Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli ameamuru fedha zilizopaswa kutumika kugharamia shamra shamra za siku ya Uhuru ambazo zingefanyika tarehe 09 Desemba 2015, kutumika kufanya upanuzi wa barabara ya Mwenge hadi Morocco jijini Dar es Salaam yenye urefu wa kilometa 4.3 kwa kuongeza njia mbili za barabara za lami.
Tayari fedha hizo kiasi cha shilingi bilioni nne zimepelekwa kwa wakala wa barabara hapa nchini TANROADS kwa ajili ya utekelezaji wa agizo hilo, linalopaswa kuanza mara moja
Akizungumza na Mtendaji Mkuu wa TANROADS Mhandisi PATRICK MFUGALE Ikulu Jijini Dar es Salaam, Dkt. Magufuli ametaka ujenzi wa barabara hiyo uanze haraka ili kukabiliana na adha ya msongamano wa magari katika barabara hiyo
Kujengwa kwa njia hizo kutaifanya barabara ya Morroco hadi Mwenge kuwa na njia tano.
Wakati huo huo, Rais John Magufuli amekutana na kufanya mazungumzo na Mwenyekiti Mstaafu wa Chama Cha wananchi (CUF) Prof. Ibrahim Lipumba Ikulu Jijini Dar es salaam.
Katika Mazungumzo hayo Prof. Lipumba amempongeza Dkt. Magufuli kwa kuchaguliwa kuwa Rais wa awamu ya tano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na pia kwa kutoa hotuba nzuri ya uzinduzi wa Bunge la 11 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania iliyokonga nyoyo za Watanzania.
Kwa Upande wake Rais Magufuli amempongeza Prof. Lipumba kwa msimamo wake thabiti wa kupinga ufisadi na amemtakia heri katika shughuli zake.
Gerson Msigwa
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU.
Dar es Salaam.
30 Novemba,2015
Sehemu ambako utaanzia upanuzi wa barabara ya Mwenge hadi Morocco jijini Dar es salaam yenye urefu wa kilometa 4.3 kwa kuongeza njia mbili za barabara za lami kufuatia agizo la Rais Dkt John Pombe Joseph Magufuli la kutumia fedha shilingi bilioni nne zilizopaswa kutumika kugharamia Shamrashamra za siku ya Uhuru Desemba 9, 2015 kutumika kufanya upanuzi wa barabara hiyo.
PICHA NA IKULU
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment
Maoni yako