Sunday, 19 April 2015

KUELEKEA UCHAGUZI MKUU.....

Kutokana na tafiti mbalimbali zilizofanywa hapa nchini na baadhi ya taasisi za utafiti, Mh. Edward Lowassa amekuwa akitajwa kama mwanasiasa anayeongoza kwa kukubalika zaidi kwa mujibu wa hizo tafiti zao.
Je, kwa mtazamo wako wewe, kweli anafaa kuwa Rais?

Saturday, 18 April 2015

KUTOKA MAGAZETINI

MADEREVA KUWENI MAKINI MTATUMALIZA

Imekuwa ni wimbo sasa kila kukicha watu wanapoteza maisha yao kwa ajali zinazoepukika. Kumekuwa na uzembe mwingi wa madereva barabarani. Tunawaomba wathamini utu na uhai wa kila mtu. Ajali nyingi zinaepukika tukiwa makini na kujali uhai.
Dreva huyu wa Basi la Taqwa yupo katika kona lakini analipita Lori la Mafuta. Hii ni hatari sana. Kwanini usiwe na subira?
Sehemu za kona kama hizi usilipite gari jingine (Donnot overtake)

Friday, 17 April 2015

WAZIRI SAMWEL SITTA AFANYA MAAMUZI MAZITO TRL(Reli) NA TPA(Bandari)

SERIKALI imewasimamisha kazi karibu viongozi wote wakuu wa Kampuni ya Reli nchini (TRL), kwa kile kilichoelezwa kuwa hujuma ya mabilioni ya shilingi yaliyotumika kununua mabehewa chakavu.

Waliosimamishwa ni pamoja na Mkurugenzi Mtendaji, Kipallo Kisamfu, Mhandisi Mkuu wa Mitambo, Ngosomwile Ngosomiles, Mhasibu Mkuu, Mbaraka Mchopa, Mkaguzi Mkuu wa Ndani, Jasper Kisiraga na Meneja Mkuu wa Manunuzi wa kampuni hiyo, Ferdinand Soka.

Wakati hayo yakiwakuta hao, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Bandari (TPA), Madeni Kipande aliyekuwa amesimamishwa kazi kutokana na tuhuma mbalimbali, sasa amefukuzwa rasmi.

Hayo yaliwekwa hadharani jana na Waziri wa Uchukuzi, Samuel Sitta alipokutana na waandishi wa habari na kutoa taarifa ya uchunguzi kuhusu ununuzi wa mabehewa machavu katika Kampuni ya Reli nchini.

Sitta, mmoja wa wanasiasa wakongwe aliyeshika nyadhifa mbalimbali serikalini ikiwa ni pamoja na uwaziri tangu enzi za utawala wa Awamu ya Kwanza chini ya Mwalimu Julius K. Nyerere, alisema mbali ya madudu yaliyoonekana katika kamati iliyoundwa na mtangulizi wake katika wizara hiyo, Dk Harrison Mwakyembe, waligundua mambo mengi Jumatatu wiki hii.

Yaliyogunduliwa ni pamoja na ukiukwaji mkubwa wa masharti ya mkataba wa ununuzi wa mabehewa hayo, kwani mzabuni alilipwa fedha zote, tofauti na taarifa za awali iliyoonesha malipo yangefanyika kwa awamu.

“Hivyo wizara ina maoni kwamba mazingira ya utekelezaji wa mkataba huu yana dalili za hujuma kwa TRL na kwa nchi yetu na siyo uzembe,” alisema Sitta.

Akifafanua hilo alisema TRL iliagiza mabehewa ya mizigo 274 ambapo zabuni ilikwenda kwa Kampuni ya Hindustan & Industrial Engineering Limited ya India, ambapo katika uagizwaji wa mabehewa hayo kulikuwa na uzembe katika ufuatiliaji kiwandani, pamoja na uzembe katika kuyapokea yakiwa mabovu.

Alisema mabehewa hayo yalipofikia 150 aliyazuiwa, hivyo 124 yakawa bado hayajafika nchini. Sitta alisema kwa mujibu wa taarifa alizonazo ilibidi mpaka sasa asilimia 50 ya gharama ya mabehewa hayo iwe imeshalipwa, lakini kinyume chake nyaraka zinaonyesha mpaka sasa pamoja na kuzuiwa kwa mabehewa 124 mzabuni huyo ameshalipwa asilimia 100.

