Sunday, 31 January 2016

WAZIRI MKUU MHE:MAJALIWA KASSIM AHUDHURIA IBADA ZA KUMWINGIZA KAZINI ASKOFU WA KKKT MHE: DK:SHOO MJINI MOSHI

Mhe Waziri Mkuu akitoa hotuba fupi katika Hafla hiyo
Mhe Waziri Mkuu akipokea yawadi ya picha kutoka kwa Askofu Fredrick Shoo
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na Askofu Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Askofu Frederick Shoo (kulia) na Askofu Mkuu wa KKKT Mstaafu Alex Malasusa baada ya ibada ya kumuingiza kazini Askofu Shoo iliyofanyika kwenye Kanisa Kuu la KKKT mjini Moshi Januari 31, 2016.

Saturday, 30 January 2016

HONGERA KAKA MJENGWA WA MJENGWA BLOG KWA KUSHIRIKI MARATHONI DODOMA

Kukamilisha kilomita 21.1. Milima ya kwetu Iringa iliniweka kwenye form nzuri kuikabili tambarare ya Dodoma.
Pichani nikimalizia mita 100 za mwisho, na kiukweli hata zingeongezwa kilomita kumi nyingine ningezimaliza. Ahsante kwa milima ya kwetu!
Najipanga sasa kuukabili Mlima Kilimanjaro mwezi Juni mwaka huu. Nataka kuhamasisha Watanzania wa Nyumbani Na Diaspora kuutangaza mlima huu mrefu kuliko yote Afrika sambamba na kuutetea theluji yake isije ikayeyuka kutokana na Mabadiliko ya Tabia Nchi ikiwamo uharibifu wa mazingira yanayouzunguka mlima huo.
Viongozi wengine walioshiriki

MHE:MAKAMU WA RAISI SAMIA SULUHU AHUDHURIA KIKAO CHA WAKUU WA MCHI YA AFRIKA HUKU ETHIOPIA

Akipokea Gwaride la Heshima kutoka kwa Jeshi la Ethiopia
Akifuatilia kwa makini Kikao hicho


Friday, 29 January 2016

ZITTO KABWE TENA

Zitto Kabwe kupitia ukurasa wake wa Facebook ameweka wazi jambo ambalo serikali inapaswa kufanya baada ya uchaguzi na kusema ni kuwasilisha mpango wa maendeleo wa miaka mitano.

"Shughuli ya kwanza ya serikali baada ya uchaguzi ni kuwasilisha mpango wa maendeleo wa miaka mitano ( kutafsiri ilani yake kwenda kwenye mpango wa utekelezaji) . Bunge linapaswa kujadili na kuidhinisha Mpango wa Maendeleo wa miaka 5 na kisha Mpango wa mwaka mmoja kuanza kutekeleza Mpango huo wa miaka 5. Kwa mujibu wa Katiba ya JMT Ibara ya 63(3)(c), Mpango wa Maendeleo wa miaka 5 hutungiwa sheria kwa ajili ya utekelezaji." Alisema Zitto Kabwe

"Leo Serikali ya Rais John Magufuli ilipangiwa kuwasilisha Mpango huo wa Maendeleo wa miaka 5. Imeshindwa. Imeleta mwelekeo wa Mpango. Haikuleta sheria na Kamati ya Bajeti Imeleta maelezo yake kuhusu Mpango wa Maendeleo wa mwaka mmoja ilhali hakuna Mpango wa Miaka 5.

"Mwenyekiti Chenge alitaka wabunge wajadili kwa mujibu wa kanuni ya 94 ambayo kimsingi ni Kanuni inayohusu Mpango wa mwaka mmoja. Serikali imejichanganya. Uongozi wa Bunge umechanganyikiwa." Aliongeza Zitto Kabwe

Zitto Kabwe alimaliza kwa kusema kuwa ni aibu kubwa kwa serikali inayojinasibu kwa kauli ya "Hapa kazi tu"

"Bunge linapaswa kuagiza Serikali ikalete Mpango wa Maendeleo wa miaka 5 ili uidhinishwe na utungiwe Sheria kabla ya kuanza kujadili mipango ya mwaka mmoja mmoja.

"Ni aibu kubwa kwa Serikali ya ‪#‎HapaKaziTu‬ kushindwa kuleta Bungeni Mpango wake wa Maendeleo wa miaka 5 na hata ule wa mwaka wake wa kwanza. Itapangaje bajeti zake? Itatekeleza vipi ilani yake? Kuongoza nchi sio kutumbua majipu tu, ni kuendesha nchi." Alimaliza Zitto Kabwe.

