Saturday, 11 March 2017

CCM "KIMENUKA"

Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake wa CCM taifa ambaye pia ni mbunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Sophia Simba na wenyeviti wa CCM wa mikoa minne wamefukuzwa uanachama wa chama hicho kwa madai ya ukiukwaji wa maadili ya chama

Mbali na maamuzi hayo, chama hicho pia kimewafukuza uanachama wenyeviti wanne wa mikoa ambao ni pamoja na Ramadhan Madabida (Dar es Salaam), Jesca Msambatavangu (Iringa), Erasto Kwilasa na Christopher Sanya (Mara).

Pia chama hicho kimetangaza kuwavua uanachama wenyeviti wake katika wilaya za Gairo, Babati Mjini, Kinondoni na Longido huku wengine wakipewa onyo kali huku.

Panga hilo pia limefika katika wajumbe wa NEC ambapo ndugu Ali Hera Sumaye kutoka Babati Mjini naye akifukuzwa uanachama na wengine kupewa onyo kali.

Maamuzi hayo yamefanywa katika kikao cha Halmashauri Kuu ya Taifa ya chama hicho (NEC) kilichokaa leo mjini Dodoma kuelekea mkutano mkuu maalum wa chama hicho utakaofanyika kesho JUmapili ya Machi 12, 2017.

Akizungumza na wanahabari mjini humo, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa chama hicho, Humphrey Polepole ametaja maamuzi mengine kuwa ni kutoa onyo kali kwa mjumbe wake wa Kamati Kuu, Dkt. Emmanuel Nchimbi ambaye ni balozi wa Tanzania nchini Brazil, huku Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Dodoma, Adam Kimbisa akisamehewa

"Ndugu Kimbisa amesamehewa makosa baada ya kuomba radhi, kujirekebisha na kuwaongoza vyema wana CCM mkoa wa Dodoma kupata ushindi wa uchaguzi mkuu, Ndugu. Emmanuel Nchimbi amepewa onyo kali na anatakiwa kuomba radhi wanachama na uongozi wa CCM, tunajua huyu ni Balozi wetu Brazil, lakini ametakiwa afanye hivyo mara moja akiwa huko huko Brazil, na taarifa yetu ataipata" Amesema Polepole

Polepole amesema maamuzi hayo ni ya mwisho, na hayatakuwa na nafasi ya kukatiwa rufaa katika ngazi yoyote ya chama hicho.

No comments:

Post a Comment

Maoni yako