Tuesday, 8 September 2015
VIDEO: MHE. LOWASSA ALIPOINGIZA UDINI KWENYE SIASA
Nimeshtushwa sana na video hii iliyosambaa ikimwonyesha mmoja wa wagombea urais akitumia karata ya udini kuomba kuchaguliwa. Jambo hili halifai kabisa. Tulikemee vikali. Haliendani na misingi ya uwepo wa taifa letu. Hii ni nchi yetu sote. Ni nchi ya wote. Rais atakayechaguliwa atakuwa ni Rais wa wote, si wa Wakatoliki, Walutheli, Waislamu na wengineo. Ni rais wa Watanzania.
Ni imani yetu, kuwa aliyetoa kauli hiyo ni mwanadamu, na ulimi hauna mfupa. Kwamba haraka atarekebisha kauli yake hiyo. Vinginevyo, kwa kuchelewa sana, hata wapinzani wake wa kisiasa, ni kama amewapigia penalti mikononi. Tunaona sasa wakiitumia kikamilifu kauli hiyo yenye kuwakera Watanzania kama mtaji wa kisiasa.
Maana, Watanzania wanajua, kuwa kamba hukatikia pabovu, na palipo na ubovu kwenye kamba inayowaunganisha Watanzania ni kwenye tofauti za kidini kama zikitumiwa kuwatenganisha. Yaweza kuhatarisha amani ya nchi.
Nchi yetu imedumu kwa miaka 54 sasa ikiwa ya amani na utulivu kutokana na misingi imara ya ujenzi wa Umoja wa Kitaifa tuliojengewa na waasisi wa nchi hii. Misingi iliyohakikisha kunakuwepo na Umoja Na Amani. Hizo ni silaha zetu mbili muhimu kama taifa.
Ndani ya miaka 54 ya Umoja Na Amani tumeshuhudia sio tu nchi jirani zikiingia kwenye machafuko na watu kuuana, bali hata nchi za Ulaya zikiingia kwenye vita vya wenyewe kwa wenyewe mfano wa machafuko ya nchi za Balkan. Tanzania kama nchi tumebaki salama. Kamwe tusikubali kuweka rehani Umoja Na Amani ya nchi yetu.
Na tuendelee na ushindani wa kisiasa kwa maslahi mapana ya nchi yetu. Tuendelee kutofautiana na kubishana kisiasa.
LAKINI, tuepuke siasa za kibaguzi, iwe wa rangi, kabila, au kanda. Na chonde chonde, tusitumie karata ya udini katika kufanikisha ushindi kwenye ushindani wa kisiasa
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment
Maoni yako