CUF WAGOMEA KURUDIA UCHAGUZI WA MACHI 20

Azimio La Baraza Kuu La Uongozi La Taifa Kuhusu Tangazo La Mwenyekiti Wa Tume Ya Uchaguzi Ya Zanzibar La Kuitisha Uchaguzi Wa Marudio Zanzibar

Baraza Kuu la Uongozi la Taifa la THE CIVIC UNITED FRONT (CUF – Chama Cha Wananchi), likiwa ndiyo chombo cha juu cha maamuzi katika Chama baada ya Mkutano Mkuu wa Taifa, limefanya kikao cha dharura leo, tarehe 28 Januari, 2016, katika Ofisi Kuu ya CUF, mjini Dar es Salaam.

Kikao hicho kilikuwa na ajenda moja tu, ambayo ni kufanya maamuzi kuhusiana na tangazo la Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar la kuitisha uchaguzi wa marudio.

Baada ya kujadili kwa kina tamko hilo la Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar, Jecha Salum Jecha, la kuitisha uchaguzi wa marudio tarehe 20 Machi, 2016 na mwenendo mzima wa hali ya kisiasa Zanzibar tokea alipotoa tamko lake batili la tarehe 28 Oktoba, 2015 kudai kwamba amefuta uchaguzi mkuu wa Zanzibar wa tarehe 25 Oktoba, 2015 na matokeo yake, Baraza Kuu la Uongozi la Taifa limefikia maazimio yafuatayo:

1. KWAMBA Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar umeshafanyika tarehe 25 Oktoba, 2015, ambapo kwa upande wa uchaguzi wa Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi na Madiwani ulikwisha kamilika na washindi wote kupewa shahada za kuwathibitisha na kuwatambua kama washindi halali.

Kwa upande wa uchaguzi wa Rais wa Zanzibar, matokeo yalikwisha bandikwa nje ya vituo vya majumuisho vya majimbo yote 54. Kilichokuwa kinaendelea baada ya hapo ni kuhakiki matokeo hayo kutoka majimboni na kazi hiyo ilikwishakamilika kwa majimbo 40 na katika hayo, matokeo ya uchaguzi wa Rais kwa majimbo 31 yalikwishatangazwa kabla ya Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi, Jecha Salum Jecha, kutangaza isivyo halali kwamba ameufuta uchaguzi huo.

2. KWAMBA Chama Cha Wananchi (CUF) hakitoshiriki katika uchaguzi wa marudio uliopangwa kufanyika tarehe 20 Machi, 2016 kwa sababu uchaguzi huo si halali kwani uchaguzi halali ulishafanyika.

3. KWAMBA linatoa wito kwa Wazanzibari wote wanaoipenda nchi yao na ambao wanaamini katika utawala wa sheria, demokrasia na kuheshimu Katiba na Sheria za nchi yetu kutoshiriki katika uchaguzi huo usio halali wa marudio.

4. KWAMBA sababu kuu ya Baraza Kuu kufikia maamuzi haya ni kutokana na matamko yote mawili ya Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar, Jecha Salum Jecha, kutokuwa halali na kwenda kinyume na Katiba ya Zanzibar na Sheria ya Uchaguzi ya Zanzibar Nam. 11 ya 1984.

Hakuna kifungu chochote cha Katiba ya Zanzibar au Sheria ya Uchaguzi ya Zanzibar kinachotoa uwezo kwa Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar na hata kwa Tume yenyewe kufuta uchaguzi au kuitisha uchaguzi wa marudio.

5. KWAMBA linazipongeza na limetiwa moyo sana na taasisi na jumuiya zote za kimataifa na kikanda zikiwa ni pamoja na Jumuiya ya Madola (The Commonwealth), Umoja wa Ulaya (European Union), Umoja wa Afrika (African Union), Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) na Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) pamoja na nchi za Marekani na Uingereza kwa msimamo wao wa kuungana na Wazanzibari na kutetea haki yao ya kidemokrasia na maamuzi halali waliyoyafanya katika uchaguzi mkuu wa tarehe 25 Oktoba, 2015 na kutaka mchakato wa uchaguzi huo ukamilishwe na matokeo yake kutangazwa.

