Sunday, 16 October 2016

KERO: BARABARA ENEO LA KISUTU MABASI YAENDAYO KASI

Barabara ya mradi wa mabasi yaendayo haraka katika kituo cha Kisutu,kilichopo katika Makutano ya barabara ya Libya na Morogoro,Mtaa wa Mtendeni,Kata ya Kisutu,Manispaa ya Kinondoni,Dar Es Salaam,inaendelea kuchimbika kufuatia sababu mbalimbali ikiwemo kinachoonekana kama mamlaka husika kuzembea ama kutochukua hatua stahiki kunusuru hali ilivyo mahala pale.

Saturday, 15 October 2016

KWA VIATU HIVI KINA DADA KAZI MNAYO

SIMU ZA SAMSUNG GALAXY NOTE 7 MATATANI

MAMLAKA ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imepiga marufuku uingizaji na usambazaji wa simu za mkononi za Smartphone Samsung Galaxy note 7 kwa kuwa zina matatizo ya betri.

TCRA pia imewataka wananchi ambao tayari wanatumia simu hizo kuzizima na kuzirudisha haraka katika maduka walikozinunua.

Meneja Mawasiliano wa TCRA, Innocent Mungy, amewataka watanzania wajihadhari kuitumia simu hiyo kwa kuwa Kampuni ya Samsung yenyewe imeiondoa sokoni.

“Simu hiyo tayari Samsung wenyewe wamesema ina matatizo ya betri na mara mbili sasa imelipuka,” amesema Mungy.

Amewaomba watu wenye simu za aina hiyo kuzirudisha madukani haraka wabadilishiwe ama kurudishiwa fedha zao.

“Hata kama uliletewa zawadi kutoka nje ya nchi nawaomba warudishe huko kuepuka matatizo yanayoweza kujitokeza,” amesema Mungy.

Hivi karibuni simu aina hiyo iliyothibitishwa na kampuni hiyo kuwa ilikuwa salama, ilishika moto kwenye ndege nchini Marekani.

Simu hiyo inadaiwa kushika moto ikiwa mikononi mwa abiria aliyekuwa kwenye shirika la ndege la Southwest Airlines.

Shirika hilo liliwaondoa kwa dharura abiria waliokuwa kwenye ndege iliyokuwa imepangiwa kusafiri kutoka Louisville, Kentucky, hadi Baltimore, Maryland muda mfupi kabla ya kupaa

Friday, 14 October 2016

NYERERE DAY


Mwili wa Hayati Mwl. Nyerere ulipowasili nchini Tanzania Oktoba 18, 1999 kutoka nchini Uingereza.
Mhe Zitto Kabwe asema haya anapokumbuka nyakati za Nyerere
Kuipitia ukurasa wake wa Facebook Zitto kabwe ameanza kuandika hivi...
Nyerere wangu mimi!
Mwaka 1984 nilianza darasa la kwanza katika Shule ya Msingi Kigoma, katika mji wa Kigoma. Nakumbuka kupelekwa Shule siku ya kwanza na mama yangu mzazi Bi Shida Salum (Mungu amrehemu) nikiwa sina viatu yaani pekupeku wala begi la mkononi, nilikuwa nimebeba mfuko wa nailoni. Nakumbuka usiku wa kuamkia siku ya kwanza kwenda shule, sikulala kwa furaha na hamu ya kuwa msomi, nilijisikia fahari kuanza shule japokuwa sikuwa na kitu chochote cha zaida zaidi ya kaptula ya shule na shati liloshonwa kwa kitambaa cha sanda. Pia nilianza shule nikiwa nimechelewa kwa mwaka mmoja maana wenzangu walianza wakiwa na miaka 7. Mwaka 1983 nilipopelekwa shule mkono wangu haukuweza kushika sikio upande wa pili, ambacho kilikuwa kipimo cha kuandikishwa darasa la kwanza.

Hali ya maisha wakati huo ilikuwa mbaya sana. Nakumbuka kwenda shuleni nikiwa sina kitu tumboni au siku nzima nilikunywa uji usio na sukari. Uji wenyewe ulikuwa ni wa unga wa njano uliotokana na mahindi ya njano ambayo tuliambiwa nchi yetu ililetewa kama msaada kutoka nchini marekani.

Shule yetu kama zilivyokuwa shule nyingi za wakati huo hatukuwa na madawati ya kutosha na vyumba vya madarasa vilikuwa vichache sana. Ilikuwa ni kawaida kwa wadogo (darasa la kwanza mpaka la tatu) kusomea chini ya mwembe na kukaa juu ya matofali. Hali hiyo ilipelekea kaptura yangu ya shule kuwekwa viraka vingi maana ilikuwa inachanika mara kwa mara. Nyakati nyingine ilibidi kwenda shuleni na shati likiwa halijakauka hasa siku za alhamis, siku ya usafi na iwapo nikiwa zamu ya mchana kwani nilikuwa nina shati moja tu tena lililotokana na kitambaa cha sanda.


