Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli, amewapongeza wachezaji wa Timu ya soka ya Wanawake ya Tanzania Bara (Kilimanjaro Queens) kwa kuandika historia ya kuwa Mabingwa wa kwanza wa Michuano ya kugombea kombe la Chalenji kwa nchi za Afrika Mashariki na Kati (CECAFA Challenge) iliyofanyika katika Mji wa Jinja nchini Uganda.
Kilimanjaro Queens imefanikiwa kutwaa Ubingwa huo baada ya kuibwaga Kenya (Harambee Starlets) kwa mabao 2-1 katika mchezo wa fainali uliofanyika jana tarehe 20 Septemba, 2016.
Katika pongezi hizo alizozitoa kupitia kwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Nape Moses Nnauye, Rais Magufuli amesema Timu ya Kilimanjaro Queens imeandika historia ambayo inalipa heshima Taifa na inaamsha morali kwa wanamichezo kufanya vizuri katika mashindano.
“Mhe. Waziri Nape Nnauye naomba unifikishie pongezi nyingi kwa Wachezaji wa Kilimanjaro Queens, Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Walimu na Viongozi wa Timu pamoja na wadau wote waliochangia kuiandaa Timu yetu ya Taifa ya wanawake ambayo hatimaye imepata ubingwa katika michuano hii mikubwa.
“Nimefurahishwa sana na ubingwa huu na nawaomba wachezaji wa Kilimanjaro Queens na wanamichezo wengine hapa nchini kuuchukua ushindi huu kama changamoto ya kuongeza juhudi katika michezo yetu ili nchi isiishie kupata ubingwa wa Chalenji bali pia ipate ushindi katika michezo na michuano mingine mingi ambayo hushiriki” Amesema Rais Magufuli.
Rais Magufuli pia amewaomba Watanzania wote kuendelea kuwaunga mkono wanamichezo na kuwatia moyo wachezaji kwa kuwa mafanikio yao yanaitangaza nchi na yana mchango mkubwa katika maendeleo.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
21 Septemba, 2016
No comments:
Post a Comment
Maoni yako