6. KWAMBA linazipongeza na kutiwa moyo pia na taasisi za hapa nchini zikiwemo taasisi na jumuiya za kidini, taasisi za haki za binadamu, vyombo huru vya habari, vyama vyengine vya siasa na Wazanzibari na Watanzania wote wanaopenda amani na demokrasia kwa msimamo wao wa kutetea maamuzi ya Wazanzibari waliyoyafanya katika uchaguzi mkuu wa tarehe 25 Oktoba, 2015 na kuendelea kusisitiza haja ya kuheshimu na kufuata Katiba na Sheria za nchi yetu na pia haja na umuhimu wa kutunza amani ya nchi yetu kwa kutaka haki itendeke.

Baraza Kuu linazihakikishia taasisi na jumuiya hizo zote na pia kuwahakikishia Wazanzibari na Watanzania wote kwamba CUF itaendelea kusimama kidete katika kulinda na kutetea Katiba na Sheria za nchi yetu na pia kutetea maamuzi ya Wazanzibari waliyoyafanya tarehe 25 Oktoba, 2015.

7. KWAMBA limesikitishwa na kushangazwa na kitendo cha Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi, kuandika barua na kutoa taarifa kwa vyombo vya habari kutaka vyama vya siasa vishiriki uchaguzi wa marudio uliopangwa kufanyika tarehe 20 Machi, 2016 bila ya kujali kwamba uchaguzi huo ni haramu na unakiuka matakwa ya Katiba ya Zanzibar na Sheria ya Uchaguzi ya Zanzibar Nam. 11 ya 1984.

Baraza Kuu halikutarajia mtu mwenye hadhi ya Ujaji kufanya kazi ya kutumikia maslahi ya watawala ambao wameamua kuvunja Katiba na Sheria za nchi yetu na kukanyanga misingi ya haki na demokrasia huku akishindwa kukemea uhuni mkubwa uliofanywa wa kubaka demokrasia na haki za watu.

8. KWAMBA limesikitishwa na kitendo cha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dk. John Pombe Magufuli, kukwepa dhamana na wajibu wake kama Mkuu wa Nchi na Amiri Jeshi Mkuu kwa kuiacha njiani kazi aliyoianza ya kutafuta ufumbuzi wa mkwamo wa uchaguzi Zanzibar.

Baraza Kuu linamtaka Rais Magufuli kujitathmini na kujiuliza anajiweka vipi na kutoa taswira gani mbele ya macho ya Watanzania na jumuiya ya kimataifa kutokana na kutosimamia ahadi yake aliyoitoa mbele ya Watanzania wakati akilizindua Bunge jipya kwamba atafanya kazi na vyama vya CUF na CCM ili kuupatia ufumbuzi mkwamo huu.

9. KWAMBA linalaani matumizi ya nguvu kubwa ya vyombo vya ulinzi na usalama vya Jamhuri ya Muungano na Vikosi vya SMZ dhidi ya wananchi wasio na hatia na ambao wamekuwa watulivu licha ya vitendo vingi vya uchokozi wa makusudi na hata mashambulizi ya hujuma dhidi yao yanayofanywa na makundi ya vijana wa CCM waliowekwa katika makambi kadhaa kisiwani Unguja.

10. KWAMBA linaitaka jumuiya ya kimataifa na hasa taasisi zinazosimamia haki za binadamu na zinazopambana na makosa ya jinai kimataifa ikiwemo Mwendesha Mashtaka wa Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya Jinai (International Criminal Court – ICC) kufanya uchunguzi wa kauli na matendo ya uhalifu, uvunjwaji mkubwa wa haki za binadamu na ubaguzi ambao umekuwa ukifanywa dhidi ya wananchi wa Zanzibar na kuchukua hatua dhidi ya watu walio nyuma ya maamuzi na utekelezaji wa matukio hayo.

11. KWAMBA linawapongeza wananchi wa Zanzibar kwa kuonesha ukomavu wa hali ya juu na kuwa watulivu licha ya machungu makubwa waliyoyapitia na wanayoendelea kuyapitia tokea pale maamuzi yao yalipopinduliwa na CCM kwa kumtumia Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar, Jecha Salum Jecha.

Baraza Kuu linatoa wito kwa Wazanzibari wote kuungana pamoja chini ya chama chao cha CUF walichokipa ridhaa halali kupitia uchaguzi mkuu wa tarehe 25 Oktoba, 2015 kutetea maamuzi yao waliyoyafanya kupitia sanduku la kura kwa njia za amani.

