RAIS Mstaafu wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete, amewasaa wanafunzi kuchagua kozi zitakazowapatia ajira wanapo hitimu masomo yao.
Akizungumza katika mahafali ya 10 ya kidato cha sita katika Shule ya Sekondari Baobab, wilayani Bagamoyo, mkoa wa Pwani juzi, Kikwete alisema wimbi kubwa la vijana wasio na ajira limechangiwa na uchaguzi mbaya wa kozi ambazo haziendani na soko la ajira la sasa.
“Nawasaa kuwa makini katika kuchagua kozi zinazoendana na soko la jira ndani na nje ya nchi ili muweze kuajiriwa na kujiajiri pindi mnapohitimu,” alisema.
Alisema zipo fursa mbalimbali ikiwamo za kibiashara katika soko la Afrika Mashariki, Afrika na Dunia, ambazo kama wahitimu watasoma kozi zinazoendana na fursa zilizopo watajikomboa na changamoto ya ukosefu wa ajira.
“Nimetembea nchi nyingi duniani na kuona fursa mbalimbali, ni vyema basi vijana wakawa wanafanya maamuzi sahihi ili waweze kutumia fursa hizo.”
“Vijana wengi wamekuwa wakichagua michepuo ya kozi ambazo haziendani na mahitaji ya soko la ajira na kuwafanya kushindwa kupata nafasi katika soko la ajira,” aliongeza kusema.
Aidha, Kikwete alizitaka shule na vyuo nchini kufundisha lugha kubwa duniani kama Kichina na Kifaransa ili kuwaongezea uwezo wahitimu kufanya kazi katika maeneo mbalimbali dunia.
Aidha, alizishauri shule kutoa mafunzo ya ujasiriliamali ili kupanua fikra za vijana na waweze kujitengenezea ajira wanapohitimu.
Naye Mkurugenzi wa Shule ya Baobab alisema shule hiyo imefanikiwa kutoa wahitimu 774 kwa kipindi cha miaka 10, ambao asilimia 95 walipata ufaulu wa kujiunga na vyuo mbalimbali ndani na nje ya nchi.
Alitaja idadi ya wahitimu wa mwaka huu kuwa ni 244, wasichana 176 na wavulana 68.
Wednesday, 4 May 2016
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment
Maoni yako