“Huu ni uzembe, ni hujuma kama kiongozi sitamstahi yeyote atakayekuwa sehemu ya hujuma,” alisema Sitta.

Alisema kutokana na hali hiyo ameagiza kwamba uchunguzi wa kubaini uwezekano wa hujuma ufanyike, hivyo amemwelekeza Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi, Dk Shaaban Mwinjaka asimamie kuundwa kwa kamati ya uchunguzi.

Alisema kamati hiyo itaongozwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa kushirikiana na Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (TAKUKURU), Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi katika Sekta ya Umma (PPRA), na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Sitta ametoa wiki tatu kuanzia Jumatatu ijayo Aprili 20, mwaka huu kuchunguza na kukamilisha kazi. Katika kipindi hicho, viongozi wakuu wa kampuni hiyo ya reli wanaowajibika na mkondo wa kashfa hiyo ya uagizaji na malipo ya ununuzi wa mabehewa hayo wote wamesimamishwa kupisha uchunguzi huo.

Aidha, alisema tangu mwanzoni mwa mwaka huu serikali ilikuwa ikifanyia kazi tuhuma zinazohusu mabehewa mabovu ya mizigo yaliyoagizwa kutoka India na TRL, baada ya kukamilika kwa uchunguzi wa tuhuma hizo na kamati iliyoundwa na Mwakyembe, aliagiza bodi ya wakurugenzi ya TRL ipitie taarifa hiyo na maelezo ya suala zima la mabehewa hayo.

Alisema katika uchunguzi huo ilibainika kuwa mabehewa mengi kati ya yaliyoagizwa yana kasoro, pia kulikuwa na uzembe katika uagizaji na ufuatiliaji kiwandani yalipokuwa yanatengenezwa na kulikuwa na uzembe katika kuendelea kuyapokea mabehewa hayo pamoja na ubovu wake kujulikana.
(Fundi wa Shirika la Reli Tanzania , Francis Mpangala naye akikaza nati katika moja ya mabehewa hayo. )

Alisema amemteua Elias Mshana kukaimu nafasi ya Mkurugenzi Mtendaji hadi hapo uchunguzi utakapokamilika. Pia ameagiza bodi ya wakurugenzi ya TRL ikutane kuteua watumishi wenye sifa kukaimu nafasi wanaozishikilia waliosimamishwa kazi.

Kipande wa TPA
Akizungumza suala la Kipande, Kaimu Mkurugenzi wa Mamlaka ya Bandari aliyekuwa amesimamishwa kazi tangu Februari 16, mwaka huu ili kupisha uchunguzi wa tuhuma mbalimbali dhidi yake, Sitta alisema Tume aliyoichagua ilikamilisha kazi yake Machi 20, na kumkabidhi taarifa ya uchunguzi wao Machi 24 kwa hatua zaidi.

“Baada ya kuisoma taarifa ya tume na hatimaye kushauriana na taasisi mbalimbali zinazohusika na masuala haya, tumeridhika pasipo mashaka yoyote kwamba isingefaa Madeni Kipande kuendelea na kazi ya kuongoza Mamlaka ya Bandari.

“Hii ni kutokana na kuridhika na utawala mbovu aliouendesha uliosababisha manung’uniko mengi miongoni mwa wateja na wadau wa bandari na mgawanyiko mkubwa wa wafanyakazi,” alisema Sitta.

Alisema kutokana na hali hiyo, serikali imeamua kumrejesha Kipande Idara Kuu ya Utumishi ili aweze kupangiwa majukumu mengine.

“Kipande ameonekana hafai kuongoza bandari ana maamuzi ya pupa, yasiyofuata taratibu pia yenye karaha. Tulichunguza uwezo wake wa kuendesha mamlaka ya bandari sasa kishapwaya inabidi arudishwe utumishi.

Hapa hatujachunguza masuala ya jinai, bali uwezo wa kutenda kazi,” alisema Sitta.

Tangu kusimamishwa kwa Kipande ambaye alikuwa anakaimu nafasi ya Mkurugenzi Mkuu, Ephraim Mgawe aliyekuwa ameondolewa kutokana na tuhuma mbalimbali, nafasi hiyo sasa inashikiliwa na Awadhi Massawe aliyepata baraka za Waziri Sitta na kuendelea kuwa Kaimu Mkurugenzi Mkuu TPA.