Baraza Kuu linawasisitiza tena Wazanzibari kwamba waendelee kutunza amani ya nchi yetu na kutambua kwamba kutunza amani si udhaifu bali ni jambo linaloipa nguvu jumuiya ya kimataifa kufuatilia haki za kidemokrasia za wananchi wa Zanzibar.

12. Baraza Kuu la Uongozi la Taifa linawatahadharisha CCM na watawala wasiowajali na kuwaheshimu wananchi kwamba zama za utawala wa mabavu usioheshimu Katiba na Sheria za nchi hazina nafasi tena katika dunia ya leo. Baraza Kuu lina imani kwamba HAKI ITASHINDA.

LIMETOLEWA NA:
BARAZA KUU LA UONGOZI LA TAIFA
THE CIVIC UNITED FRONT
(CUF – Chama Cha Wananchi)
DAR ES SALAAM
28 JANUARI, 2016

Thursday, 28 January 2016

VIDEO: DADA ALIYEKUTWA NDANI YA SHIMO LA CHOO KAMA MSUKULE

Nimekuwekea video hii kuonyesha baadhi ya ndugu zetu watanzania ttusivyo na utu wala huruma. Hii imetushushie heshima sana watanzania ambao daima tumeonekana watu wema na wenye roho nzuri kwetu wenyewe na majirani, na jinsi video hii imesambaa majirani wanatushangaa. Tumekumbwa na nini hadi tunawafanyia hivi wenzetu????

HALI YA SINTOFAHAMU YAENDELEA BUNGENI LEO TENA

Hali ya sintofahamu imeendelea ndani ya bunge baada ya wabunge wote wa Upinzani kutoka ndani ya bunge.

Hali hiyo imetokea baada ya Naibu Spika Tulia Mwansasu kumtaka katibu wa Bunge kuarifu bunge ratiba inayoendelea, ambapo katibu wa Bunge alibainisha kwamba kazi ya ratiba ya leo inaonyesha kwamba ni kuchangia hotuba ya Rais aliyoitoa wakati wa ufunguzi wa Bunge.

Baada ya hapo wabunge wa upinzani waliomba miongozo kutoka kwa Naibu Spika, ambapo Naibu spika alimruhusu Mbunge wa Tarime Mjini Ester Matiko.

Mbunge huyo aliuliza swali kuhusu mapungufu yaliyojitokeza kwa elimu bure kwa wanafunzi kutozwa michango katika jimbo lake.

Naibu wa spika akitoa majibu ya muongozo huo alisema kwamba serikali inatambua matatizo yanayojitokeza na inayafanyia kazi

Jambo hilo liliwakasirisha wabunge wa upinzani na kuzidi kuomba miongozo ambapo Naibu Spika aliwakataza na kuruhusu ratiba iliyo mbele ya bunge kuendelea,hali ambayo iliwafanya wabunge wa upinzani wasuse na kutoka nje.

==>Wabunge wa CCM wanaendelea kujadili Hotuba ya Rais

Wednesday, 27 January 2016

FUJO TENA BUNGENI DODOMA

Askari wa FFU walipoingia bungeni leo kuwatuliza Wabunge wa Upinzani waliokuja juu kupinga kusimamishwa kwa matangazo ya TBC live from Bungeni

HAYO YALITOKEA BAADA YA MHE WAZIRI NAPE MNAUYE KUSEMA HAYA:
"Kutokana na ufinyu wa bajeti Serikali imenuia kuzuia vipindi vya bunge kurushwa Live na Televisheni ya Taifa (TBC) isipokuwa vipindi vya maswali na majibu tu. Vipindi vingine vitarekodiwa na kurushwa kwa marudio kuanzia saa 4 usiku."- Waziri wa Habari Nape Mosses Nnauye.

MHE. ANDREW CHENGE,MWENYEKITI MPYA WA BUNGE

Mwenyekiti wa Bunge, Mtemi Andrew Chenge akiongoza kikao cha Bunge mjini Dodoma Januari 27, 2016

TUPIGE VITA KIPINDUPINDU KWA VITENDO

Halmashauri ya Manispaa ya Ilala yapiga marufuku uuzwaji holela wa bidhaa katika soko la Buguruni unaochafua mazingira ya soko na kuhatarisha afya za walaji.
Hayo yamesemwa leo na Afisa Habari wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilala David Langa wakati akifafanua kuhusu kero ya wauzaji holela wanaopanga bidhaa chini katika soko la Buguruni.
“Bidhaa zinazopangwa chini katika soko la Buguruni sio rasmi na hakuna utaratibu unaoruhusu wauzaji kufanya biashara hiyo, hivyo natoa tahadhari kwa wale wote wenye tabia hiyo kuwa ni marufuku kufanya biashara ya kupanga bidhaa chini na sio kwa soko la Buguruni tu ila katika masoko yote yaliyopo katika manispaa yetu” Alisema Langa.