Kwa dhahiri, watoto wa masikini na matajiri tulikuwa shule moja, darasa moja hata wote kukaa kwenye matofali. Watoto watawala na watawaliwa tulicheza mpira pamoja, kuruka dana na hata kuruka kamba. Hatukujisikia wanyonge kwa sababu hatuna viatu au kuvaa kaptura zenye viraka na mashati ya sanda. Kamwe sikumbuki kudharauliwa shuleni sababu ya uduni wa maisha yangu. Heshima ilitokana na uwezo wako darasani na kupitia hilo nilipata marafiki wa kutoka madaraja yote ya maisha. Nakumbuka mtoto wa Mkurugenzi wa Maendeleo Mkoa wa Kigoma ndugu Daniel Masanja ndiye alikuwa rafiki yangu wa karibu na kwa kuwa sikuwa na hata pesa ya kununua bajia wakati wa mapumziko, yeye alikuwa ananinunulia.


Huko baadaye, ada yangu ya kidato cha kwanza ililipwa na Mzee Sebastian Kasomi ambaye mwanaye Kasomi Mabula alikuwa rafiki yangu mkubwa mara alipohamia shuleni kwetu akitokea mjini Shinyanga. Mzee Kasomi alikuwa Mkuu wa idara ya Kodi ya Mapato mkoani Kigoma.


Licha ya uduni wa maisha watoto wengi tuliishi kwa matumaini makubwa sana. Mwalimu wetu Mkuu ndg. Daniel Andulile alikuwa mkali sana kwa watoto wote bila kujali daraja la maisha la wazazi wao. Alikuwa anatucharaza viboko kwa makosa na utundu bila ubaguzi. Alisisitiza sana kusoma kwa bidii ili kujenga Taifa. Dhana hii ya kujenga Taifa iliingizwa kwenye akili zetu na sisi kumeza bila kujali maana yake. Wakati mwingine tulikuwa tunarudi nyumbani huku tukijadili kitoto kuwa tunajenga Taifa. Kila siku mwendo wa kilometa Sita kwenda na kurudi shuleni.


Elimu hii isiyo ya kibaguzi sasa najua ilitokana na sera za Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere. Jitihada zangu darasani ndio ziilikuwa kipimo cha utu wangu na sio uwezo wa kiuchumi wa wazazi wangu.. Elimu iliyompa fursa sawa za kuendelea na kusonga mbele mtoto aliyekuwa kigoma, kantalamba au Dar es salaam. Elimu iliyokuza ndoto, kuinua ari na kujenga matumaini ya kila mtoto wa kitanzania. Elimu iliyovunja na kusambaratisha matabaka ya kiuchumi na dhamana. Elimu iliyojenga uzalendo na hamasa ya kutumikia taifa letu kwa misingi ya haki, uadilifu na upendo.


Sikuwahi kukutana na Mwalimu Nyerere isipokuwa niliwahi kumwona akiwa ndani ya gari nikiwa nimepanga mstari barabarani alipofanya ziara mkoani kwetu mwaka 1987 nikiwa darasa la nne. Lakini nilikuwa kama ninaishi naye kutokana na namna nilivyotaka kuwa kama yeye. Nikiwa darasa la pili nakumbuka katika mkebe wangu ( mathematical set) mkuu kuu niliweka picha ya kukatwa kutoka kwenye gazeti ya Mwalimu na Kawawa. Na nilijisikia fahari kuwa na picha zao, mara zote nilipokuwa nafungua mkebe kutoa kalamu nilijisemea kimoyomoyo, “siku moja nitakuwa kama wewe”


Licha ya maisha magumu tuliyokuwa tunaishi, maisha ya kupanga mawe kwenye mstari wa kununua mahitaji muhimu kama sukari, sabuni na mafuta kutoka duka la ushirika, maisha ya kushindia uji wa yanga na kutembea mwendo mrefu kwenda shuleni, niliishi kwa imani kubwa kuwa mimi na watoto wengine tupo sawa. Usawa katika kupata elimu, usawa katika kucheza na usawa katika ndoto na matumaini. Nimemaliza elimu ya Chuo Kikuu, ndoto niliyoruhusiwa kuwa nayo kwa sababu ya sera za Ujamaa, za Mwalimu Nyerere.


Ujamaa haukuwa katika usawa wa elimu tu ambapo kila mtoto alipata elimu bure na bora katika Shule za umma bila ubaguzi bali pia namna jamii iliishi. Mtoto alikuwa analelewa na jamii nzima. Ukifanya makosa mtaani mzazi yeyote anakuadhibu ili kukurekebisha. Ukifanya jambo jema, mzazi yeyote anakupongeza.


