MGOMBEA Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk John Magufuli amesema akifanikiwa kuchaguliwa kuwa kiongozi wa juu wa nchi hii, atahakikisha anatekeleza ipasavyo Ilani ya Uchaguzi wa chama hicho.
Alisema hayo mjini hapa jana jioni alipokuwa akisalimiana na mamia ya wananchi, walioenda kumwona akiwa safarini kutoka nyumbani kwake Chato mkoani Geita kuelekea Dodoma. Alisema ni kwa kutekeleza kikamilifu Ilani hiyo, ndipo maendeleo ya kweli nchini yatapatikana.
Hata hivyo, alisema kuwa atahakikisha analeta maendeleo kwa watu wote bila ubaguzi wa dini, rangi, kabila wala itikadi.
“Maendeleo hayana Chama. Nikifanikiwa kuwa Rais nitaleta maendeleo kwa kila mtu... Kwa wana-Chadema, Wana-Cuf na hata kwa wale wasio na Chama,” alisema Dk Magufuli.
Aidha, alisema akifanikiwa kuwa Rais, atakuwa mtumishi wa watu na kuhakikisha anachagua serikali ya watu makini wasioonea wananchi.
“Namwomba Mwenyezi Mungu nisije kuwa Rais wa kujikweza, wa kujivuna na wa kusahau watu wangu” alisema Dk magufuli.
Dk Magufuli aliwakosha wananchi na kushangiliwa kwa nguvu pale alipotiririka kwa salamu za makabila mbali mbali nchini, kuanzia Kaskazini hadi Kusini, Mashariki hadi Magharibi mwa Tanzania “Huo ndio Utanzania wetu,” aliwaambia wananchi baada ya kumaliza na kuongeza kuwa atahakikisha anazingatia na kudumisha misingi yote mizuri, iliyoachwa na waasisi wa Taifa hili na marais waliopita.
No comments:
Post a Comment
Maoni yako