DARAJA LA KIGAMBONI KUANZA KUTUMIKA MWEZI MACHI 2016

Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano sehemu ya Ujenzi Eng. Joseph Nyamhanga amesema daraja la Kigamboni litaanza kutumika kuanzia Machi mwaka huu.

Akizungumza mara baada ya kukagua hatua za ujenzi wa daraja hilo Eng. Nyamhanga amemtaka msimamizi wa ujenzi huo kuhakikisha hatua ya ujenzi iliyobaki inakamilika katikati ya mwezi februari na kuanza kazi mwanzoni mwa mwezi Machi.

“Hakikisheni Machi mosi magari yaanze kupita rasmi kwenye daraja hili na hivyo kufungua ukurasa mpya kwa wakazi wa Kigamboni ambao kwa muda mrefu wamekuwa wakikabiliwa na msongamano katika eneo la Magogoni”, amesema Eng. Nyamhanga.

Eng. Nyamhanga amesisitiza kuwa Serikali inaangalia uwezekano wa kuunganisha daraja la Kigamboni na barabara ya Charambe,Mlandizi hadi Chalinze ili kupunguza msongamano wa magari katikati ya Jiji.

Amemtaka meneja wa mradi wa ujenzi wa daraja hilo toka Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), Eng. John Msemo kuhakikisha anatafuta Wakala makini atakayesimamia na kuendesha mradi huo.

Daraja la Kigamboni lenye urefu wa mita 680, unasimamiwa na Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) na Wizara ya Ujenzi,Uchukuzi na Mawasiliano linatarajiwa kuishi zaidi ya miaka 100 na kuwa na uwezo wa kupitisha mizigo ya tani 56 zinazokubalika katika nchi za jumuiya ya madola.

IMETOLEWA NA ;
KITENGO CHA HABARI NA MAWASILIANO
WIZARA YA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO.

WAZIRI LUKUVI AAGIZA "BOMOENI JENGO HILI"

Jengo hili lililopo Mtaa wa Indira Ghandhi jijini Dar linalotakiwa kubomolewa kwakuwa limejengwa chini ya viwango
Ufa unaoonekana katika jengo hilo na hivyo kuashiria ni 'jipu'
^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^
WAZIRI wa Nyumba, Ardhi na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi amewaagiza watendaji wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilala na Shirika la Nyumba la Taifa kubomoa jengo refu lilojengwa chini ya kiwango lililopo katika mtaa wa Indira Ghandhi ndani ya mwezi mmoja kuanzia sasa.

Lukuvi ametoa kauli hiyo jijini Dar es Salaam kabla ya kuelekea kwenye ziara fupi katika Wilaya ya Bagamoyo Mkoani Pwani ambapo nako pia amebaini matatizo mbalimbali katika sekta ya Ardhi.

“Miezi sita iliyopita Rais Mstaafu alikuja hapa akaagiza jengo hili libomolewe na nyie mkajiridhisha kweli lafaa kubomolewa sasa inakuwaje mpaka leo linaendelea kuwepo? Naagiza mfanye haraka jengo hili ndani ya mwezi mmoja taratibu za ubomoaji ziwe zimeanza ili kulinusuru taifa kuingia katika janga jingine.”alisema Waziri Lukuvi.

Akiwa bagamoyo waziri Lukuvi alibaini katika Wilaya ya Bagamoyo upotevu wa viwanja vya wanachi ambavyo walitakiwa kupewa katika eneo la ukuni ambapo vimetoweka

Mara baada ya kupata taaarifa hiyo mmoja wa wakaazi wa bagamoyo ambaye alitoa malalamiko juu ya viwanja hivyo mbele ya mkutano wa hadhara na kutaja kuwa Halmashauri ilichukua kiasi cha pesa kuanzia laki sita kwa kila mtu mwaka 2005 na kuahaidi kuwapatia viwanja lakini mpaka leo hawajapewa.

Mara baada ya kupata taarifa hiyo waziri Lukuvi aliwagiza watendaji wa wilaya hiyo ndani ya miezi sita wawe wamewapatia wakazi hao viwanja hivyo.

