombea mbalimbali wamekuwa wakitoa ahadi ambazo ukizitathimini kwa jicho la tatu hazitekelezeki. Kwa Magufuli hilo halipo, yeye amekuwa akiahidi ahadi ambazo anaamini zinatekelezeka.

Hakutaka kuonekana muongo. Hakutaka kutenda dhambi hiyo na ndiyo maana kila alipopita amesisitiza Watanzania wamuombee ili aweze kuifanya kazi ya urais katika matakwa ya Mungu.

“Ndugu zangu nimeomba kazi hii ya urais nikiamini naiweza. Nikiwatazama hapa mlivyokusanyika, mnadhihirisha kwamba mnanipenda. Ndugu zangu mniombee...”-Magufuli.

Ameyasema hayo huku machoni akionesha anamaanisha. Hiyo imemuongezea imani kubwa Magufuli kwa Watanzania. Akizungumzia umasikini anaonekana anaguswa na tatizo hilo, ana kiu ya kutaka kulitatua.

Mungu ni upendo, Magufuli anahiza amani, umoja kwa Watanzania wote kwa sababu ana hofu ya Mungu, huyo ndiye rais mtarajiwa wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania!







No comments:

Post a Comment

Maoni yako