NEC - "UCHAGUZI MKUU HAUTASOGEZWA MBELE"

Tume ya uchaguzi nchini (NEC)imesema tarehe ya Uchaguzi mkuu Mwaka huu iko pale pale ambapo ni siku ya terehe 25 mwezi octoba mwaka huu.

Kauli ya NEC inakuja ikiwa ni siku moja kupita baada ya Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo Chadema Freeman Mbowe kuitangazi serikali kiama endapo itasogeza mbele tarehe ya uchaguzi mkuu

Akifanunua Kauli hiyo ya Mbowe leo Jijini Dar es Salaam,Mwenyekiti wa NEC Jaji mstaafu Damian Lubuva wakati wa Mkutano na Waandishi wa Habari amesema taarifa zinazosemwa na wanasiasa kwamba tume hiyo itasogeza mbele uchaguzi Mkuu si za kweli na zinalengo la kuwachanganya wananchi kwani tume hiyo inakwenda vizuri na uandikishaji wa Mfumo mpya wa BVR.

Jaji Damian ameongeza kuwa kwa sasa Uandikishaji wa Wapiga kura kwenye Mkoa wa mdogo wa Njombe unatarajia kumalizika kesho na kuanza rasmi uandikishaji kwenye mikoa mingine ya Mtwara,Lindi na Iringa ambapo amasema kwa sasa watafanya kwa kasi zaidi.

Amebainisha kuwa tatizo lililokuwa linawakabili kwa kuwa na mashine chache za uandikishaji wamelitatua kwakuwa sahivi tayari mashine nyingine 1600 zinatarajiwa kuwasili kesho, jambo ambalo anadai litafanikishwa kasi ya uandikishaji.

Aidha,amesema shehena nyingine ya mashine inatarajiwa kuja tarehe 25 mwezi huu na mpaka ifikapo mwezi wa Sita mwaka huu watakuwa wameshapata mashine zote elfu nane walizokuwa wakizihitaji , jambo ambalo amesema litawafanya wamalize kuwaandisha wananchi nchi nzima mwezi wa saba mwaka huu

AFRIKA KUSINI HALI SI SHWARI

Kwa siku kadhaa sasa hali imekuwa si shwari nchini Afrika Kusini kufuatia mapigano ya kupinga wahamiaji nchini humo. Wakazi wa zehemu mbali mbali nchini humo wamekuwa wakiua wahamiaji, kuchoma nyumba na mali zao mbalimbali wakipinga uwepo wao nchini humo. Hili limetia dosari maana ni Waafrika wanawaua waafrika wenzao.
Askari wakiweka lindo katika eneo la machafuko
Raia wakikimbia bomu la machozi

AJALI NYINGINE MBEYA LEO

Watu 19 wamefariki dunia baada ya Hiace waliokuwa wakisafiria kuacha njia na kupinduka maeneo ya Kiwira wilayani Rungwe Mkoani Mbeya.Ajali hii inafuatia madereva wa mabasi makubwa kugoma kusafirisha abiria na Hiace kuchukua jkumu. Dreva wa basi hili dogo alikuwa kwenye mwendo mkali na kushindwa kulimudu kisha kupinduka na kutumbukia mtoni. Mwenyezi Mungu awaweke marehemu wote palipo pema AMINA.(Tunaomba radhi kwa Picha.)

CHAKULA MUHIMU LAKINI KULA KWINGINE MTIHANI

Familia moja nchini India imepata wakati mgumu kufuatia watoto wao kuwa na maumbo makubwa kupita umri na kimo chao.
Wazazi wao wamesema wamekuwa wakipata wakati mgumu wa kuwahudumia watoto hao chakula kutokana na kula chakula kingi, kwa wiki wanakula chakula kinachotosha kuliwa na familia mbili kwa mwezi mzima

Thursday, 16 April 2015

TUNAELEKEA WAPI?

KWA MTINDO HUU AJALI HAZIEPUKIKI

Imekuwa tabia ya madreva wengi kudharau sheria za barabarani na hata matumizi ya busara wanapokuwa wanaendesha vyombo vya moto. Tazama picha hizi hapa chini kwa hisani ya Michuzi Blog.
Tusaidiane tudhibiti ajali. Toa taarifa uonapo ukiukwaji wa sheria za barabarani