Monday, 25 January 2016

KIKWETU KWETU

Raha yake ule kwa mkono huku umeketi chini sakafuni
Ulinzi shirikishi. Hapana chezea kitu cha Wali/Pilau

UDAKU: IDRISS SULTAN NA WEMA SEPETU SASA MAMBO HADHARANI


Nimekuwekea hapa sauti ya Idrissa ya mahojiano yake na AYO TV

ANGALISHO: BONGO MOVIES 'MNAIGIZA HADI KUIGIZA'

Nimekuwa nikijiuliza kwanini Tasnia yetu ya Bongo Movies inaonekana kusua sua katika soko la ndani na hata Kimataifa? maana ukiangalia movies tunazoangalia watanzania wengi ndani na nje ya nchi sio za nyumbani bali za mataifa mengine na kwa Afrika ni Movies za Nigeria (Nollywood). tatizo ni nini? Jibu ni rahisi sana; Bongo Movies ubunifu na umakini katika tasnia unasua sua.

ANGALIA PICHA HII HAPA CHINI........................

Huyu ni Jambazi mwenye silaha anamvamia mwanadada nyumbani kwake ili kumpora, lakini angalia miguuni kavua viatu asichafue tiles. Huo muda wa kutoka nje na kuvaa viatu atapata wapi??? Mwingine unakuta mfano ni mwanadada anamwekea mume wake sumu kwenye juice afu akishakoroga anaonja kama imekolea, inawezekanaje? Kwa haya na mengine mengi mtamshawishi vipi mtanzania apende kazi zenu?

VIDEO: MAGWANDA ALIYOVAA MHE DK. MAGUFULI YATOLEWA UFAFANUZI

Baada ya watu kadhaa kuzusha minong'ono juu ya Mavazi rasmi ya kijeshi aliyokuwa amevaa mhe Amiri Jeshi Mkuu wa Tanzania,Dk.John Magufuli alipokuwa njiani Arusha kuelekea Monduli juzi, yametolewa maelezo.


Hata hivyo nakuwekea picha za Maraisi wengine wakiwa katika mavazi hayo ili kupunguza sintofahamu
Mhe. Dk. John Magufuli-Rais wa Tanzania
Mhe.Uhuru Kenyatta-Rais wa Kenya
Mhe. Barack Obama-Rais wa Marekani
Mhe.Goodluck Jonathan-Aliyekuwa Rais wa Nigeria
Mhe.Vladmir Putin-Rais wa Urusi
mhe.Paul Kagame - Rais wa Rwanda

Saturday, 23 January 2016

UCHAGUZI ZANZIBAR KURUDIWA 20 MACHI, 2016

Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) imetangaza tarehe ya marudio ya uchaguzi visiwani humo baada ya matokeo ya uchaguzi uliopita kufutwa.

Uchaguzi huo sasa utafanyika Jumapili tarehe 20 Machi.
Tangazo hilo limetolewa na mwenyekiti wa ZEC Jecha Salim Jecha.

Jecha amesema tarehe hiyo iliamuliwa na tume baada ya mkutano hapo jana.

"Uchaguzi huo utahusisha uchaguzi wa Rais, wajumbe wa Baraza la Wawakilishi na Madiwani na hakutakuwa na uteuzi mpya wa wagombea wala mikutano ya kampeni," amesema Bw Jecha.

"Wagombea wote walioteuliwa hapo awali wataendelea kuwa wagombea katika uchaguzi huu."

AMIRI JESHI MKUU WA TANZANIA MHE.RAIS MAGUFULI KATIKA UBORA WAKE

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akisalimiana na wananchi wa Kisongo nje kidogo ya jiji la Arusha waliojitokeza kumsalimia wakati akielekea Monduli kwa ajili ya kufunga zoezi la Onesha uwezo Medani.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akizungumza jambo na Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Nchini General Davis Mwamunyange wakati waufungaji wa zoezi la Onesha Uwezo Medani lililofanyika Monduli nje kidogo ya Jiji la Arusha.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akielekea kwenye uwanja wa maonesho akiwa pamoja na Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Nchini General Davis Mwamunyange.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amefunga “Zoezi la Onesha Uwezo Medani” lililoandaliwa na kutekelezwa na Kamandi ya Jeshi la Nchi Kavu ambalo ni sehemu ya Jeshi la wananchi Tanzania katika eneo la Lang’arurusu nje kidogo ya Chuo Cha Mafunzo ya Kijeshi Monduli Mkoani Arusha.

