Wakati zikiwa zimebaki siku mbili kabla ya kuanza harakati za kampeni za Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba 25, mwaka huu, imedhihirika kuwa wagombea wa nafasi ya urais wakiwamo wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na wa upinzani kupitia Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), watalazimika kuwekeza zaidi nguvu zao katika mikoa tisa yenye wapigakura wengi ili kujihakikishia ushindi mapema.
Uchunguzi uliofanywa na Nipashe kwa kutumia ripoti ya Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) na Mtakwimu Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar unaonyesha kuwa mikoa hiyo tisa ndiyo inayotarajiwa kuchangia zaidi ya asilimia 50 ya kura zote na kwamba, ikitokea mgombea wa chama chochote akavuna ushindi wa asilimia 100 katika maeneo hayo, ni wazi kwamba ataibuka mshindi, hata kama atafanya vibaya katika maeneo mengine ya nchi.
Kwa mujibu wa kitabu cha makadirio ya idadi ya watu na wapigakura kilichotolewa Machi, 2015 kwa ushirikiano wa NBS na Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Zanzibar, Tanzania itakuwa na watu 48,522,228 ifikapo siku ya kupiga kura na kati ya hao, 24,253,541 ndiyo wanaotarajiwa kupiga kura. Kati yao, wapiga kura 23,533,050 ni wa Tanzania Bara na 720,491 ni wa Zanzibar.
Taarifa ya makadirio hayo iliyosainiwa na Mtakwimu Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Mohamed Hafidh Rajab na Mkurugenzi wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu, Dk. Albina Chuwa, mikoa tisa inayoonekana kuwa na wapiga kura wengi kulinganisha na maeneo mengine ni Dar es Salaam yenye wapiga kura 2,932,930, sawa na asilimia 12.09; Mbeya wapiga kura 1,477,365 (6.09%); Mwanza 1,403,743 (5.79%); Morogoro 1,264,829 (5.22%) na Kagera wapiga kura 1,264,829, sawa na asilimia 5.02.
Mikoa mingine inayokamilisha idadi ya ngome tisa muhimu za ushindi kwa wagombea urais ni Tabora inayokadiriwa kuwa na wapiga kura 1,124,167 ( 4.64%); Tanga 1,120,310 ( 4.62%); Dodoma 1,095,318 (4.52%) na Kigoma inayokadiriwa kuwa na wapiga kura 1,032,161, sawa na asilimia 4.26 ya wapiga kura wote.
Ripoti hiyo ya NBS iliyotumia uchambuzi wa taarifa za sensa ya watu na makazi ya mwaka 2012, inaonyesha kuwa jumla ya idadi ya wapiga kura katika mikoa hiyo tisa ni 12,668,211, sawa na asilimia 52.23 ya wapiga kura wote. Kwa ujumla, mikoa mingine yote nchini ikiwamo mitano ya visiwa vya Zanzibar inatarajiwa kuwa na wapiga kura 11,585,330, ambayo ni sawa na asilimia 47.77.
Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Mwaka 1977, Ibara ya 41 (6), inaeleza kuwa mgombea yeyote wa nafasi ya urais atakayepata kura nyingi dhidi ya wagombea wengine ndiye atakayetangazwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kadhalika, Sheria ya Taifa ya Uchaguzi ya Mwaka 1985 (Sura ya 343), vifungu vya 35E na 35F inatoa mamlaka kwa Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi kumtangaza mgombea aliyepata kura nyingi kuwa mshindi wa nafasi ya urais.
