MGOMBEA urais kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), chini ya mwamvuli wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), Edward Lowassa, ameisimamisha tena Dar es Salaam kwa saa kadhaa huku akiwataka Watanzania kutokosa usingizi kwani hakuna kura itakayoibwa.
Lowassa alisema hayo jana jijini Dar es Salaam kwa nyakati tofauti alipokuwa kwenye mikutano ya kampeni Wilaya ya Kinondoni katika majimbo ya Kawe na Kibamba.
Akiwa katika mkutano uliofanyika katika viwanja vya Shule ya Msingi, Bunju A kwenye Jimbo la Kawe, alisema watu wasikose usingizi bali wasubiri Oktoba 25 ifike.
Licha ya kwamba Lowassa alifika Bunju saa saa 9:25 alasiri, viwanja hivyo vilianza kufurika watu kuanzia asubuhi kwani mkutano ulitarajiwa kuanza saa 5:00 asubuhi.
Hali ilikuwa hivyohivyo kwenye Jimbo la Kibamba ambako licha ya kiongozi huyo kufika katika eneo hilo saa 11:30 jioni, watu walianza kufurika asubuhi, hali iliyofanya barabara ya Morogoro kupitika kwa shida.
MSIKOSE USINGIZI
Akizungumza katika Mkutano wa Kawe, Lowassa alisema shaka dhidi ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), iliyopo sasa inatokana na jeuri ya wapinzani wao.
“Kuna maneno mengi yanasemwa kuhusu NEC... nawahakikishieni hawataiba ng’o, tuko imara, tutalinda kura zetu hadi zitakapohesabiwa.
“NEC na CCM hamtaweza kuiba kura zetu, Watanzania tukatae kuibiwa kura na kulaghaiwa,” alisema Lowassa.
Aidha Lowassa alisema kuna watu wa ofisini wanataka mageuzi, lakini wanatishwa, na wengine ni wafanyabiashara wanaotaka kutusaidia.
“Hao wanaowatisha walie tu, hawawezi kumshughulikia mtu yeyote,” alisema.
Alisema atabadilisha mfumo wa utendaji kazi wa Serikali kutoka ulivyo sasa na kuwa wa kasi. “Itakuwa ni spidi 120”, alisema.
Aliendelea kusema: “Zimebaki siku 48, tukatae msongamano wa magari Dar es Salaam, adha na tabu katika hospitali na vituo vyetu vya afya, michango ya shule za sekondari na msingi, tatizo la maji na ajira.
No comments:
Post a Comment
Maoni yako