Akizungumza na Askari na Maafisa wa Jeshi la wananchi Tanzania kabla ya kufunga zoezi hilo, Rais Magufuli amesema katika awamu yake ya tano ya uongozi amedhamiria kulitumia Jeshi la wananchi Tanzania katika kujenga uchumi, ikiwemo kuanzisha viwanda na kampuni za ujenzi ili kuharakisha maendeleo.

Ametoa mfano wa kiwanda cha Nyumbu ambacho kipo chini ya jeshi la wananchi Tanzania na kueleza kuwa wakati umefika wa kukiimarisha na kukiendeleza kiwanda hicho, ili kiweze kufanya uzalishaji mkubwa kwa manufaa ya nchi ikilinganishwa na hali ilivyo hivi sasa.

“Zipo nchi nyingi ambazo majeshi yao yanatumika katika uchumi na yanafanya kazi nzuri ya kupigiwa mfano, wakati umefika na sisi kufanya hivyo. Hata hizi sare za jeshi na viatu, hatuna sababu ya kuvinunua kutoka nje ya nchi, tunaweza kutengeneza sisi wenyewe” Alisisitiza Rais Magufuli.

Rais Magufuli amelipongeza Jeshi la wananchi wa Tanzania (JWTZ) kwa kuandaa “Zoezi Onesha Uwezo Medani” ambalo limethibitisha uwezo, weledi na utayari lilionao katika jukumu lake la kiulinzi.

Ameahidi kuwa ataendeleza juhudi zilizofanywa na viongozi wenzake waliotangulia za kuliimarisha kwa vitendea kazi na maslai ya wanajeshi ili liweze kutekeleza wajibu wake bila vikwazo.

Pamoja na kuwapongeza Askari na maafisa wa Jeshi la wananchi Tanzania walioshiriki katika zoezi hilo, Rais Magufuli ameagiza Askari Mgambo na Askari wa Jeshi la kujenga Taifa (JKT) walioshiriki zoezi hilo kuajiriwa na jeshi la wananchi Tanzania.

Akitoa maelezo ya awali kabla ya hotuba ya Rais Magufuli, Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amesema Wizara yake itaongeza na kusimamia juhudi za kuliboresha jeshi hilo kwa zana, vifaa na maslai kwa wanajeshi ili kuwajengea uwezo na morali ya kutekeleza majukumu yao ya kuilinda nchi, pamoja na kutoa msaada stahiki kwa nchi zenye kuhitaji ulinzi wa amani popote duniani.

Kwa upande wake Mkuu wa majeshi ya Ulinzi nchini, Jenerali Davis Adolf Mwamunyange amemhakikishia Rais Magufuli kuwa Jeshi la wananchi Tanzania lipo imara na litaendelea kutekeleza majukumu yake kwa weledi, nidhamu ya hali ya juu na uzalendo mkubwa.

Kabla ya kuwahutubia maafisa wa jeshi la wananchi, Askari na wananchi waliohudhuria ufungaji wa “Zoezi Onesha Uwezo Medani”, Rais Magufuli ameoneshwa zana mbalimbali za kivita ikiwa ni pamoja na kushuhudia upigaji wa mizinga ya masafa mafupi, masafa ya kati na masafa marefu.

Gerson Msigwa

Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU

Arusha

22 Januari, 2016

WIZARA YA ELIMU YAFUTA MFUMO WA "GPA" NA KURUDISHA "DIVISION"

Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako amefuta mfumo wa matokeo ya GPA kwa wanafunzi wa kidato cha nne, sita na ualimu na kurudisha ule wa zamani wa divisheni.

Mbali na hilo, Ndalichako ameagiza kuondolewa kwa mtihani wa pili (paper two) kwa watahiniwa binafsi ambao ulianza mwaka 2014.

Katika mkutano na waandishi wa habari jana, Profesa Ndalichako alisema Serikali haitawavumilia watu ambao wanataka kuchezea elimu.

“Nilitembelea Baraza la Mitihani Tanzania (Necta), Januari 7, nikaagiza wanipe sababu za msingi za kutoka divisheni kuingia GPA, hadi leo wameleta maelezo bila ya sababu za msingi na maelezo yao yamejikita katika blabla ambazo hazijitoshelezi,” alisema Profesa Ndalichako ambaye katika mkutano huo aliongozana na naibu wake, Stella Manyanya na Katibu Mkuu wa Necta, Dk Charles Msonde.