Katika uchaguzi mkuu uliopita 2010, waliojiandikisha kupiga kura walikuwa wananchi 20,137,303. Rais Jakaya Kikwete alitangazwa kuwa mshindi baada ya kupata kura 5,275,899 kati ya kura 8,626,283 zilizopigwa, sawa na asilimia 61.16. Waliomfuatia ni Dk. Willibrod Slaa wa Chadema aliyepata kura 2,271,885 (26.34%), Prof. Ibrahim Lipumba (CUF) kura 697,014 (8.08%), Peter Mziray Kuga wa APPT kura 96,932 (1.12%), Hashim Rungwe wa NCCR-Mageuzi kura 26,321 (0.3%), Mutamwega Mgahywa wa TLP kura 17,434 (0.20%) na Fahmi Dovutwa wa UPDP kura 13,123, sawa na asilimia 0.15
WALIOJIANDIKISHA BVR
Licha ya makadirio ya NBS na Mtakwimu Mkuu wa Zanzibar, takwimu za Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) zinaonyesha kuwa idadi kamili ya watu wenye sifa ya kupiga kura baada ya kukamilika kwa kazi ya uandikishaji kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga Kura linalotumia mfumo wa Kielektroniki (BVR) ni 23,782,558, sawa na asilimia 99.5 ya waliokadiriwa kujiandikisha. Hata hivyo, NEC bado haijatoa mchanganuo wa idadi ya waliojiandikisha kwa kila mkoa, bali imetaja baadhi ya mikoa hiyo ambayo ni pamoja na Dar es Salaam iliyoandikisha watu 2,845,256, Tabora (1,083,926), Kilimnjaro (794,556), Manyara (673,357), Kagera (1,039,268), Mara (884,985), Lindi (569,261), Ruvuma (826,779) na Mtwara watu 682, 295..
MAGUFULI, LOWASSA
Wakati kampeni zitakapoanza, mgombea urais wa CCM, John Pombe Magufuli na mgombea urais wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) anayewakilisha pia vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), Edward Lowassa, ndiyo wanaotarajiwa kuwa na mchuano mkali na hivyo haitashangaza kuwaona wakielekeza nguvu zaidi katika mikoa tisa yenye wapiga kura wengi kuliko mingine. Mbali na Chadema, Ukawa huundwa pia na Chama cha Wananchi (CUF), NCCR-Mageuzi na NLD.
Hadi sasa, tayari Magufuli na Lowassa wameonyesha kuzingatia ripoti ya NBS na Mtakwimu Mkuu Zanzibar kwani wameshatembelea baadhi ya mikoa hiyo wakati wakijitambulisha baada ya kupitishwa na vyama vyao na kuvuta umati wa watu. Baadhi ya maeneo hayo ni Dar es Salaam, Mwanza na Mbeya.
Wagombea wengine waliochukua fomu za urais ni Omari Mohamed Sombi wa AFP, Christopher Mtikila (DP), Fahmi Dovutwa (UPDP), Maxmillian Lyimo (TLP), Hashimu Rugwe (Chauma), Chief Lutasola Yemba (ADC) na John Chipaka wa Tadea.
Tanzania ina vyama vifuatavyo vilivyoandikishwa kwa msajili hadi sasa:Chama Cha Mapinduzi, CHADEMA, Civic United Front,NCCR–Mageuzi,Tanzania Labour Party, United Democratic Party,
ACT, ADC ,AFP ,CCK, CHAUMMA, CHAUSTA, DP, MAKINI, Jahazi Asilia, NLD, NRA, PPT-MAENDELEO, SAU, TADEA, UMD,na UPDP
MWAMKO KUJIANDIKISHA
Wakizungumzia mwamko wa wananchi katika kujiandikisha mwaka huu, baadhi ya wasomi wamesema hali hiyo inatokana na sababu nyingi ikiwamo ya kuzidi kuenea kwa elimu ya uraia, hasa kuhusiana na umuhimu wa kushiriki uchaguzi.
Akizungumza na Nipashe, Mhadhiri mwandamizi Idara ya Sayansi ya Siasa na Utawala Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk. Alexander Makulilo, alisema hali hiyo inaonyesha watu wamehamasishwa vya kutosha, lakini ni muhimu waliojiandikisha wakajitokeza pia kupiga kura.
Aidha, Mhadhiri Mwandamizi Idara ya Sayansi ya Siasa na Utawala Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk. Benson Bana, alisema wingi wa watu waliojiandikisha unaonyesha kuwa mwamko wa kisiasa umekuwa ukiongezeka mwaka hadi mwaka.
“Jingine ni matarajio ya kuchaguliwa rais mpya na siyo yule yule tena, kila mtu ana hamu ya kuchagua rais mpya,” alisema Dk. Bana.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment
Maoni yako