Katibu Mkuu wa Chama Cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad anatarajiwa kuzuru mikoa ya Kusini mwa Tanzania katika kipindi ambacho bado kuna sintofahamu kuhusu nafasi ya Uenyekiti wa chama hicho.
Mwanasiasa huyo ambaye ataongozana na Mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi ya chama hicho, Julius Mtatiro pamoja na Wajumbe wa Baraza Kuu watazuru Mtwara na Lindi ikiwa ni miezi michache baada ya Mwenyekiti wa chama hicho anayetambuliwa na Ofisi ya Msajili wa Vyama Vya Siasa, Profesa Ibrahim Lipumba kuzuru eneo hilo la kusini.
Akizungumzia ziara hiyo, Naibu Mkurugenzi wa Habari, Uenezi na Uhusiano wa Umma wa chama hicho, Mbarala Maharagande alisema kuwa lengo la ziara hiyo ni kukagua shughuli za chama na kupokea maoni ya pamoja ya namna ya kuboresha utendaji wa chama hicho kwa ngazi za chini.
Maalim Seif anatua katika eneo hilo wakati ambapo kukiwa na mvutano baada ya baraza la madiwani kufanya jaribio lililoshindikana la kumng’oa Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Mtwara Mikindani, Geofrey Mwanchisye.
Jaribio hilo liligonga mwamba baada ya Mwanasheria wa Halmashauri hiyo, Sifaeli Kulanga kueleza kuwa hoja zao hazina msingi kwani tuhuma zao kuhusika na matumizi mabaya ya fedha za umma yanakinzana na ripoti ya kamati maalum iliyoundwa na Mkuu wa Mkoa wa Mtwara.
Kesi kuhusu Uenyekiti wa chama hicho inaendelea Mahakamani ambapo Baraza Kuu la chama hicho linapinga barua ya Msajili inayomtambua Lipumba kama Mwenyekiti wa chama hicho wakati ambapo Baraza hilo lilikuwa limetangaza kumfuta uanachama.
No comments:
Post a Comment
Maoni yako