Alisema kuna mgongano mkubwa katika upangaji wa GPA kwani kidato cha nne ufaulu unaanzia 3.6 -5, kidato cha sita katika daraja hilo wanaanzia 3.7 -5 wakati ufaulu kama huo kwa mafunzo ya ualimu unaanzia 4.4 -5 ambao ni mkanganyiko mkubwa unaozalisha watu wasio na ubora wa kiwango husika.

“Baadhi ya watahiniwa waliopitia katika mfumo huo na kufaulu wanaonyesha kiwango kidogo cha maarifa kuliko kiwango cha ufaulu,” alisema.

Alisema kuwapo gredi E kwenye alama za ufaulu wakati haihesabiki katika upangaji wa GPA, kunawafanya watahiniwa waliopata E kujiona wako bora kuliko wenye D mbili na F zote ambao wanahesabiwa wamefaulu.

Alisema Necta imetoa maelezo mengi ambayo yameonekana hayana uhalisia wala wa kukamilisha sababu badala yake wamejikita katika visingizio.

Alisema Necta walimweleza kuingia katika mfumo huo ilikuwa ni maoni ya wadau lakini alipowauliza ni wadau kiasi gani na mikutano hiyo ilifanyikia wapi, hawakuwa na majibu na hakuna hata mkutano ambao uliwahi kufanyika.
“Jambo jingine lazima mkumbuke kuwa, mfumo huu haujaenda hata kwa kamishna wa elimu kupata kibali, ndiyo maana wadau waliniambia kuwa nisingetoa siku saba badala yake ningeufuta mara moja,” alisema Ndalichako.

Alipinga madai kwamba uliruhusiwa na Serikali, akisema ulianza kutumika tangu 2014 wakati maagizo ya Serikali Mtandao (EG) yalieleza kuwa kila kitu kianze kutumika Juni 16, mwaka huu.

Alisema alidanganywa kwa kuambiwa wizara iliagiza wakati amebaini kuwa wizara ilipitisha kanuni za mitihani Oktoba 28, 2015 na kuingiza katika gazeti la Serikali Novemba 6 mwaka jana ikiwa ni miaka miwili tangu mfumo wa GPA uanze kutumika.

Kwa upande wa watahiniwa binafsi, alisema kuanzia sasa hakutakuwa na mitihani miwili ambayo mmoja ulikuwa ni kwa ajili ya upimaji endelevu, hivyo watahiniwa watafanya mtihani mmoja tu.

Hata hivyo, Dk Msonde alisema watahiniwa binafsi wa sasa watasahihishiwa mitihani yao kwa mfumo wa mitihani miwili kwa kuwa walishafanya

ZIARA RASMI YA KWANZA YA KIKAZI MIKOANI YA MHE.RAIS MAGUFULI

Rais John Magufuli anatarajiwa kuwasili mkoani hapa leo kwa ziara ya kikazi ya siku mbili. Hii ni ziara yake ya kwanza tangu alipoapishwa kushika wadhifa huo Oktoba 25, mwaka jana.

Maandalizi ya kumpokea Rais yalikuwa yamepamba moto jana ikiwa ni pamoja na kupanua barabara inayoingia na kutoka makazi ya Rais jijini hapa.
Katika Ikulu ndogo ya jijini Arusha jana jioni, wafanyakazi walionekana wakiweka mazingira sawa ya kumpokea Rais ambaye atawasili mchana kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (Kia)
Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Felix Ntibenda aliwataka wananchi kujitokeza kwa wingi kumlaki kiongozi huyo.

“Tuonyeshe moyo wa upendo na ukarimu kwani mkoa huu una heshima ya kuwapokea viongozi wa kitaifa na kimataifa na ulinzi umeimarishwa kuhakikisha muda wote kunakuwa salama,” alisema Ntibenda.

Mkuu wa Wilaya ya Arusha Mjini, Fadhili Nkurlu alikagua barabara inayoelekea Ikulu ndogo huku askari polisi wakiwa doria katika barabara zinazoingia na kutoka eneo hilo.
Katika ziara hiyo, Rais Magufuli ambaye pia Amiri Jeshi Mkuu, atatembelea Chuo cha Jeshi cha TMA, Monduli ambako keshokutwa, atawatunuku kamisheni ya uofisa, maofisa wateule wa jeshi.
Iwapo Rais Magufuli atafikia Ikulu ndogo ambayo makazi ya kiongozi wa nchi anapokuwa kwenye ziara mikoani, atakuwa anatendea kazi kauli zake wakati wa kampeni za kupunguza matumizi yasiyo ya lazima.