JK akiwa katika mazungumzo White House jijini Washington DC na Rais wa
Marekani Barack Obama na Secretary of the State Hillary Clinton Mei 20 mwaka huu
Rais Barack Obama wa Marekani amemsifia Rais Jakaya Mrisho Kikwete wa Tanzania, akimwelezea kama kiongozi wa mfano ambaye amefanya kazi nzuri ya kupeleka huduma za waziwazi kwa wananchi wake.
Rais Obama amesema kuwa Rais Kikwete ni mmoja wa viongozi wa Afrika walioonyesha uongozi thabiti ambao uko tayari kusonga mbele katika kuwaletea maendeleo wananchi wao.
Rais Obama amemwaga sifa hizo kwa Rais Kikwete katika mahojiano na taasisi ya mawasiliano kwa njia ya inteneti ya AllAfrica.Com wakati akijiandaa kufanya ziara yake ya kwanza katika eneo la Afrika Kusini mwa Sahara, kwa kutembelea Ghana.
Rais Obama aliwasili Ghana usiku wa kuamkia leo (Ijumaa, Julai 10, 2009) kuanza ziara ya siku mbili ya kwanza katika eneo la Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara. Rais Obama anatarajiwa kuondoka Ghana leo kurejea kwao Marekani.
Kabla ya kutembelea Ghana, Rais Obama tayari alikwishakutembelea Bara la Afrika kwa kuzuru nchi ya Misri, iliyoko Afrika Kaskazini katika wiki za karibuni.
Rais Obama ambaye aliwasili Ghana akitokea katika Mkutano wa Nchi Zenye Viwanda Vingi Zaidi Duniani wa G8 nchini Italia, aliiambia taasisi ya AllAfrica.Com katika mahojiano yaliyofanyika Ikulu ya Marekani kabla ya kuondoka kuelekea Russia, Italia na Ghana:
“Lazima kukumbuka kuwa pamoja na kwamba nitaitembelea Ghana kwa ziara hii, tayari nimemkaribisha Tsvangirai wa Zimbabwe katika Ofisi ya Rais wa Marekani. Tulikuwa na Rais Kikwete wa Tanzania kabla ya hapo katika Ofisi hii hii, na katika kila mkutano najaribu kuelezea ujumbe huo huo.”
Aliongeza Rais Obama: “Tumeona kazi nzuri sana inayofanywa na uongozi katika Tanzania ukielekeza nguvu zake katika kutoa huduma za wazi wazi na dhahiri kwa wananchi wake, na kila mahali ambako watu wanataka kujisaidia, na sisi tunataka kuwapo kama washirika wa uongozi.”
Rais Obama alimwalika Rais Kikwete kuwa kiongozi wa kwanza kabisa wa Bara la Afrika kukutana naye katika Ofisi ya Rais wa Marekani tokea kuapishwa kuwa kiongozi wa Marekani Januari 20, mwaka huu.
Rais Kikwete alikutana na kufanya mazungumzo na Rais Obama katika Ikulu ya Marekani mwezi Mei mwaka huu, 2009.
Akisisitiza kuhusu umuhimu wa Bara la Afrika na uongozi wa Rais Kikwete na Afrika kwa jumla, Rais Obama alisema: “Nadhani Bara lote ni muhimu. Na nadhani kuwa tunao uongozi imara katika Bara la Afrika ambao uko tayari kusonga mbele na tunataka kusonga mbele nao.”
Rais Obama pia alisisitiza kuwa Afrika inahitaji kuendelea na juhudi zake za kuimarisha utawala bora, ili kuzidi kuvutia uwekezaji kutoka Marekani.
“Jambo la kwanza ni kwamba itakuwa vigumu kuvutia uwekezaji kutoka nje bila kuwako na utawala bora. Uwekezaji wa namna inayoboresha maisha ya kila siku ya wananchi wa Afrika. Kama maofisa wa Serikali wanataka binafsi kulipwa asilimia 10, ama 15, ama 25 juu ya kiasi cha uwekezaji, hakuna mwekezaji ambaye atakwenda kuwekeza kule. Hilo ni jambo la kwanza.”
Aliongeza kiongozi huyo: “Jambo la pili, nadhani wakati baba yangu aliposafiri kutoka Kenya kuja Marekani na akarudi nyumbani kwenye miaka ya 1960, pato la taifa la Kenya na Korea Kusini lilikuwa sawa...kwa hakika la Kenya lilikuwa kubwa zaidi. Nini sasa kimetokea katika miaka 50 tokea wakati huo hadi sasa?”
Alisisitiza: “Tulichoshuhudia ni Korea kuchanganya uwekezaji kutoka nje, kujishikamanisha na uchumi wa dunia pamoja na mkakati mkali wa aina ya viwanda ambavyo vililenga katika kuzalisha kwa ajili ya kuuza nje, msisitiko mkubwa kwenye elimu ya nguvukazi yenye ujuzi, ikisisitiza kuwa uwekezaji wa nje unakwenda sambamba na upatikanaji wa teknolojia, ili kuweza kuvijenga na kuviendeleza viwanda vya ndani.”
Rais Obama amesema kuwa kwa maana hiyo Afrika inayo mifano ya kuiga. “Hivyo, tunayo mifano. Tunajua kiasi cha kazi na nguvu na juhudi kinachotakiwa. Jambo ambalo hatujaliona ni matumizi endelevu, yasiyoyumba ya mifano hiyo katika Afrika kwa miaka yote hii, na nadhani wakati sasa umefika wa kuanza.”
Ziara ya Rais Obama inafuatia ile nyingine ya kiongozi aliyemtagulia wa Marekani, Rais George W Bush iliyofanyika mwanzoni mwa mwaka jana, akitembelea nchi nne za Afrika, na kukaa muda mrefu zaidi, siku nne, katika Tanzania akiwa mgeni wa Rais Kikwete.