WAZIRI MKUU
Kwa mujibu wa wasomaji hao, nafasi ya uwaziri mkuu wengi wameipeleka kwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Vangimembe Lukuvi (Mkoa wa Iringa).
“Huyu bwana ni mwenye subira, mstahimilivu, mvumilivu na mtulivu lakini pia ni mchapa kazi. Tumeona alivyoinyoosha wizara yake ya ardhi. Hata alipokuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar, alifanya vizuri. Anaweza kumsaidia rais katika ubora wake,” alisema msomaji mwingine akisema anaitwa Bakar Omar, mkazi wa Tabata Matumbi.
NISHATI NA MADINI
“Mimi naamini Wizara ya Nishati na Madini atarudishwa Sospeter Augustino Muhongo (Mkoa wa Mara). Huyu alijiuzulu uwaziri kwa kashfa ya Akaunti ya Tegeta Escrow, lakini baadaye alisafishwa kwamba hakuhusika. Akiwa kwenye wizara ile aliiweza kwa kipindi kifupi tuliona mabadiliko. Msaidizi wake awe Charles Mwijage (Mkoa wa Kagera),” alisema mama Mapunda, mkazi wa Kigogo Luhanga.
MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA KIMATAIFA
“Mimi mawazo yangu lazima Magufuli atamrejesha Benard Kamilius Membe (Mkoa wa Lindi) au atamuweka mama Asha-rose Mtengeti Migiro (atamteua) kwa sababu, Magufuli kimataifa hajulikani sana. Kwa hiyo ili mambo yake yaende vizuri, lazima atawategemea hawa kwa vile wana uzoefu na nje kwa muda mrefu.
“Migiro alishakaa Umoja wa Mataifa akimsaidia Katibu Mkuu, Ban Ki-moon. Membe yeye alikuwa waziri wa wizara hiyo kwa miaka kumi,” alisema Celina Samson, mkazi wa Ilala Boma.
WIZARA YA AFYA
“Naamini Hussein Ally Mwinyi (Zanzibar) anaiweza. Arudishwe pale kwani hata alipokuwa awali aliiweza. Lakini naibu wake anafaa sana kuwa Mbunge wa Kigamboni, Faustine Ndungulile (Mkoa wa Dar es Salaam). Huyu jamaa kwenye afya ni mkali,” alisema Joseph Hamisi, mkazi wa Temeke Sokota.
WIZARA YA UJENZI
“Hii wizara ndiyo ya Magufuli mwenyewe. Kwanza naamini ataipeleka kwenye ofisi yake. Waziri wake ataitwa waziri wa nchi ofisi ya rais, ujenzi, uchukuzi na miundombinu. Atampa Harrison Mwakyembe (Mkoa wa Mbeya). Asaidiwe na Gerson Lwenge ( mpya Mkoa wa Njombe), hawa jamaa wataiweza kwani na wao ni mchakachaka kama Magufuli mwenyewe,” alisema Kidawa Halfan, mkazi wa Kigamboni, Tungi, Dar.
MAWASILIANO SAYANSI NA TEKNOLOJIA
Mzee Salimu Jenda, mkazi wa Mikocheni: “January Makamba (Mkoa wa Tanga), naamini atarudi kuwa waziri kabisa. Lakini huyu anatakiwa kusaidiana na Hamis Kigwangala (Mkoa wa Tabora). Hii timu ikiwa pamoja mambo yataiva.”
WIZARA YA FEDHA
“Kwanza hii wizara naamini itaunganishwa na Mipango. Mwigulu Lameck Nchemba (Mkoa wa Singida) ni sahihi kwake kuwa waziri kamili badala ya unaibu kama alivyokuwa mwanzo. Asaidiwe na yule mama Angelina Mabula (mpya Mkoa wa Mwanza) ni mzuri sana. Ni mchumi na mbobezi wa mambo ya uhasibu. Wataiweza hii wizara ikiwa moja,” alisema Maua Jumanne, mkazi wa Kibamba.
WIZARA YA ULINZI
Sakina Ngalawa, mkazi wa Vingunguti: “Kwanza hii wizara iungwe na wizara ya mambo ya ndani, iwe moja tu. Magufuli alishasema ataunda baraza dogo. Anayeimudu ni Kangi Lugola (mpya Mkoa wa Mara) ni mpiganaji mzuri sana. awe waziri kamili akisaidiwa na Injinia Stella Manyanya (Mkoa wa Ruvuma)
WIZARA YA SHERIA
“Anayefaa ni Job Ndugai (mpya Mkoa wa Dodoma). Unajua yule bwana yupo vizuri sana kwenye sheria na ana misimamo. Wanasheria wote wako vile,” alisema Roman Joseph, mkazi wa Mbagala Kuu.
OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA NA URATIBU WA BUNGE
“Jamani mimi naona Nape Nnauye (mpya Mkoa wa Lindi) ndiyo anaiweza. Tumeona alivyopigania chama chake mpaka kubaki madarakani. Ni mzuri kwenye kuratibu na kusimamia sera,” alisema Anna Mmakonde, mkazi wa Msasani.
WIZARA YA ELIMU
“Jenista Joachim Mhagama (Mkoa wa Ruvuma), angetolewa kwenye sera na uratibu wa bunge awe waziri kamili wa elimu. Huyu mama ataiweza, ni mpiga kazi mzuri sana,” alisema Saimen Kimari, mkazi wa Buguruni.
Hata hivyo, haya yanabaki kuwa maoni na mtazamo wa wasomaji wetu, nafasi hizo za utumishi, zinabaki kuwa maamuzi ya rais mwenyewe kulingana na sifa zao.
No comments:
Post a Comment
Maoni yako