Jeshi la Polisi August 15, 2017 limetoa tamko la kupiga marufuku Waendesha Bodaboda kubeba watoto wenye umri wa chini ya miaka 10 na kwamba atakayekiuka agizo hilo pamoja na mzazi aliyeruhusu mwanawe kubebwa watachukuliwa hatua za kisheria ikiwa ni pamoja na faini, kifungo au vyote viwili.
Kamishna Msaidizi wa Polisi ambaye pia ni Afisa Mnadhimu wa Kikosi cha Usalama Barabarani, Theopista Malya, amesema kuwa watoto wamekuwa kwenye hatari kubwa wakipandishwa kwenye Bodaboda na wakati mwingine waendesha bodaboda hubeba watoto zaidi ya mmoja jambo ambalo ni lazima likemewe.
Aidha, alisema kuwa Jeshi hilo limeandaa kipindi maalumu cha Radio kitakachorushwa na Clouds FM kila siku ya Jumatano saa 2:00 Usiku kikiwa na lengo la kuongeza elimu kwa waendesha Bodaboda katika kuzingatia Usalama Barabarani pindi wanapofanya shughuli zao.
Mwenyekiti wa Taasisi ya Mabalozi wa Usalama barabarani (TSA), John Seka alisema kipindi hicho kitalenga kuwapa elimu waendeshaji wa bodaboda.
Pia, alitumia nafasi hiyo kuwataka wafuate sheria zilizowekwa na Sumatra ili waepukane na mkono wa sheria.
Paulina Shayo ambaye ni mwakilishi kutoka WAT Saccos alisema kuwa wanatoa mikopo kwa bodaboda na kwamba mikopo hiyo itawasaidia kuwa wamiliki halali wa vyombo hivyo.
MAHAFALI YA 16 KIDATO CHA NNE KOM SEKONDARY YAFANYIKA
33 minutes ago