Thursday, 4 June 2009
FAMILIA YENYE WATU WANAOISHI UMRI WA MIAKA MINGI
NYANYA mmoja aliyekuwa akiishi katika kitongoji cha Fuka Wanri, wilaya ya Siha, mkoa wa Kilimanjaro aliyejulikana kwa jina la Sylvesta David Maimu aliyezaliwa Mei 25, 1901. Bibi Sylvesta, ambaye pia alijulikana kwa jina la Manka, akiwa ni binti wa pili wa Marehemu Isaack Nyaka Mwanri na Paulina Kikoka Mmari, alifariki dunia Jumatano ya Mei 13, 2009 akiwa na umri wa miaka 108. Kama ilivyokuwa katika maisha yake, wazazi wake nao walipata baraka ya maisha marefu. Marehemu Isaack, ambaye ni baba yake, alifariki dunia akiwa na umri wa miaka 87. Na kifo hicho kilitokana na ajali ya kuanguka. Bibi Paulina, ambaye ni mama yake Silvesta, alifariki mwaka 1987 akiwa na umri wa miaka 115. Bibi Nkaushuba, ambaye ni dada mkubwa wa marehemu, alifariki dunia mwaka 1998 akiwa na umri wa miaka 101. Mama Masiwa, ambaye ni mdogo wake marehemu Sylvesta, angali hai akiwa na umri wa zaidi ya miaka 95. Wadogo zake wengine waliofariki hivi karibuni (miaka ya umri yao ikiwa katika mabano) ni Mama Eliesta Mwanri (78) na Mama Anade Nkini (87). Mdogo wake wa mwisho ambaye bado yuko hai ni Adeline Mwanri ambaye ana umri wa miaka 84. Kaka zake, Justo Mwanri na Josiah Mwanri—wote walifariki dunia wakiwa na umri wa miaka 84 na 95. Hadi anafariki dunia, Sylvesta Maimu alikuwa na watoto saba, wajukuu 36, vitukuu 26 na vilembwe watano. Miongoni mwa wajukuu zake ni Dickson Maimu wa Wizara ya Mambo ya Ndani, Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa, na Aneth Mmari (55), wa Shirika la Nyumba la Taifa kama Mhasibu Msaidizi.