TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amewateua wakuu wawili wapya wa mikoa kujaza nafasi zilizoachwa wazi na wakuu wa Mikoa ambao wanawania ubunge wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Taarifa iliyotolewa leo, Jumatatu, Septemba 14, 2015 na Katibu Mkuu Kiongozi (KMK), Balozi Ombeni Sefue inasema kuwa katika uteuzi wake, Rais Kikwete amemteua Ndugu Amos Makalla kuwa Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro na Ndugu Jordan Rugimbana kuwa Mkuu wa Mkoa wa Lindi.
Aidha, Rais Kikwete amewahamisha wakuu wawili wa mikoa – Ndugu Mwantumu Bakari Mahiza aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Lindi kwenda kuwa Mkuu wa Mkoa wa Tanga na Ndugu Saidi Magalula ambaye anakuwa Mkuu wa Mkoa wa Rukwa akitokea Mkoa wa Tanga.
Ndugu Magalula anachukua nafasi iliyoachwa wazi na Ndugu Stella Manyanya anayewania ubunge mkoani Ruvuma pia.
Ndugu Makalla ambaye alipata kuwa Mbunge wa Jimbo la Mvomero, Morogoro na Naibu Waziri wa Maji anachuku anafasi iliyoachwa wazi na ndugu Leonidas Gama ambaye anawania ubunge mkoani Ruvuma.
Ndugu Rugimbana ambaye alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Morogoro anakuwa Mkuu wa Mkoa wa Lindi kuchukua nafasi iliyoachwa wazi na Ndugu Mahiza. Uteuzi na uhamisho huo ulianza Jumamosi, Septemba 12, mwaka huu, 2015 na wakuu wapya wa mikoa wataapishwa kesho kutwa Jumatano, Septemba 16, 2015, Ikulu, Dar es Salaam.
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR ES SALAAM.
14 Septemba, 2015
No comments:
Post a Comment
Maoni yako