Mwaka 1985 mwezi Novemba nilipokuwa natoka shuleni, karibia na Benki ya Taifa ya Biashara Tawi la Obed Katikaza, nilikutana na Mama Colleta Furugunya tuliyekuwa tunaishi mtaa mmoja na nikimwita bibi Colleta. Aliponiuliza matokeo yangu ya mtihani wa kumaliza muhula wa pili wa darasa la pili kwa kujiamini nikampa karatasi yangu ya matokeo. Nilikuwa nimeshika nafasi ya tatu darasani nyuma ya Ramadhan Kalukula na Haki Manyaga. Bibi Colleta alinishika mkono mpaka duka la Viatu, Bora Shoes na kuninunulia jozi yangu ya kwanza ya viatu. Viatu vile viliitwa Asante Salim, aliyekuwa Waziri Mkuu wa mwisho wa Mwalimu Nyerere ambaye alikuwa anajaribu kubadili hali mbaya iliyokuwepo. Hivyo ndivyo nilivyopata viatu vyangu vya kwanza vya shule. Shukrani kwa sera nzuri ya ujamaa, mshikamano na upendo.


Hizo ni enzi.

Thursday, 13 October 2016

NDEGE 2 MPYA ZA AIR TANZANIA KUANZA SAFARI KESHO Oct 4; NAULI ZAO HIZI

Ndege mbili mpya za Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) aina ya Bombardier Q400 zinatarajia kuanza kazi wakazi wa mikoa ya Mwanza, Arusha na Zanzibar watakuwa wa kwanza kupata ofa.

Ofisa Habari wa shirika hilo, Lilian Fungamtama amesema safari mpya za ndege hizo ikiwamo ya Dar es Salaam - Mwanza, nauli iliyopangwa ni Sh160,000.

Amesema safari za Dar es Salaam - Arusha nauli yake itakuwa Sh180,00 na Zanzibar - Dar es Salaam ni Sh85,000.

“Ofa hii imetolewa na ATCL kwa safari mpya za ndege hizo,” alisema Fungamtama.

Amesema hakutakuwa na safari ya moja kwa moja kutoka Dar es Salaam kwenda Zanzibar, lakini itakuwapo ya kutoka Dar es Salaam -Arusha hadi Zanzibar.

“Ndege ya kutoka Dar es Salaam kwenda Arusha ndiyo itakayokwenda kuchukua abiria Zanzibar haitatokea Dar es Salaam moja kwa moja,” alisema.

Akifafanua kuhusu nauli hizo, Fungamtama alisema nauli ya kutoka Dar kwenda Kigoma itakuwa katika madaraja mawili ambayo ilikuwapo tangu awali.

Amesema bado ndege hizo hazijaanza safari katika mikoa yote hadi hapo watakapotangaza.

Akizungumzia safari za nje ya nchi, alisema itakuwapo ya kutoka Dar es Salaam - Hahaya hadi Comorro ambayo nauli yake ni Sh543,950 kwenda na Sh926,650 kwa kwenda na kurudi.

“Lengo letu ni kutoa huduma nzuri itakayomridhisha kila mteja,” alisema Fungamtama.

Wednesday, 12 October 2016

MWL NYERERE AENZIWA KWENYE JENGO JIPYA LA UMOJA WA AFRIKA

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel amezindua jumba jipya makao makuu ya Umoja wa Afrika ambalo limepewa jina la Rais mwanzilishi wa taifa la Tanzania, Julius Nyerere.
Jumba hilo ambalo jina lake kamili ni Jumba la Amani na Usalama la Julius Nyerere limejengwa kwa ufadhili kutoka Ujerumani.
Litakuwa makao ya idara ya Amani na Usalama ya AU na litatumiwa pia na maafisa wa kutoa tahadhari ya mapema kuhusu mizozo barani pamoja na kuratibu juhudi za kulinda amani za AU.
Ujenzi wa jumba hilo, ambalo ukubwa wake wa sakafu ni mita 13,500 mraba na linaweza kutumiwa na wafanyakazi 360, uligharimu euro 27 milioni.
Jumba hilo Ofisi za kufanyia kazi, vyumba vya mikutano vya kutumiwa na Baraza la Amani na Usalama, chumba cha kuratibia shughuli, maktaba na vyumba vya shughuli za pembeni.
Mwalimu Nyerere, ambaye alikuwa rais wa Tanzania hadi 1985, alikuwa mmoja wa viongozi waanzilishi wa Muungano wa Nchi za Afrika (OAU) ambao sasa ni Umoja wa Afrika (AU).
Alishiriki sana katika jitihada za kuendeleza bara la Afrika na kusaidia mataifa ambayo hayakuwa yamepata uhuru kujipatia uhuru wake.
Mwalimu Nyerere alipigania sana kumalizwa kwa ubabe wa Wazungu katika nchi za Rhodesia (sasa Zimbabwe), Afrika Kusini, na taifa la Kusini Magharibi mwa Afrika/Namibia (sasa Namibia).

Tuesday, 11 October 2016

MHE BAKHRESA WA AZAM KUJENGA VIWANDA ZAIDI

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akiwa katika mazungumzo na Mwenyekiti wa makampuni ya Azam Bwana Said Salim Bakhresa ambapo alimueleza waziri mkuu nia yake yakuendelea kujenga viwanda zaidi vya kusindika matunda na chakula mazungumzo hayo yamefanyika ofisini kwa waziri mkuu magogoni Dar es salaam leo Picha na Chris Mfinanga

Sunday, 9 October 2016